Monday 3 April 2017

MAZITO ZAIDI YAFICHUKA MCHANGA WA DHAHABU


KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, amefichua namna mabilioni ya fedha yalivyokuwa yakiibwa kutoka kwenye baadhi ya migodi ya madini nchini.

Amesema katika kufanya hivyo, makontena yasiyopungua 50,000 ya mchanga wenye madini, ikiwemo dhahabu, yalisafirishwa kwenda kuuzwa nje ya nchi kati ya mwaka 2001 hadi 2016.

Akizungumza katika semina ya siku mbili ya Makatibu wa Siasa na Uenezi wa Kata zote 102 za mkoa wa Dar es Salaam, iliyomalizika jana, Polepole alisema kwa mujibu wa sheria za kimataifa, kila kampuni ya madini inatakiwa kubainisha kiasi halisi cha mapato inayopata.

Alisema kuwa mchanga unaopelekwa nje ya nchi hauendi kuchenjuliwa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu, badala yake unauzwa kwa kampuni zingine zilizoko huko na wahusika kujipatia fedha zaidi.

Polepole alisema baadhi ya migodi nchini imekuwa ikijipatia shilingi bilioni 400,  kila mwaka, ambazo zinatokana na biashara ya kuuza mchanga wenye madini ya shaba, fedha na dhahabu nje ya nchi.

Kiongozi huyo mwandamizi wa CCM, alisema kiasi hicho ambacho ni sawa na asilimia 30, ya mapato yote, hakitolewi taarifa katika mamlaka za ukusanyaji wa kodi za serikali.

Alibainisha kuwa taasisi mbalimbali za kimataifa zilizopo nje ya nchi, ndizo zilizoinong'oneza serikali kuhusiana na suala la uporaji huo wa madini kwa kutumia udanganyifu, kisha zikaiomba ichukue hatua za haraka ili kukomesha wizi huo.

"Kwa hiyo tunaposema tunaibiwa sana madini yetu, tunamaanisha hivyo. Lazima makampuni yanayofanya hivyo sasa yajirekebishe na serikali ina haki ya kuchukua hatua stahiki," alisema.

Kutokana na hali hiyo, Polepole aliwataka makatibu wa siasa na uenezi wa kata zote nchini, kuwaelimisha wananchi ili wajue ukweli na pia wawe mstari wa mbele kutoa ufafanuzi unaohusu upotoshaji mbambali unaofanywa na baadhi ya watu.

Alisema kuwa viongozi hao katika ngazi zote, ndio wasemaji wa CCM katika maeneo yao, hivyo wanapaswa kufahamu jinsi ya kukisemea Chama katika upande wa kwanza, na pia kuyatangaza mazuri yote yanayofanywa na serikali, ukiwemo utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015/2020.

"Tunapoona mambo yanapotoshwa, sisi (makatibu wa uenezi ngazi zote), ndio tunaopaswa kutoa ufafanuzi ili kuonyesha watu ukweli," alisema na kuongeza kuwa, baadhi ya vyama vinadanganya ili kukidhi matakwa yake ya kisiasa. 

Akizungumzia kile kinachoitwa kuwa ni hali ngumu ya uchumi, Polepole alisema matatizo mengine yanasababishwa na watu wanaofanya biashara za magendo, wakwepaji wa kodi na wabadhirifu wa mali ya umma.

Alisema watu hao ndio wanaosababisha wananchi waichukie serikali, jambo linalosababisha kuwepo kwa manung'uniko na kunyoshewa kidole CCM. 

Aliipongeza serikali ya awamu ya tano kwa juhudi kubwa inazofanya kuziba mianya ya rushwa, kupambana na ufisadi na kuongeza kuwa, wanaoathirika hawawezi kuipenda.

"Hao ndio wanaokwenda wakiichafua serikali na CCM," alibainisha na kuwataka viongozi hao wa ngazi ya kata, kusimama imara na kukisemea Chama katika maeneo yao ya kazi.  

Alisema neema na utajiri wote wa nchi ni lazima utiririke kwenda kwa wananchi ili kujenga au kukarabati miundombinu kama ya barabara, viwanja vya ndege ama kuboresha sekta za afya, elimu na kuongeza kuwa, hayo ni baadhi ya mageuzi makubwa yaliyofanywa na CCM mwezi uliopita.

Polepole anakuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa kwanza wa CCM, kuwapa semina elekezi makatibu wa siasa na uenezi katika historia ya Chama, ambacho kimekuwepo madarakani kwa miaka mingi sasa.

No comments:

Post a Comment