Tuesday, 4 April 2017
DK. SHEIN: HUU SIO WAKATI WA KUPIGA SIASA VIJIWENI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka wananchi kutambue kwamba huu sio wakati wa kukaa maskani na kupeana ahadi zisizokuwepo, badala yake wafanyekazi na serikali itaendelea kuwaunga mkono.
Dk. Shein, alisema hayo mwishoni mwa wiki, katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya Mgagadu-Kiwani, mkoa wa Kusini Pemba, iliyojengwa kwa fedha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), ambapo kazi ya ujenzi ilifanywa na kusimamiwa na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kupitia Idara ya Ujenzi na Utunzani (UUB).
Katika hotuba yake kwa wananchi, Dk. Shein alisema wakati wa kupiga siasa umekwisha na kilichopo sasa ni kila mmoja kufanya kazi kwa bidii.
Alisema jukumu la kufanyakazi kwa bidii ni la kila mmoja kwa walioajiriwa maofisini na wale wanaojishughulisha na kilimo ili kujiletea maendeleo.
Rais Dk. Shein alisema uchaguzi umekwisha hadi mwaka 2020 na kuongeza kuwa, licha kwamba vyama vya siasa vipo, lakini hakuna chama kitakacholeta serikali nyingine kwa sasa.
Alimkariri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, akisema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo madarakani kisheria na imekuwa ikiwaheshimu na kuwapelekea maendeleo pale walipo.
Dk. Shein alisema kwa sasa yeye ndiye Rais wa Zanzibar na kila analolisema ana uhakika nalo kwani hana kawaida ya kusema uwongo.
Aliwaasa wananchi kisiwani humo kuendelea na shughuli zao na kutosikiliza 'tumbaku' za mitaani.
“Wananchi fanyenikazi na zingatieni maelezo ninayosema. Mbali ya mimi kuwa Rais wenu, pia ni mwenzenu na ndugu yenu. Mjue kuwa hapa hakuna serikali nyingine itakayokuja kwa kuwa serikali halali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo na itaendelea kuwepo,”alisisitiza.
Dk. Shein aliwaeleza wananchi katika hafla hiyo kuwa, barabara hiyo ni ya watu wote na waitumie kwa maslahi yao, kwani fedha zilizotumika zinatokana na kodi za wananchi wa Unguja na Pemba, huku akiwataka waitunze na kuienzi.
Miongoni mwa barabara, ambazo Dk. Shein alizitaja kuwa zimo katika ujenzi ni Ole-Vitongoji, Pujini hadi Kengeja yenye urefu wa kilomita 35, ambayo tayari imeanza kuwekwa kifusi na baadae itatiwa lami.
Alisema kwa sasa serikali ipo katika mikakati ya ujenzi wa barabara ya Chake Chake-Ziwani hadi Wete, aliyosema itajengwa kwa kiwango cha lami huku ujenzi wake ukitarajiwa kuanza muda si mrefu kutoka sasa.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Balozi Ali Karume alisifu ushirikiano mkubwa uliopo katika wizara yake, jambo alilosema ndiyo chachu ya mafanikio.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment