Monday, 13 February 2017

MWANAJESHI JWTZ ANASWA NA KILO 23 ZA MIRUNGI


ASKARI wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kikosi cha 37KJ, kilichopo Pande, jijini Tanga, Koplo Rashid Mohamed, ametiwa mbaroni akiwa na kilo 23 za mirungi alizokuwa akizisafirisha  kwenye pikipiki yake maeneo ya Amboni mjini hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, SACP Benedict Wakulyamba, alisema tukio hilo lilitokea juzi, katika eneo la Amboni, wakati mwanajeshi huyo mwenye namba MT 82494, alipokuwa akisafirisha mirungi hiyo.

Kamanda huyo alisema Koplo Rashid alikuwa akiendesha pikipiki yenye namba MT 705 BNA, aina ya Cruiser, akitokea Amboni kwenda Tanga Mjini, ambako inaaminika amekuwa akiuza mirungi nyumbani kwake Mikanjuni.

"Mwanajeshi huyo inaonekana alikuwa akisafirisha mirungi hii na kuiuza kwani anakaa maeneo ya Mikanjuni, Tanga mjini. Taratibu za kisheria zimekamilika, anatarajiwa kupandishwa mahakamani kesho (leo) kwa hatua zaidi," alisema SACP Wakulyamba.

Katika hatua nyingine, Wakulyamba alisema kati ya Januari Mosi hadi Januari 31, mwaka huu, kesi zilizoripotiwa kutokana na watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya aina ya heroin na cocaine, zilikuwa 56.

Alisema jumla ya watu 52, walikamatwa wakiwa na kilo 1.2, za dawa hizo za kulevya.

Kamanda huyo alisema jeshi lake lipo makini kuhakikisha wanadhibiti makosa mbalimbali yanayofanyika mkoani humo na kuwataka wananchi watoe ushirikiano ili kufanikisha mapambano hayo.

No comments:

Post a Comment