Monday, 13 February 2017

CCM INAPASWA KUJIPANGA VYEMA KWA AJILI YA UCHAGUZI MKUU UJAO




Na Pius Msekwa

Februari  5,  mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatimiza miaka 40 ya uhai wake. Ni jambo jema sana kwa viongozi na wanachama wote wa CCM, kutumia fursa hii kufanya tathmini ya kina juu ya nafasi halisi, au fursa halisi, tuliyo nayo katika siku za usoni, ya kuendelea kupata ushindi katika chaguzi zijazo za urais, ubunge na udiwani.

Kuzungumzia jambo  hili wakati huu ni muhimu, kwa sababu Ibara ya 5 (1) ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi, ambayo inabainisha madhumuni na malengo ya Chama chetu, imeweka wazi kwamba lengo lenye umuhimu wa kwanza kabisa kwa Chama chetu, ni:-

“Kushinda katika uchaguzi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa Tanzania Bara na Zanzibar, ili tuweze kuunda na kushika madaraka ya serikali hizo, Tanzania Bara na Zanzibar.

Maana yake ni kwamba, kwa mujibu wa Katiba ya Chama chetu,  ‘kushinda katika uchaguzi mkuu’ ndiyo kazi yenye umuhimu wa kwanza kabisa ya Chama chetu.             Ndiyo sababu nimeona ni vema kutumia fursa hii ya sherehe za miaka 40 ya kuzaliwa kwa CCM,  kukumbushia lengo hilo kuu la Chama chetu.

Nimevutika kufanya hivyo kwa sababu kubwa kwamba, kuanzia uchaguzi mkuu wa 2010, na kufuatiwa na uchaguzi  mkuu wa mwaka 2015, Chama chetu, ingawa  kwa hakika kilipata ushindi wa kutosha kukiwezesha kushika serikali zote mbili, lakini wapo wanachama  wengine walisononeka kuona kwamba, Chama chetu hakikupata ushindi wa kishindo kama ilivyozoeleka katika miaka yote ya nyuma tangu tulipoingia katika mfumo wa ushindani wa vyama vingi vya siasa. Badala yake, ushindi wetu ulishuka kidogo. 

Kwa hiyo lengo la maandalizi ya chaguzi zote zijazo, hayana budi kujielekeza katika kuupaisha tena ushindi wa Chama chetu.

Nikinukuu maneno maarufu ya Mwalimu Nyerere wakati wa vita dhidi ya nduli Iddi Amin Dada wa Uganda;  Ni kwamba UWEZO wa kupata ushindi tunao,  NGUVU ya kupata ushindi tunayo na NIA ya kupata ushindi kwa hakika tunayo.  Kwa hiyo tukidhamiria, tutaendelea  kushinda. 

Kwa nini ushindi wa Chama chetu ulishuka?
Ukweli ni kwamba ushindi wa CCM ulishuka kidogo, siyo kwa sababu nguvu ya upinzani imepanda, la hasha. Bali ni kwa sababu ya makosa yaliyofanywa na CCM yenyewe.

Kama nitakavyofafanua hapa chini, makosa hayo ndiyo yaliyosababisha baadhi ya wananchi, wainyime CCM kura katika chaguzi husika. 
Kwa jumla matokeo  hayo yalikuwa hivi:-
(a)   Idadi ya wabunge wa CCM ilipungua kutoka 206 wa  mwaka 2005 hadi 187, mwaka 2010, hali ambayo pia iliathiri mgawo wetu wa Viti Maalumu vya wanawake, ambapo idadi yao kwa upande wa CCM pia ilipungua.
(b)   Idadi ya madiwani wa CCM pia ilishuka. Na mgawo wetu wa madiwani wa viti maalumu vya madiwani wanawake,  pia ilishuka.
 (c)  Idadi ya kura za mgombea urais wa CCM vilevile ilishuka, kutoka 80.2% ya mwaka 2005 hadi 61.2% ya  mwaka 2010.                                                                                                                        

Hali hiyo ya kushuka kwa ushindi wa Chama chetu ilijirudia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ambapo mgombea urais wa CCM alipata ushindi wa asilimia 58.46% ya kura zote halali; ambao ni chini ya aslilimia 61.2%, alizozipata mgombea urais wa CCM katika uchaguzi mkuu uliotangulia wa mwaka 2010.

