Tuesday, 4 April 2017

BUNGE LASHINDWA KUPITISHA WAGOMBEA WA UPINZANI EALA




BUNGE limeshindwa kupitisha majina ya wagombea wa ubunge wa Afrika Mashariki (EALA) wa vyama vyote vya upinzani kutokana na kutokidhi vigezo.

Kufuatia hatua hiyo, Katibu wa Bunge, Dk.Thomas Kashililah, ameviandikia barua vyama vyenye haki ya kugombea ili virekebishe mapungufu hayo na kuwasilisha majina na nyaraka zinazohitajika katika ofisi yake kabla ya leo saa 7:00 mchana.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mjini hapa jana na Dk. Kashililah, uteuzi wa wagombea hao wa vyama vya upinzani, utafanywa wakati wowote kuanzia saa 7:00 mchana, baada ya kupokea na kuchambua nyaraka zitakazowasilishwa kwake na vyama husika.

“Machi 17, 2017, nilitoa tangazo kwenye gazeti la serikali namba 376, kuhusu siku ya uteuzi na siku ya uchaguzi, kuwa Machi 30, 2017, saa 10:00 jioni kuwa ni siku ya uteuzi wa wagombea na pia Aprili 4, 2017, saa 11:00, asubuhi kuwa ni siku ya uchaguzi wa wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki,”alisema.

Alisema uteuzi  wa wagombea katika kundi C wa vyama vya upinzani, haukufanyika kutokana na mapungufu mbalimbali yaliyobainika kwenye nyaraka za uteuzi wa wagombea, ambayo yanakiuka masharti ya Ibara ya 50 ya Mkataba wa Kuanzishwa kwa Jumuia ya Afrika Mashariki.

Pia, alisema yanakiuka Ibara ya 67 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kifungu cha 4(4) cha Sheria ya Uchaguzi wa Wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki ya Mwaka 2011, iliyotungwa na Bunge la Afrika Mashariki.

Dk. Kashililah aliutaja muhtasari wa mapungufu yaliyobainishwa kwa vyama husika, ambavyo ni CHADEMA kuwa uteuzi wao hakuzingatia jinsia ili kuwezesha utekelezaji wa masharti ya kifungu cha 4(4) cha Sheria ya Uchaguzi wa Wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki, inayoelekeza angalu theluthi moja (1/3) ya wajumbe 9 ioneshe uwepo wa jinsia zote mbili.

Mapungufu mengine  ni kukosekana kwa fomu za maombi ya wagombea,   orodha ya waombaji na fomu ya matokeo ya kura.

Kwa upande wa CUF, alisema uteuzi wake pia haujazingatia jinsia ili kuwezesha utekelezaji wa masharti ya kifungu cha 4(4) cha sheria ya  uchaguzi wa wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki,  inayotaka angalau  wajumbe 9 ioneshe uwepo wa jinsia zote mbili.

Dosari nyingine ni fomu za uteuzi wa wagombea kuwasilishwa na mamlaka mbili tofauti, wagombea wawili kutokuwa na uthibitisho wa uraia na kutokuwepo kwa fomu ya uthibitisho wa hiari ya kugombea kwa wagombea wote.

Nyingine ni kukosekana kwa orodha ya waombaji kwa mgombea mmoja, fomu ya matokeo ya kura kwa wagombea wote na kutokuwepo kwa fomu ya mahudhurio kwa mgombea mmoja.

Katibu huyo wa bunge alisema, watu 505 walijitokeza kugombea, CCM ikiwa na wagombea 471, CHADEMA 17, CUF wanane, NCCR-Mageuzi watatu na ACT-Wazalendo sita.

Alifafanua kuwa wagombea hao walichujwa na vyama vyao na kupata majina ya watu 20, waliopitishwa kugombea, ambapo CCM iliwapitisha 12, CHADEMA wawili, CUF wanne, NCCR-Mageuzi mmoja na  ACT-Wazalendo mmoja.

“Kati ya wagombea hao, wanaume ni 12 na wanawake wanane, ambapo CCM-wanawake sita na wanaume 6, CHADEMA wanawake na wanaume wawili, CUF mwanamke mmoja na wanaume watatu, NCCR-MAGEUZI mwanamke mmoja na wanaume hakuna wakati
ACT-Wazalendo mwanaume mmoja huku kukiwa hakuna wanawake,"alisema.

Katibu huyo alisema majina hayo yaliwasilishwa na vyama vyao kwenye ofisi yake Machi 30, 2017, kabla ya saa 10 jioni, kama masharti ya kanuni ya 5(4) ya Nyongeza ya Tatu ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 yanavyotaka.

“Baada ya hatua hiyo, nilifanya uchambuzi wa nyaraka zilizowasilishwa ili kujiridhisha na uzingatiwaji wa masharti ya uteuzi wa wagombea kwa mujibu wa Ibara ya 50 ya Mkataba, Ibara ya 67 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Sheria ya Uchaguzi wa Wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki na Kanuni 5(1), (2) na (3) ya Nyongeza ya Tatu ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016,”alisema.

Aidha, alisema aliyagawa maombi ya kugombea katika makundi ya uchaguzi ambapo kundi A, wanawake ni Happiness Lugiko, Zainabu Kawawa (CCM), Kundi B kutoka Zanzibar ni Abdullah Hasnu Makame, Maryam Ussi Yahya, Mohamed Yusuf Nuh na Rabia Hamid Mohamedi(CCM).

Kundi C, ambalo ni vyama vya upinzani ni Ezekia Wenje na Lawrence Masha (CHADEMA), Nderakindo Kessy (NCCR-Mageuzi), Profesa Kitila Mkumbo (ACT-Wazalendo), Sonia Magogo, Habibu Mohamed Mnyaa, Thomas Malima na Twaha Taslima (CUF).

Alilitaja Kundi D, kwa upande wa Tanzania Bara kuwa ni Adam Kimbisa, Anamringi Macha, Makongoro Nyerere, Ngwaru Maghembe, Fancy Nkuhi na Happiness Mgalula (CCM).

Aliwataja wagombea waliokidhi vigezo na masharti ya kuteuliwa kugombea, ambao ni kutoka CCM kuwa ni kutoka kundi A, wanawake ambao ni Happiness Lugiko, Zainabu Kawawa huku Kundi B, kutoka Zanzibar, Abdullah Hasnu Makame, Maryam Ussi Yahya, Mohamed Yusuf Nuh na Rabia Hamid Mohamed.

Wengine  kutoka Kundi D, Tanzania Bara ni Adam Kimbisa, Anamringi Macha, Makongoro Nyerere, Dk. Ngwaru Maghembe, Fancy Nkuhi na Happiness Mgalul.

No comments:

Post a Comment