Wednesday, 15 February 2017

MANJI NDANI YA SKENDO MPYA


MFANYABIASHARA maarufu nchini, Yussuf Manji ameendelea kupata wakati mgumu kutokana na Idara ya Uhamiaji nchini, kukuta raia 25 wa kigeni wakiwa wameajiriwa katika Kampuni ya Quality Group, wakati hawana vibali vya kufanyia kazi.

Kutokana na hali hiyo, idara hiyo imesema itamfikisha mahakamani mfanyabiashara huyo, kwa tuhuma za kuwaajiri wageni, ambao hawana vibali, ambapo wasaidizi wake wawili wametiwa mbaroni kwa upelelezi zaidi.

Kamanda wa Idara ya Uhamiaji mkoa wa Dar es Saalam, John Msumule, alisema jana, kuwa idara hiyo imebaini uwepo wa wafanyakazi hao wasio na vibali baada ya kwenda kwenye ofisi hizo Februari 10, mwaka huu.

“Baada ya kwenda katika ofisi hizo, tulikuta wafanyakazi wa kigeni 128, ambao kati yao, 25 tulikuta hawana vibali vya kuwaruhusu kufanya kazi nchini,” alisema.

Aliongeza kuwa, kwanza walianza kutafuta hati za kusafiria za wafanyakazi hao, ambao ni raia wa India na kuanza kuzichambua, ambapo walikuta hati 25, zina makosa kwa kukosa vibali vya kufanyakazi hapa nchini.

Msumule alisema kutokana na hali hiyo, waliamua kuwatia mbaroni wasaidizi wawili wa mfanyabiashara huyo, Vikranand Sharam na Smithe Vikran, kwa ajili ya upelelezi zaidi.

Ofisa huyo alisema baada ya kubaini hilo, waliamua kumfuatilia Manji ili waweze kumkamata na kumweka mahabusu, lakini walipata taarifa kuw amelazwa hospitali.

“Lazima niseme ukweli kuwa, wote tunaowashikilia hatutawapeleka mahakamani peke yao, bali tutamuunganisha na mwajiri wao kujibu kosa linalowakabili,” alisema.

Kamanda huyo alimtaka mfanyabiashara huyo atakapopata taarifa, afike kwenye ofisi hizo haraka iwezekanavyo, ili aweze kupelekwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

“Katika kesi hiyo, hatutajali cheo cha mtu wala fedha zake na tutamuunganisha na wafanyakazi wake kwa kuwaajiri watu wasiokuwa na vibali,”alisisitiza.

Msumule alisema mtu yeyote atakayekiuka sheria, atakamatwa na kuwekwa ndani ili kujibu mashitaka bila kujali cheo cha mtu katika suala hilo.

Akizungumzia wafanyakazi hao wa kigeni waliokutwa kwenye kampuni hiyo, Msumule alisema kati ya wageni hao 128, 103 walikutwa na vibali huku 25, wakiwa hawana vibali vya kufanyia kazi, ambapo kundi hilo kubwa ni raia wa India.

Alisema waliamua kuwakamata wasaidizi hao wawili, ambao ndio wenye dhamana ya kuhifadhi hati za kusafiria na vibali hivyo, kutokana na kutoa taarifa kwamba, hawako Dar es Salaam, wako Arusha, kwa nia ya kukwamisha ukaguzi huo.

Kamanda Msumule alisema katika kufanya ukaguzi kwenye ofisi ya Manji, ilidaiwa hati hizo na vibali vya kufanyia kazi zimehifadhiwa na wasaidizi wake hao wawili waliodai wako Arusha, kwa kuwa ndio wenye funguo.

Katika hatua nyingine, taarifa zilizopatikana jana kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kitengo cha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, ambako Manji amelazwa, zinasema hali yake inaendelea vizuri.

Ofisa Habari wa Taasisi hiyo, Anna Nkinda, alisema jana kuwa, hali ya Manji inaendelea vizuri.

Wakati huo huo, Kamanda huyo alisema idara hiyo imefanya ukaguzi kwenye kampuni nyingine kadhaa, zikiwemo Luck Spin, iliyoko kwenye jengo la Diamond Plaza na kuwakamata wageni tisa wakiwa hawana vibali vya ukazi.

Aliwataja raia hao wanaoshikiliwa kuwa ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Lel Hostan, raia wa Taiwan, Lin Hui Yu (Taiwan), Ming Bao (China), Hartono (Indosea), Chenchin Hao (Taiwan), Yu Chin Hui (Taiwan), Melky (Indosea) na Lin Piao Yu (Taiwan).

Kamanda huyo alisema wageni hao wamelipishwa faini na kurudishwa nchini mwao kutokana na kuwa, wanatumia vibali vya muda mfupi vya biashara kinyume na utaratibu.

Kampuni nyingine, ambayo imefanyiwa ukaguzi ni ya ulinzi ya Alpha Romeo, ambayo mwajiri wake anatambulika kwa jina la Beatrice Samson Malemo, aliyemwajiri Vingstone Gausi, raia wa Malawi.

Msumule alisema kuna baadhi ya raia wa kigeni, ambao walikamatwa kutokana na kosa la kufanyakazi bila kuwa na kibali cha ukazi, akiwemo Chen Kuo Ching, ambaye alilipa faini.

No comments:

Post a Comment