Kushuka huku kwa ushidi wa CCM kulisababishwa na nini?  Kwa maoni yangu, hali hiyo ya kushuka kwa ushindi wa CCM,  haikusababishwa na kuongezeka kwa nguvu ya vyama vya upinzani. La hasha. Ukweli ni kwamba ushindi wetu ulishuka kutokana na makosa yaliyofanywa na CCM yenyewe, yaliyowafanya wapigakura wengi wajenge chuki dhidi yake.

Uchambuzi wetu.

Kwa mfano, kwa upande wa ubunge, makosa mengi yalifanyika ya kuwaengua baadhi ya wagombea wa CCM waliokuwa na uwezo wa kushinda katika majimbo yao. Makosa hayo yalifanyika wakati wa mchakato wa uteuzi. Walipoenguliwa hivyo, waliachana na CCM wakahamia CHADEMA.

Wote hao waliohama kutoka CCM waliibuka washindi katika majimbo yao hayo, wakiwashinda wagombea wa CCM.  Ndiyo kusema kwamba kura ziliwafuata wagombea hao kwa sababu tu ya kufaa kwao binafsi kuwa viongozi. Haiwezekani kuwa ushindi wao ulitokana na nguvu ya CHADEMA katika maeneo hayo!  Kwa maneno mengine, huo ulikuwa ni ushindi uliotokana na nguvu ya mgombea mwenyewe, na siyo  kutokana na nguvu ya  Chama husika.

Sasa tuangalie sababu zenyewe za kushuka kwa ushindi wa CCM.  
Uchambuzi wetu unaonesha kwamba, kuna sababu za aina mbili. Kwanza zipo sababu  zilizokuwa nje ya uwezo wa Chama  na kuna sababu nyingine zilizosababishwa na makosa yaliyofanywa na Chama chenyewe. Ufafanuzi wake ni kama ifuatavyo:-

(a)  Sababu zilizokuwa nje ya  uwezo wa Chama.                                                                                           Sababu hizo ni hizi zifuatazo:-

  (i) Kuibuka kwa wimbi la chuki dhidi ya CCM.

Sababu mojawapo ya kuibuka kwa wimbi la chuki dhidi ya CCM miongoni mwa wananchi, ni ile ambayo tayari nimekwisha kuitaja, yaani  kuwa CCM imekaa madarakani mfululizo kwa muda mrefu.
 
Wapo baadhi ya watu ambao hali hiyo inakuwa ni kero kwao. Hawajali hata kama CCM inafanya kazi nzuri namna gani ya kutekeleza Ilani yake, wao wangependa iondoke tu madarakani ili kuwapisha wengine.

(ii)  Hali ngumu ya maisha ya watu.

Kutokana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi yaliyotokea duniani kote, watu wengi wamekumbwa na hali ngumu ya maisha.  Pato la wafanyakazi ni dogo na halitoshelezi mahitaji. Vijana wengi hawana ajira. Wakulima vijijini hawana soko la mazao yao, na mengine mengi.

Isitoshe, matatizo yote haya yanakuwapo wakati CCM ilikwisha kuahidi ‘maisha bora kwa kila Mtanzania ’katika Ilani yake ya uchaguzi ya miaka 2005 hadi 2010.  Kwa hiyo wapo watu wengi waliokuwa wanauliza: ‘Hayo maisha bora tuliyoahidiwa yako wapi’?  Ni dhahiri kwamba hali hii ngumu ya maisha ya watu inazaa chuki dhidi ya Chama tawala  na serikali yake. Kwa jumla, hivyo ndivyo hulka ya binadamu ilivyo.   


