Monday 13 February 2017

MAKONDA AKABIDHI MAJINA YA VIGOGO 97


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amekabidhi orodha yenye majina 97, ya wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Rogers Sianga.

Makonda amesema katika orodha hiyo aliyoikabidhi jana, yapo majina  ya watu wazito, waliojihusisha na mtandao huo kuanzia serikali za awamu ya pili, ya tatu, ya nne na ya tano.

“Kamishna leo nakukabidhi orodha ya watu wa daraja la tatu. Daraja hili ni tofauti kidogo na lile la kwanza na la pili. La pili lilikuwa na mtikisiko kidogo, lakini hili litakuwa ni zaidi,”alisema Makonda.

Aliongeza: “Hili la tatu kidogo joto litakuwa limepamba moto. Na hili linahusisha kuanzia uongozi awamu ya tatu hadi serikali ya awamu ya tano.”

Alisema kundi hilo linahusisha makundi mengi, wakiwemo wafanyabiashara wa ndani ya nchi, lakini wenye mtandao mkubwa na ule wa nje, ambao wanaweza kuingiza kilo za dawa za kulevya 200 hadi 500.

"Kwa siku cocaine inayosambazwa Dar es Salaam ni wastani wa kilo 10 hadi 15, kiwango ambacho ni kikubwa,”alibainisha Makonda.

Alisema mbali na majina ya wauzaji katika orodha hiyo, pia inahusu  watu wa kati wanaosimama baina ya wauza dawa za kulevya na viongozi au watendaji wa taasisi mbalimbali za serikali.

“Katika orodha hii wapo wengine kazi yao kubwa ni kusimama kati na kuchukua kamisheni, lakini anaweza kuwasiliana na kiongozi au mtumishi wa taasisi ili aruhusu mzigo wa dawa za kulevya kupitishwa,” alisema Makonda.

Aliongeza: “Katika orodha hii, wengine ni watoto wa viongozi wazito wanatumia nafasi hizo kuwaomba viongozi kuwafungulia milango wauzaji wa dawa za kulevya.”

Alisema orodha hiyo inahusisha wafanyabiashara wa mihadarati, ambao  jamii imekuwa ikiwasubiri kwa hamu kubwa ili kutajwa.

“Mimi staili yangu ni kuwataja hadharani, sasa sijui kamishna yeye anakuja kwa staili gani. Ila sio kwamba kukabidhi kwetu majina haya basi tumejitoa katika vita hii. Bado tutaendelea. Tuna awamu zingine nne zinakuja,”alisema Makonda.

Alisema vita hiyo itawagusa viongozi wa dini wanaotajwa kujihusisha na mtandao huo.

“Viongozi hawa  wa dini pia sitaona haya kwashughulikia. Mtikikisiko huu utakuja katika kanisa na  misikiti,”alionya Makonda.

Makonda alisema katika jiji la Dar es Salaam, kuna klabu za usiku 20, ambazo zinahusika na biashara hiyo na kwamba, baadhi ya wamiliki waliokamatwa wameanza kutoa ushirikiano.

Pia, alisema vipo vijiwe zaidi ya 107, vilivyokubuhu kwa dawa za kulevya na kwamba, mbaya zaidi yapo maeneo, ambayo kinamama wanajifanya kuuza vitumbua, kumbe wanauza kete za dawa hizo.

Aliongeza kuwa zipo bandari bubu zaidi ya 50, ambazo baadhi zinahusika kuingiza dawa za kulevya na alinyooshea kidole utitiri wa  maduka ya kubadilishia fedha, ambayo alidai mengi hutumika kutakatisha fedha.

MANJI CHINI YA UANGALIZI WA POLISI

Wakati huo huo, mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji, amebainika kuwa chini ya uangalizi wa polisi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Manji, alitolewa juzi saa 11:45 jioni, kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, akiwa  ndani ya gari la wagonjwa lenye namba za usajili DFP 6309, aina ya Toyota Land Cruiser na kukimbizwa katika taasisi hiyo.

Gazeti hili lilifika katika Taasisi ya Jakaya Kikwete jana,  ili kujua hali ya Manji, ambapo uongozi wa taasisi hiyo ulielekeza kuwa taarifa hizo zitatolewa na ofisa habari.

Alipotafutwa, ofisa habari wa taasisi hiyo, Anna Nkinda, alisema yupo safarini kutoka Dodoma na hajui chochote.

“Sijui kwa kweli kama yupo hapo. Ni vyema umtafute Mkurugenzi Mtendaji, Profesa Mohamed Janabi, kwa ajili ya kutoa taarifa sahihi za Manji,”alisema.

Profesa Janabi alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, alisema hawezi kulitolea
ufafanuzi kwa kuwa yupo chini ya uangalizi wa jeshi la polisi, hivyo sehemu sahihi ya kupata taarifa hiyo ni polisi.

Manji alishikiliwa na polisi tangu Alhamisi ya wiki iliyopita, alipojisalimisha baada ya kwenda kuitikia wito.

ASKOFU GWAJIMA, AZZAN WARIPOTI POLISI

Katika hatua nyingine, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,  Josephat Gwajima na aliyekuwa mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan, wameripoti jana kwenye Kituo Kikuu cha Polisi, Dar  es Salaam.

Askofu Gwajima na Azzan, waliripoti kituoni hapo baada ya kuachiwa kwa masharti na polisi, kuhusiana na vita dhidi ya dawa za kulevya.

Mapema, Askofu Gwajima aliachiwa Jumamosi iliyopita huku Azzan akiachiwa juzi na kuhitajika kuripoti kituoni hapo kila watakapotakiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Azzan alisema  tuhuma dhidi yake hazijaanza sasa, hivyo wananchi wanasikiliza kupitia mitandao ya kijamii.

Pia, alisema baada ya  kuripoti kituoni hapo, polisi walimchukua kwa ajili ya kumfanyia vipimo na kwenda nyumbani kwake kufanyiwa ukaguzi, lakini hakubainika na  kitu chochote.

“Watu wengi hawajui kuwa nina maadui wangapi, hivyo yawezekana mtu akaamua kutaja tu na mimi naamini kuwa watu  wengi wana chuki na mimi na maadui ni wengi kuliko marafiki,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya  Maadili, Amani ya Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madehebu  ya Dini Nchini, William  Mwamalanga, alimuelezea Askofu Gwajima kuwa  ameripoti kituoni hao kwa lengo la kuangaliwa  nidhamu yake.

Alisema katika orodha ya wachungaji  wanaotumia  dawa  za kulevya katika kamati  yake, Askofu Gwajima hakuwa  miongoni mwao na  uthibitisho ulipatikana kuwa  si  mtumiaji wa dawa hizo baada  ya kuchukuliwa vipimo.

Mwamalanga  aliwataka viongozi wa dini kuhakikisha wanakuwa  watii hasa wanapoitwa na vyombo vya  dola, ikiwa ni  pamoja na polisi pale wanapohitajika.

No comments:

Post a Comment