Tuesday 29 March 2016

FEDHA ZINAZOTOLEWA KWA DART HAZITOSHI- BUNGE



KAMATI ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, imeeleza kutoridhishwa kwake na fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), katika kukamilisha shughuli zake.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson Rweikiza, alisema hayo jana, baada ya kamati yake kupokea taarifa ya wakala huo na kufanya ziara ya kujionea miundombinu ya mradi, mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam.

“Mradi haupati fedha kama inavoidhinishwa na bunge, fedha mnazopata hazikidhi kufanikisha miradi ya maendeleo,” alisema.

Akitoa mfano, alisema katika mwaka wa fedha 2015/16, bunge liliidhinisha sh. bilioni 4.9, lakini hadi ilipofika mwisho mwa roba ya pili, wakala ulipokea sh. milioni 464, sawa na asilimia 9.3.

Alisema kwa kuwa mradi huo unalenga kuboresha maisha ya wananchi, kuchangia uchumi na kuondoa msongamano wa magari jijini, kamati itaweka msukumo bungeni ili wakala upate fedha zote wanazopangiwa.

Awali, Kaimu Mtendaji Mkuu wa DART, Mhandisi Ronald Lwakatare, aliiambia kamati hiyo kuwa ufinyu wa bajeti inayowafikia, imekuwa ni kikwazo katika utekelezaji wa mradi huo.

“Kwa sasa tunahitaji shilingi milioni 400 kwa ajili ya kujenga uzio katika vituo vikubwa ili watu wasiweze kuingia katika mabasi bila ya kulipa nauli, lakini fedha hizo hazipo,” alisema Mhandisi Lwakatare.

Alisema mabasi ya mradi yanatarajia kuanza majaribio hivi karibuni na kwamba, kinachosubiriwa ni kukamilika kwa mfumo wa utozaji nauli kwa vile zitatozwa kupitia kadi maalumu.

Akifafanua, alisema kadi hizo zipo tayari na watalaamu bado wanazifanyia kazi, namna abiraia atakavyoweza kuitumia kwa ufanisi katika mradi huu.

Pia, alisema madereva wataanza kufanya mazoezi hivi karibuni ili yatakapoanza, wananchi waweze kusafiri bila usumbufu.

Alisema huduma ya usafiri itatolewa na mtoa huduma za mpito, Kampuni ya UDA-RT na kusimamiwa na wakala.

Alisisitiza kuwa wananchi watapatiwa elimu ya namna ya kutumia kadi  za mfumo huo wa nauli ili waweze kuwa na ufahamu wake.

Alisema mradi huo unalenga kupunguza msongamano jijini na kurahisisha maisha kwa wananchi, hivyo wabunge na serikali wajitahidi kuupatia wakala rasilimali watu na vitendea kazi vinavyotakiwa kwa wakati.

Mjumbe wa kamati hiyo na mbunge, Mwanne Mchemba alisema kamati imesikia kilio cha wakala huo cha bajeti na kwamba, watawapigania ili wananchi waweze kupata usafiri huo nafuu.

“Mradi umekamilika kwa asilimia 98 na unatakiwa kuanza kazi haraka,” alisema.

No comments:

Post a Comment