Tuesday 29 March 2016

TAARIFA YA CAG YATUA MIKONONI MWA JPM, AMUAPISHA CHIKU GALLAWA KUWA MKUU MPYA WA MKOA WA SONGWE


RAIS  Dk. John Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mkuu wa mkoa mpya wa Songwe, Luteni mstaafu Chiku Gallawa baada ya kumwapisha, Ikulu, Dar es Salaam jana.

RAIS Dk. John Magufuli akipokea ripoti ya ukaguzi wa hesabu za serikali kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Asad.
RAIS Dk. John Magufuli amepokea taarifa ya ukaguzi wa hesabu za serikali kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Taarifa hiyo yenye ripoti tano, imepokelewa ikiwa ni utaratibu wa kikatiba unaomtaka CAG kukabidhi kwa Rais, taarifa ya ukaguzi kabla ya mwisho wa
mwezi Machi.

Baada ya kupokea taarifa hiyo, taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana, mjini Dar es Salaam, ilisema Rais Magufuli ataikabidhi mbele ya Bunge katika siku saba za mwanzo za kikao kijacho cha Bunge, kitakachofanyika mjini Dodoma.

Rais Magufuli alimpongeza CAG na timu yake kwa kuandaa taarifa hiyo na ametoa wito kwa chombo hicho kuendelea kufanya kazi kwa uhuru na ufanisi, huku
akiahidi kuwa serikali itatoa ushirikiano wa kutosha kufanikisha kazi
zake.

Wakati huo huo, Rais Dk. Magufuli amemwapisha Mkuu wa Mkoa mpya wa Songwe, Luteni mstaafu Chiku Gallawa, ambaye hakuapishwa na wakuu wa mikoa wenzake
Machi 15, mwaka huu.

Uapisho huo ulifanyika jana, Ikulu, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Luteni mstaafu Chiku anakuwa mkuu wa mkoa wa kwanza kwa
mkoa mpya wa Songwe, ulioanzishwa kwa kuugawa mkoa wa Mbeya.

No comments:

Post a Comment