Wednesday 15 February 2017

MAKAMANDA WA POLISI WATAKIWA KUKAZA BUTI


JESHI la Polisi limewaagiza makamanda wa polisi wa mikoa yote nchini, kuongeza nguvu ya mapambano katika oparesheni dhidi ya dawa za kulevya.

Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, Dar es Salaam, Advera Bulimba, ilisema hatua hiyo imechukuliwa ili kuhakikisha biashara haramu ya dawa za kulevya inakomeshwa hapa nchini.

"Jeshi la Polisi nchini limetoa maelekezo kwa  makamanda wa polisi katika mikoa yote, kuongeza nguvu za operesheni katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya, kwa kuwakamata wanaotumia, wanaouza na wanaosafirisha," alisema Advera.

Aliongeza kuwa makamanda wote wameagizwa pindi wanapoendesha operesheni dhidi ya dawa za kulevya, kutokuangalia sura ya mtu, cheo, wadhifa wala nafasi aliyonayo katika jamii.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limekemea tabia ya baadhi ya watu wanaokusanyika katika vituo vya polisi, pindi baadhi ya watuhumiwa wa makosa mbalimbali wanapotakiwa kufika kwenye vituo hivyo kwa ajili ya kuhojiwa kuhusiana na tuhuma zinazowakabili.

"Ni marufuku kwa mtu ama kikundi chochote kukusanyika katika kituo cha polisi bila ya kuwa na sababu ya msingi na watakaobainika watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria," alisisitiza Advera.

Alisema Jeshi la Polisi nchini linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, zikiwemo za watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na taarifa hizo zitafanyiwa kazi kwa siri ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa katika hali ya usalama.

No comments:

Post a Comment