(b) Sababu zilizosababishwa na Chama chenyewe.

(i)  Kujiamini kupita kiasi.

Chama chetu ni cha siku nyingi, yaani ni Chama kikongwe.
Hali hii ya kuwa Chama chetu kimekaa madarakani kwa muda mrefu sana, inaweza kwa upande mmoja kukipatia faida, lakini pia kwa upande mwingine inaweza kukipatia hasara.

Upande wa faida ni kwamba kwa sababu ya kuwapo kwake madarakani kwa muda mrefu, kitakuwa kimejulikana sana kwa watu wengi;  na vilevile  kitakuwa kimejipatia uzoefu mkubwa  katika uendeshaji wa mambo ya siasa na utawala. Kwa kiwango fulani, hali hiyo ya kujulikana sana inaweza kukipatia Chama fursa nzuri ya kujipatia ushindi.

 Lakini siyo ya kutegemea sana, kwa sababu hali hiyo ya kujulikana sana inaweza tu kutasaidia, endapo itaambatana na mambo mengine mawili yafuatayo:  Kwanza, ni lazima wananchi  kwa jumla wawe wameridhishwa na utekelezaji wa shughuli zake na pia  matendo au maadili  ya viongozi wake. 

Pili, wananchi wawe wana hofu ya kufanya mabadiliko, yaani wawe  hawataki kufanya majaribio ya kuweka madarakani  Chama kingine (au muungano wa vyama vingine vya siasa). Hofu ya aina hiyo imejieleza katika methali ya kiswahili isemayo kwamba “Zimwi likujualo, halikuli likakwisha”. Kwa hiyo,  ikitokea kwamba wapigakura wametawaliwa na hofu ya aina hiyo, kweli  inawezekana watachagua kubaki na ‘zimwi ulijualo’.                                                      

Lakini  katika mazingira ya nci yetu,  itakuwa ni jambo la kujidanganya kwa Chama tawala kama CCM, endapo kitaweka matumaini makubwa na kuamini kwamba, hilo  linaweza kutokea.

Lakini  upande wa hasara ni mkubwa zaidi na ni hatari zaidi.  Kwanza, ni kwamba kwa Chama  kuwapo madarakani mfululizo kwa muda mrefu, kunaweza kuwafanya baadhi ya wananchi kuchoshwa tu na hali hiyo, wakatamani  kupata mabadiliko. Na hali hii inaweza kutokea hata kama Chama kilichopo madarakani kinafanya kazi zake vizuri ya kutekeleza Ilani yake ya uchaguzi.  Kwani watu wanaweza kusukumwa tu na hulka ya binadamu ya kukinai hali hiyo, wakataka kujaribu watawala wengine!

Hatari hii inakuwa ni kubwa zaidi pale viongozi wa Chama tawala wanaposhindwa  kuwaridhisha wananchi kwa kuwatatulia matatizo yao,  au pengine hata Chama kinapowaudhi wananchi, kutokana na matendo yasiyoridhisha ya baadhi ya viongozi wake, hususan wakigundulika kuwa wanashiriki katika matendo  maovu ya rushwa na ufisadi.

Kushuka kwa ushindi wetu katika uchaguzi wa 2010 na 2015, kunaonesha dalili  za kuanza kuchokwa kwa Chama chetu na baadhi ya wananchi. Ni kama mlio wa majogoo ya asubuhi,  ambao unapaswa kutuzindua usingizini.

(ii)               Kuwapo kwa makundi yanayohasimiana ndani ya Chama.

Hali ya kuwapo kwa makundi yanayohasimiana ndani ya Chama, pia ilichangia kwa kiasi kikubwa katika kushusha ushindi wa Chama chetu katika uchaguzi wa 2010, kwa namna mbili. Kwanza, makundi hayo yalidhoofisha nguvu ya umoja wa Chama chetu katika kushindana na vyama vingine.  Lakili pili, katika baadhi ya maeneo,  makundi hayo yalifanyiana fitina za kisiasa za kundi moja kutaka kuliangusha kundi lingine. Fitina hizo kwa hakika zilichangia katika kupunguza ushindi wa CCM katika maeneo hayo.

   (iii)    Kukosekana kwa umakini katika uteuzi wa wagombea wa Chama chetu. 

Vilevile, kulikuwapo na ukosefu wa umakini katika mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM wa ubunge na udiwani. Pale ambapo baadhi ya wagombea waliokuwa wanakubalika zaidi kwa wananchi wa maeneo yao walinyimwa uteuzi bila sababu za msingi, wakahamia vyama vya upinzani na wakajipatia ushidi dhidi ya wagombea wa CCM. 

Vitendo vya aina hii vilijenga hasira na chuki miongoni mwa wagombea hao  pamoja na mashabiki wao. Chuki hizo zilisababisha Chama chetu kukosa kura, kwani wapiga kura wengi ama hawakwenda kabisa kupigakura, au walikwenda kupigakura zinazoitwa ‘kura za hasira’ walizowapigia wagombea wa vyama vingine, kwa shabaha ya kuiadhibu CCM kwa makosa yake hayo.

(iv)  CCM kubebeshwa zigo la rushwa na ufisadi.

Suala la rushwa limekuwa ni mzigo mkubwa sana kwa Chama chetu. Pamoja na juhudi, ambazo serikali ya CCM imezifanya za kupambana na rushwa nchini, zikiwa ni pamoja na kuunda chombo mahsusi cha kupambana na kudhibiti rushwa (TAKUKURU)  na pia kutunga sheria maalumu ya mwaka 2010, kwa ajili ya kudhibiti matumizi ya fedha kwa wagombea uchaguzi;  bado wananchi wengi, hususan wa vyama vya upinzani, wanakishutumu Chama chetu  kwamba, kimeshindwa kudhibiti rushwa.
Lakini  pamoja na shutuma hizo za rushwa, kumekuwapo pia na tuhuma nyingine za ufisadi zinazoelekezwa kwa baadhi ya viongozi wa CCM, pamoja na madai kwamba Chama chetu kimeshindwa kuchukua hatua madhubuti za kuwawajibisha watuhumiwa hao wa ufisadi.  Hali hiyo imejenga chuki kwa kukifanya Chama chetu kibebeshwe lawama ya kuwa eti kinakumbatia mafisadi.

(v)  CCM kushindwa  kudhibiti makundi yake yanayohasimiana.

Mbio za urais katika uchaguzi wa mwaka 2015, zimekiumiza sana Chama chetu ndani kwa ndani; kwani makundi ya baadhi ya vigogo waliojipanga kuwania nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano, yaliwagawa vibaya sana wana-chama wetu  na kuathiri  umoja na mshikamano ndani ya Chama kwa kiwango kikubwa sana. Kwa hakika, umoja na mshikamano ndani ya Chama ni nguvu kubwa inayotuhakikishia ushindi mzuri katika mashindano na vyama vingine. Nguvu hiyo ikipungua, lazima na ushindi pia utapungua. Kwa hiyo nguvu hiyo ilipopungua katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ushindi wetu pia ukapungua.

Maandalizi kwa ajili ya kupata ushindi mnono katika chaguzi zijazo.

Kushindwa kwa Chama chetu kudhibiti mapungufu hayo yaliyotajwa, kunaweza kutafsiriwa kwamba, Chama kilijitengenezea mazingira ya kujiumiza chenyewe.
(self-inflicted injury). Kwa hiyo katika maandalizi ya chaguzi zijazo, hatuna budi  kujipanga upya.

Na  njia mojawapo  iliyo wazi kabisa ya kujipanga upya ni kuondoa zile  kasoro na mapungufu hayo, ambayo yalikiumiza Chama chetu. Kasoro hizo zilikiumiza Chama chetu  kwa sababu ndizo zilizosababisha kuibuka kwa chuki dhidi yake  miongoni mwa Jamii.  

Hata hivyo, inafurahisha kuona kwamba  mapungufu na kasoro hizo zilikwishaanza kufanyiwa kazi, kuanzia pale Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama, katika vikao vyake vya mwezi Aprili, 2011,  ilipoamua kufanya mageuzi makubwa ndani ya CCM, ambayo yalipewa jina maarufu la  ‘kujivua gamba’.  Maamuzi hayo tayari yameingizwa katika Katiba ya Chama cha Mapinduzi Toleo la 2012. Lakini ni muhimu kuzingatia kwamba, bado hayajatekelezwa, kwa sababu  yanasubiri utekelezaji wake kuanza katika chaguzi zijazo.

Maamuzi ambayo yanasubiri utekelezaji.

Maamuzi yanayosubiri utekelezaji ni haya yafuatayo, kama yalivyoandikwa katika kumbukumbu rasmi za vikao husika:-

“Utaratibu wa uteuzi wa wagombea wa CCM
wa ubunge, uwakilishi na udiwani.

“Utaratibu wa kushirikisha wanachama wote wa CCM kupigakura za maoni ni mzuri, na hakuna mawazo yoyote ya kuubadilisha. Lakini tumebaini kasoro nyingi zilizokuwapo katika mchato wa uteuzi wa wagombea wa CCM,  kwa hiyo:-
“Tumeamua kuchukua hatua, ambazo zitaondoa mwanya wa matumizi makubwa ya fedha katika uchaguzi, kwa njia zifuatazo:-

(a)   Kwamba wanachama wa CCM watakaojaza fomu za kuomba kufikiriwa kuwa wagombea wa CCM wa nafasi hizo, kwanza watachujwa, ili kupata wagombea wasiozidi watatu, ambao ndio watakaoshiriki katika zoezi la kupigiwa kura za maoni zitakazopigwa na wanachama wote wa eneo linalohusika; badala ya utaratibu uliopo sasa ambapo wale wote waliojaza fomu wanakwenda kwenye kupigiwa kura za maoni na wanachama wote.

(b)  Tumebaini kasoro nyingine katika utoaji kadi za wanachama kwa ajili ya upigaji kura za maoni; kwamba kulikuwa na kadi nyingi sana zilizotolewa kiholela tu siku chache kabla ya siku yenyewe ya kupiga kura za maoni.  Kwa hiyo, lli kuondoa tatizo hili, tumeamua kwamba itawekwa siku maalumu ya mwisho kwa ajili ya utoaji kadi kwa wanachama watakaopiga kura za maoni kwa wagombea wa CCM.

(c)  Kuhusu  kikao chenye mamlaka ya kuchuja wagombea ubunge na uwakilishi, Toleo la 2012 la  Katiba ya CCM ya 1977, imekabidhi kazi hiyo kwa Mkutano Mkuu wa Jimbo katika Ibara yake ya 63 (4) (e) inayosomeka kama ifuatavyo:
“Kupiga kura za maoni ya awali kwa waombaji wa nafasi ya Ubunge na Uwakilishi
katika Jimbo husika”.

Maana yake ni kwamba Mkutano Mkuu wa CCM wa kila Jimbo la Uchaguzi ndio utakaopiga kura za maoni kwa wagombea wote waliojaza fomu, kwa lengo la kuwachuja ili wabaki watatu tu, ambao ndio watakwenda kupigiwa kura na wanachama wote wa CCM.     

Ni vizuri Chama Cha Mapinduzi kiandae utataribu wa kutekeleza maamuzi haya, ili yaweze kutumika katika chaguzi zijazo.


piomsekwa@gmail.com  /  0754767576.











  









  

No comments:

Post a Comment