Tuesday 29 March 2016

POLISI WATAKIWA KUTUMIA MBINU ZA KIJESHI KUDHIBITI UJAMBAZI


KAMATI ya Bunge Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imelitaka Jeshi la Polisi kutumia mbinu za kijeshi kudhibiti ujambazi, ambao umekuwa ukitikisa jiji la Dar es Salam na maeneo mengine ya nchi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Balozi Adadi Rajabu, alisema hayo jana, baada ya kikao cha kamati hiyo, iliyokuwa ikipokea taarifa kutoka Jeshi la Uhamiaji.

Alisema wakati sasa umefika kwa jeshi hilo kutumia mbinu zake kukomesha ujambazi, hasa ule wa kuvamia benki, sehemu za biashara na vituo vya polisi.

“Hali hii ya ujambazi inatakiwa kukomeshwa ili shughuli za mabenki  na vituo vyetu vya polisi viwe salama,” alisema.

Mwenyekiti huyo, ambaye pia ni Mbunge wa Muheza, alisema kamati yake ilishakutana na Waziri wa Mambo ya Ndani na imelielekeza jeshi la polisi kuwa waangalifu wakati wote.

“Tunawataka watumie mbinu walizofundishwa na tunatambua wanajua namna ya kudhibiti vitendo hivi,”alisema.

Alisema inashangaza kuona mtu mwenye silaha anaporwa na wahalifu, ambao huzitumia kwenye shughuli za kihalifu baadae.

“Kamati inatambua kuwa kuna changamato mbalimbali zinazowakabili za kifedha, tutalifanyia kazi bungeni ili waendelee kufanya kazi zao vizuri na kwa ufanisi,” alifafanua.

Alisema baada ya kupokea taarifa ya bajeti za Wizara ya Mambo ya Ndani, Ulinzi na Mambo ya Nje, iliyotolewa mwaka jana, kuanzia Julai hadi sasa, wamegundua kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali haukufikia malengo kutokana na ufinyu wa bajeti.

“Tumebaini kuwa wizara hizi zote zimekuwa na ufinyu wa bajeti, madeni na miradi kutokamilika,” alifafanua.

Alisema kamati imezingatia changamoto zao na kwamba watazifanyia kazi bungeni.

Alitoa pongezi kwa wizara hizo kwa kutekeleza majukumu yao pamoja na ufinyu wa bajeti na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Akitoa mfano, alisema mabalozi wanafanya kazi nzuri ya kuiwakilisha nchi nje ya nchi na kuwataka kuendelea kufanya kazi hiyo kwa mafanikio ya nchi.

“Mabalozi wanafanya kazi za kidiplomasia, ambazo ni muhimu sana katika mahusiano ya kimataifa,” alisema.

No comments:

Post a Comment