Tuesday, 4 April 2017

BUNGE LA BAJETI LAANZA DODOMA


MKUTANO wa saba wa Bunge la Bajeti, umeanza leo mjini Dodoma na unatarajiwa kumalizika Juni 30, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, mkutano huo utakuwa mahususi kwa ajili ya kupitisha bajeti ya serikali pamoja na kujadili utekelezaji wa bajeti za wizara zote kwa mwaka wa fedha 2016/17, na makadirio ya matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Shughuli nyingine zitakazofanyika kwenye mkutano huo ni kiapo cha uaminifu kwa Mama Salma Kikwete, ambaye ameteuliwa hivi karibuni na Rais, Dk. John Magufuli kuwa mbunge.

Nyingine ni bunge kufanya uchaguzi wa wabunge tisa wa Bunge la Nne la Afrika Mashariki (EALA), ambao utafanyika leo, baada ya kipindi cha asubuhi cha maswali na majibu.

"Uchaguzi huu utafanyika baada ya wabunge waliopo sasa kumaliza muda wao, ambao utaisha Juni, mwaka huu," ilisema taarifa hiyo.

Aidha, kabla ya uwasilishwaji wa bajeti ya serikali, bunge litajadili hotuba ya hali ya uchumi wa Taifa, itakayowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.

Aidha, katika mkutano huo, miswada mitatu itawasilishwa bungeni, ambayo ni Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Fedha wa mwaka 2017, Muswada wa Sheria ya Fedha mwaka 2017 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2017.

Katika mkutano huo, maswali ya kawaida 515, yanatarajiwa kuulizwa na kujibiwa bungeni.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 38 (1) ya kanuni za kudumu za bunge, wastani wa maswali 72 ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, yataulizwa na kujibiwa siku za alhamisi.

No comments:

Post a Comment