Wednesday, 15 February 2017
RPC ILALA ATOA USHAHIDI KESI YA TUNDU LISSU
NA FURAHA OMARY
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni, amepanda katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kutoa ushahidi kwenye kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) na wahariri wa gazeti la MAWIO.
Hamduni ameieleza mahakama kuwa, gazeti hilo lilichapisha habari iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Machafuko yaja Zanzibar’, ambacho kilileta hofu na kuamsha mihemko ya wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Ofisa huyo wa polisi, mwenye cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi, alidai hayo jana, mahakamani hapo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi hiyo inayomkabili Lissu na wenzake watatu.
Mbali na Lissu, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la MAWIO, lililofungiwa na serikali kwa muda usiojulikana, Simon Mkina, mwandishi Jabir Idrisa na mchapishaji kutoka Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama kuchapisha chapisho la uchochezi, kuchapisha habari ya uchochezi yenye kichwa cha habari ‘Machafuko yaja Zanzibar’ kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002, makosa ambayo wanadaiwa kuyatenda kati ya Januari 12 na 14, mwaka huu.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, Hamduni alidai amekuwa kamanda wa polisi wa mkoa huo, tangu Mei, 2016 na kabla ya hapo, alikuwa Naibu Mkuu wa Upelelezi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, cheo ambacho alikuwa nacho kuanzia Desemba,2015 hadi alipoteuliwa kuwa kamanda.
Alidai Januari 14, 2016, akiwa ofisini kwake, alipokea taarifa za uhalifu na matishio ya usalama kutoka kwa wakuu wa upelelezi wa mikoa mitatu ya kipolisi ya kanda hiyo, juu ya uwepo wa mikusanyiko isiyo rasmi katika maeneo yanapouzwa magazeti.
Shahidi huyo alidai alielezwa kwamba, watu walikuwa wakijadili kwa mihemko kwamba, kuna machafuko, ambayo yatatokea Zanzibar, hivyo alimjulisha Mkuu wa Upelelezi wa kanda hiyo na kitengo cha upelelezi, ambapo makao makuu ya polisi walimpa taarifa kwamba hali kama hiyo ilijitokeza Zanzibar.
“Nilitafuta gazeti la MAWIO ili kusoma kilichoandikwa kuona kama kuna taarifa zozote zinazoamsha uchochezi, hofu au hali yoyote. Niliposoma ukurasa wa kwanza, kulikuwa na kichwa cha habari ‘Machafuko yaja Zanzibar’, ambacho chenyewe kilikuwa kinaleta hofu, hivyo nikafungua jalada la uchunguzi kuona kama kuna jinai.
“Nilifikia uamuzi huo, baada ya kusoma habari hiyo katika ukurasa wa tatu na wa nne, ambako nako niliona kuna baadhi ya maneno yanaweza kuleta mihemko na kuanzisha chuki na hofu kwa jamii nzima dhidi ya serikali yao Zanzibar,” alidai.
Alidai baada ya jalada kufunguliwa, aliteua maofisa wawili wa upelelezi ili waendelee kufanya upelelezi, kukusanya ushahidi na mwisho wa siku wapeleke jalada kwa mwanasheria wa serikali, kuona kama kuna jinai, ambapo hatimaye washitakiwa walikamatwa na kufikishwa mahakamani.
Baada ya shahidi huo kumaliza kutoa ushahidi wake kwa upande wa Jamhuri, mawakili wa utetezi, Peter Kibatala, Jeremiah Ntobesya, wakili wa mshitakiwa Mehboob na wa mshitakiwa Lissu, walianza kumhoji maswali kamanda huyo wa Polisi.
Wakati akihojiwa na upande huo wa utetezi, shahidi huyo alidai gazeti hilo lilikuwa likiuzwa Tanzania Bara na Zanzibar na kwamba, hana takwimu sahihi za nakala za gazeti zinazosambazwa.
Pia, alidai kwa upande wa hali ya mikusanyiko Zanzibar, taarifa alizipata kutoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman. Alidai habari hiyo kwenye gazeti ilikuwa imeandikwa na Jabir.
Aidha, alidai kichwa cha habari chenyewe chatosha kuleta hofu na kwamba, sehemu kubwa ya habari hiyo ilikuwa inahusisha mahojiano baina ya mwandishi na Lissu.
Wakati Lissu akimhoji shahidi huyo, kuliibuka mabishano ya kisheria, ambayo upande wa Jamhuri ulipinga hoja na hakimu baada ya kusikiliza, kuamua kuahirisha shauri hilo hadi leo kwa uamuzi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment