Monday, 13 February 2017

KAMISHNA DAWA ZA KULEVYA AONYA KUWA HAKUNA ATAKAYEPONA


SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kumwapisha Rogers Sianga, kuwa Kamishna  Mkuu wa  Mamlaka ya  Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, kamishana huyo ameanza kazi kwa kasi baada ya kutangaza kuorodhesha majaji na mahakimu wanaodaiwa kujihusisha na kuvuruga kesi za dawa za kulevya.

Aidha, ametangaza kusakwa na kukamatwa mara moja kwa maofisa wa serikali, waliohusika katika kusaidia kuingiza nchini viatilifu vinavyotumika katika utengenezaji wa dawa za kulevya.

Pia, ametangaza kuwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya, hatapona mtu  na kwamba vita hiyo ni endelevu.

Kamishna Sianga alitangaza hayo jana, alipokuwa akizungumza na watendaji wa mkoa wa Dar es Salaam, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), madhehebu ya dini, kamati ya ulinzi na usalama, viongozi wa kamati ya amani, vyombo vya usalama  na wawakilishi kutoka  taasisi mbalimbali.

Alisema mamlaka yake imejipanga kikamilifu katika kuendeleza vita hiyo na kwa kuanzia, itaanza kupambana na aliouita mgogoro wa baadhi ya majaji na mahakimu wasio waadilifu, ambao wamekuwa wakihusika kuvuruga kesi za dawa za kulevya.

“Kumekuwa na mahakimu na baadhi ya majaji, ambao kwa makusudi wanavuruga kesi za dawa za kulevya. Tunaandaa orodha, ambayo  tutaipeleka kwa jaji mkuu ili tuombe kuwachukulia hatua.

"Tutaanzia hapo kwa sababu kesi nyingi zinaharibika na zinachukua muda mrefu bila sababu za msingi,” alisema Sianga.

Aliongeza: “Mtu anakaa tu anadai kwa sababu  mimi ni Jaji basi  nitaamua ninavyotaka. Hatuwezi kufanya hivyo. Kuna kesi ya kilo 50 za dawa za kulevya Tanga, mtu ameachiwa, hakimu anadai eti hajaona kosa.”

Alitolea mfano kesi nyingine, ambayo mtu alikamatwa na tembe  180, akiwa amezimeza tumboni, lakini jaji alimuachia huru.

“Jaji alisema nikimuangalia tu mtu huyu, naona ana vidonda vya tumbo, namuachia. Hivi kweli jaji, ambaye hana taaluma ya udaktari, anadai eti akimwangalia mtu anaamini ana vidonda vya tumbo?” Alihoji Kamishna Sianga.

“Hakuna mtu aliye juu ya sheria. Jaji au hakimu wanapaswa kutafsiri sheria kama zilivyo. Tunaandaa orodha. Tutapitia kesi zote za dawa za kulevya  na  kesi zilizovurugwa na mtu aliyevuruga, ikiwa ni mwanasheria, jaji au hakimu tutakwenda naye,”alionya.

Kuhusu sakata la viatilifu vya dawa za kulevya,  Kamishna  huyo alimuagiza Kamishna wa Operesheni wa mamlaka hiyo, Mihayo Kagolomkela, kuwasaka na kuwakamata maofisa wote wa serikali, ambao walihusika katika kusaidia uingizaji wa viatilifu vinavyotumika kutengenezea dawa za kulevya.

“Nakuagiza kamishna wa operesheni, hawa maofisa wote wa serikali, ambao walihusika kikamilifu kusaidia kuviingiza hapa nchini viatilifu hivyo, wakamatwe mara moja na kuhojiwa,"alisisitiza.

Alisema mapambano ya dawa za kulevya yanayoendelea nchini, yataendelea kwa kasi ile ile na yatatekelezwa kwa kufuata sheria.

“Alichokianzisha  Rais Dk. Magufuli na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, tutaenda nayo hivyo hivyo. Halitasalia jiwe juu ya jiwe,”alisema.

Sianga alisema mamlaka inajua mahali mashamba ya bangi na mirungi  yalipo, hivyo hawatapepesa macho na kusisitiiza kuwa, vita hii sio ya Dar es Salaam pekee, bali ni ya nchi nzima.

Aliongeza kuwa, vita hiyo itaendana na utoaji wa elimu ya kuepuka dawa za kulevya katika  shule na vyuo ili vijana wachukie dawa  hizo.

Katika hatua nyingine, Kamishna huyo aliagiza kukamatwa mara moja kwa mtuhumiwa wa dawa za kulevya aliyemtaja kwa jina la Yusuf Kiboko.

KAMISHNA WA OPERESHENI AONYA

Kwa upande wake, Kamishna wa Operesheni wa mamlaka hiyo, Kagolomkela alisema  tayari msako wa maofisa wa serikali waliosaidia kuingiza nchini tani 21, za viatilifu vinavyohusu utengenezaji wa dawa, umeanza. 

“Pia mafaili ya  kesi mbalimbali, ambazo kwa njia moja au nyingine ziliharibiwa kwa maslahi binafsi, orodha tumekwishaiandaa ili hatua ziweze kuchukulia,”alibainisha.

Mbali na hilo, Kamishna Kagolomkela alisema msako wa waganga wakuu wa hospitali mbalimbali nchini, ambao wamekuwa wakijihusisha na kuwauzia  watumiaji wa dawa za kulevya, dawa  zinazosambazwa katika hospitali zao kwa matumizi ya kawaida, nao umeanza.

"Wapo wakuu wa hospitali wanapokea dawa hizo, lakini huziuza mitaani kwa vijana wanaotumia dawa za kulevya. Hawa tutawatafuta na kuwakamata,”alisema kamishna huyo.

Kwa upande wake, Kamishna wa Intelijensia wa mamlaka hiyo, Fredrick Kibuta, alisema vita hiyo haikusudii kuonea mtu yeyote.

“Taarifa zitakuwa sahihi dhidi ya mtuhumiwa, atakayefunguliwa mashtaka.
Kwa maana hiyo, hatupo kwa ajili ya kuonea mtu. Vita hii ni kali na inahitaji kupiganwa kweli kweli. Haihitaji kumchekea mtu. Ukimchekea adui utaumia wewe. Naomba wananchi waendelee kutuletea taarifa,” alisema.

MWANAMKE WA MIAKA 60 MBARONI

Katika hatua nyingine, Mwandishi Wetu, Solomon Mwansele anaripoti kutoka Mbeya kuwa, vita dhidi ya dawa za kulevya imezidi kupamba moto,
ambapo watu watano, akiwemo mwanamke wa miaka 60, wamekamatwa na polisi mkoani humo.

Watuhumiwa hao, akiwemo mwanamke huyo, walikamatwa kwa kujihusisha na usambazaji na uuzaji wa dawa za kulevya mkoani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, alisema Februali 11, mwaka huu, saa 2:00 usiku,  polisi walifanya msako katika maeneo ya Manga na Nsalagha na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.

Kidavashari aliwataja waliokamatwa kuwa ni Shaban Ramadhan (40), mkazi wa Uyole, Rashid Yassin (35), mkazi wa Nonde na Roda Mwambera (60).

Wengine ni Mrisho Ramadhan (22), mkazi wa Airport na Musa Kimbe (33),
mkazi wa Nonde.

No comments:

Post a Comment