Tuesday 4 April 2017

TANZANIA, EU ZATIA SAINI MKATABA WA BIL. 490/-


MIAKA mitatu tangu kuibuka kwa sakata la Tegeta Escrow, Serikali ya Tanzania na Jumuia ya Umoja wa Ulaya (EU), hatimaye zimethibitisha bado zina mahusiano mazuri baada ya pande hizo kutiliana tena saini msaada wa miaka minne wenye thamani ya sh. bilioni 490.

Fedha hizo ni kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano (FYDP-II), unaoanza kutekelezwa kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha ya 2017/2018.

Katika hafla fupi ya kusaini mkataba huo iliyofanyika ofisi ya wizara ya fedha jijini Dar es Salaam jana, takriban mabalozi 10 wa nchi wanachama wa EU walihudhuria, wakiongozwa na Mkuu wa Ujumbe wa EU nchini, Roeland Van Der Geer.

Akizungumza kwenye hotuba yake fupi, Van De Geer alisema fedha hizo ni sehemu ya sh. trilioni 1.5 zilizoahidiwa kutolewa na EU kuanzia 2014 mpaka 2020, kwa ajili ya bajeti za mwaka wa fedha, ikitoa kipaumbele masuala ya nishati na sekta ya kilimo.

Kiongozi huyo alisema kiasi hicho cha fedha kwa awamu hii kitatolewa kwa vipindi tofauti katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka huu, ambapo kila mwaka EU itatoa sh. bilioni 120.

"Hatukatai kila urafiki una changamoto hivyo tunakubali Tanzania na EU kuna tofauti zetu ila mambo yanakwenda vizuri, ndio sababu tunatoa kiasi hiki cha fedha ili taifa hili liendelee kusimama," alisema.

Pia alisema kwenye fedha hizo, wanaendelea kufanya mazungumzo na serikali ya Rais Dk. John Magufuli, ili zitumike kuongeza nguvu kwenye ukusanyaji wa kisasa wa mapato ya serikali, wakisisitiza kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mpaka sasa imeonyesha kufanya kazi nzuri.

Vilevile alisema fedha hizo wanatamani zielekezwe kwenye kuongeza kasi ya kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma, kuboresha sera zinazoonekana kuwa na mapungufu.

Alisema Tanzania iko kwenye kasi ya kuufikia uchumi wa viwanda utakaofanya taifa liwe miongoni mwa zenye kipato cha kati ifikapo 2025, kazi ambayo ni kubwa, inayohitaji serikali kukusanya mapato ili kusaidia utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha kikamilifu.

Sambamba na hilo Balozi huyo aliongeza kuwa ni wazi kwamba miaka mitano iliyopita sekta za kisera zilikumbwa na changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa rasilimali, matumizi mabovu ya fedha yaliyotokana na usimamizi hafifu lakini EU wanaamini hali itaimarika kutokana na uongozi uliopo madarakani.

Alishauri kuwa serikali pamoja na harakati zake za kuwaletea wananchi maendeleo, iweke pia mkazo kwenye uhuru wa habari, mahusiano ya kibiashara hususan yanayoihusisha Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), ili mambo yaendelee kuwa mazuri.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Doto James, alisema Serikali inaishukuru EU kwa msaada huo wa fedha ambao kutokana na mazungumzo yaliyofanyika baina ya pande hizo, kila kitu kitakwenda vizuri.

Alisema EU imekuwa rafiki wa kudumu wa Tanzania na kwamba hiyo inadhihirika kutokana na misaada iliyopita ukiwemo wa euro milioni 300, ambao uliwasilishwa serikalini kwa wakati kwa asilimia takriban 97.

Katibu Mkuu huyo alisema kwenye yote ambayo wameshauriwa na EU, watayazingatia ikiwemo kuangalia ufikiaji wa malengo ya maendeleo endelevu (SDG), ili Tanzania iyafikie sambamba na kukamilisha malengo ya FYDP II.

Ikumbukwe kuwa baada ya kutokea kwa sakata la Tegeta Escrow, ambalo lilihusisha akaunti iliyokuwa na mamilioni ya fedha zilizodaiwa kutumiwa tofauti na makusudio, baadhi ya watu hususan wa mataifa ya nje, walidai hakuna uhusiano mzuri kati ya Tanzania na EU.

Ili kufuta dhana hiyo, EU jana walisema kuwepo kwa vipindi vya kutokuelewana miongoni mwa marafiki ni jambo la kawaida lakini EU na Serikali ya Tanzania haiwezi kuvunja urafiki kutokana na historia.
 
 

No comments:

Post a Comment