Monday 13 February 2017

MAJALIWA AAGIZA MAENEO YA MAGEREZA YAPIMWE

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Kamishna Mkuu wa Magereza, Dk. Juma Malewa, asimamie upimaji wa maeneo yanayomilikiwa na Magereza kote nchini na kuhakikisha yanawekewa mipaka.

Alitoa agizo hilo jana katika kikao baina ya kamishna huyo mpya na maofisa Magereza wa mikoa yote na maofisa wanaoshughulikia kilimo na viwanda, alichokiitisha ofisini kwake mjini Dodoma.

“Magereza yetu mengi yako kwenye maeneo ambayo hayajapimwa. Baadhi ya maeneo kuna migogoro kwa sababu wananchi wamejenga karibu kabisa na maeneo ya Magereza. Lazima tupime maeneo yote na kuyawekea alama mipakani ili kubainisha maeneo yetu,”alisisitiza.

Mbali ya maeneo ya Magereza, Waziri Mkuu Majaliwa alisema jeshi hilo lina mashamba makubwa, ambayo hayajapimwa hali ambayo amesema imechangia baadhi ya wananchi kulima ndani ya maeneo ya jeshi hilo.

“Natambua kuwa jeshi hili lina mashamba makubwa, lakini nayo pia hayajapimwa. Kila RPO ni mjumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wake, tumieni wapima ardhi kutoka kwenye halmashauri zenu na mhakikishe kuwa maeneo hayo yanapatiwa hati,”alisema.

Aliongeza: "Umefika wakati sasa kila gereza litambue na kuainisha fursa walizonazo ili waweze kuamua ni kwa kiasi gani wanaweza kujitegemea kwa uzalishaji. Kama ni kilimo, ufugaji au uzalishaji wa umeme, tuangalie ni kipi kinaweza kuvutia uwekezaji, lakini cha msingi zaidi ni lazima tuwe na hati za maeneo tuliyonayo."

Majaliwa alisema kuna baadhi ya magereza yalikuwa maarufu kwa kilimo, lakini hivi sasa hakuna hata moja lenye trekta na kama yapo ni moja au mawili tu.

“Sasa hivi teknolojia ya kilimo imebadilika, ni lazima tutumie zana za kilimo ili kwenda na kilimo cha kisasa," alisema.

Akizungumzia kuhusu ufugaji na uvuvi wa samaki, Waziri Mkuu aliagiza jeshi hilo litumie maofisa wake waliobobea kwenye sekta hizo, kuendeleza na kuhamisha ujuzi wao kwa wafungwa wanaotumikia vifungo ili wanapotoka gerezani, wawe na ujuzi, ambao utawasaidia kujikimu kimaisha wanaporudi kuishi uraiani.

“Nimetembelea maonyesho ya Nanenane na Sabasaba, huko nimekuta wamejenga banda la kuku juu ya bwawa la samaki. Hii ina maana kuku wanakula na kinyesi chao kinakuwa ni chakula kwa wale samaki walioko bwawani,” alisema.

Amemtaka Dk. Malewa aangalie uwezekano wa kuanzisha karakana na ujenzi kwenye kila gereza ili maofisa na wafungwa waliopo humo watumike kufanya kazi kwenye karakana hizo.

“Nimetembelea Gereza la Isanga, nikakuta kuna milango haina komeo. Kwa vile hakuna karakana, inabidi atafutwe fundi kutoka mtaani ili aje kutengeneza kitasa au komeo. Tuanzishe karakana na tuziboreshe,”alisisitiza.

Alisema uwepo wa karakana hizo ziwe ni za umeme, ujenzi au useremala, utasaidia kupunguza gharama za uendeshaji kwa jeshi la magereza kwa kuwa matengenezo madogo madogo yatafanywa na watu wa kwenye karakana badala ya kutumia watu wa nje.

“Badala ya kutegemea wazabuni, kule kwenye udongo mzuri, tafuteni vifaa mfyatue matofali ya hydraform. Kule kwenye mchanga, fyatueni ya saruji. Kuweni na matofali ya kutosha kulingana na mahitaji yenu, mtakuwa mmepunguza gharama za ujenzi wa nyumba za askari kwa kiasi kikubwa,” alisisitiza.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba; Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Tate Ole Nasha; Kamishna Jenerali wa Magereza, Makatibu Wakuu wa Wizara ya Kilimo wanaoshughulikia Kilimo na Mifugo na Katibu Mkuu wa Mambo ya Ndani.

No comments:

Post a Comment