Monday 1 May 2017

WASOMI, WANASIASA WAPONGEZA KUTIMULIWA WENYE VYETI FEKI





BAADHI ya wasomi na wanasiasa nchini wamepongeza juhudi za serikali za kuwaondoa watumishi walioghushi vyeti huku wakiomba ukaguzi huo usiishie sarikalini tu bali uguse hata  taasisi nyingine.
Kauli za wasomi na wanasiasa hao zimekuja siku chache baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, kuweka hadharani majina ya watumishi walioghushi vyeti.
Baada ya kupokea ripoti hiyo kutoka kwa Waziri Kairuki, Rais, Dk. John Magufuli aliamua kuwafuta kazi watumishi wote 9,932 waliobainika kughushi vyeti.
Pia, aliagiza ifikapo Juni 15, mwaka huu, watumishi hao wafikishwe mahakamani endapo wataikaidi kujiondoa wenyewe.
Aidha, alisisitiza kuwa majina ya watumishi hao yachapishwe gazetini ili kila mmoja awafahamu.
Aliongeza kuwa, watumishi wengine 1,538, ambao vyeti vyao vina utata kwa kutumiwa na watumishi zaidi ya mmoja, wachunguzwe kwa kina ili kujua ni nani mhusika, ambaye anastahili kupata mshahara.
Wakizungumza na Uhuru kwa nyakati tofauti mjini Dar es Salaam, jana, wasomi hao walisema juhudi zinazofanywa na serikali, zinatakiwa kupongezwa kwa sababu haiwezekani watu wasio na vyeti wafanyekazi na wenye vyeti wahangaike mitaani.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Banna, alisema watumishi hao wamefukuzwa kazi, lakini kila mmoja anatakiwa kujiuliza wameingiaje serikalini.
“Lakini ni lazima twende mbali, waliingiaje ingiaje pale na hadi kuajiriwa? Na mamlaka za kudhibiti vyeti na kuvihakiki walikuwa wapi?” Alihoji.
Alisema inatia ukakasi kuona menejimenti ya rasimaliwatu haifanyikazi zake vizuri hadi kuruhusu watumishi kufanyakazi wakiwa na vyeti vya kughushi.
“Mifumo katika menejimenti ya rasilimali watu inatakiwa kusimamia suala hili vizuri ili dosari iliyojitokeza  isiweze kutokea tena,” alisema.
Pia, alishauri wale wote waliofukuzwa kazi, wapewe stahiki zao ili waweze kujikimu wanapokwenda kuanza maisha mapya.
Hata hivyo, alisema zoezi hilo lisiishie serikalini tu, bali linatakiwa kufika kwa wanasiasa, mawaziri, wabunge, wenyeviti wa mitaa, vijiji na watendaji.
Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk. Thimothy Lyanga, alisema mtu aliyeghushi cheti halafu akaenda kufanyakazi, siku zote anakuwa hana maadili ya kazi.
 “Kama umeweza kughushi cheti, hata ukienda kufanyakazi ni lazima utakuwa hauna maadili. Na hawa watu ndiyo wanaofanya kunakuwa na rushwa, maana maisha yao yanazungukwa na udanganyifu,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, aliishauri serikali kufanya zoezi hilo kuwa endelevu ili waweze kuwatambua wale wote, ambao wanaghushi vyeti na kusababisha wenye vyeti halisi kukosa kazi.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, naye ameunga mkono uamuzi wa serikali wa kuwachukulia hatua watumishi wote wa umma waliobainika kutumia vyeti feki, ikiwemo kuwafukuza kazi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

“Bila shaka hatua hii itapanda mbegu ya uwajibikaji, kuchochea uadilifu na kuhakikisha weledi kwenye utumishi wa umma,” alisema.
Aidha, alisema kauli ya Rais, Dk. John Maguli ya  kuwasamehe wale watakaojiondosha kazini wenyewe na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale watakaoendelea kubaki kwenye nafasi zao, ni kinyume cha sheria na katiba ya nchi.
“Kisheria Rais hana mamlaka ya kumsamehe mtu anayetuhumiwa kufanya kosa la jinai iwapo mtu huyo hajafikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuhukumiwa,” alisema.
Pia, aliishauri serikali kufanya mchakato huo wa vyeti ili uguse viongozi wa kisiasa wa vyama vya upinzani na CCM.

No comments:

Post a Comment