Thursday, 13 October 2016

MJI WA DODOMA LAZIMA UPANGWE - WAZIRI MKUU


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema mji wa Dodoma ni lazima upangwe ili uwe tofauti na miji mingine hapa nchini.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana, alipozungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Moladi Tanzania, Abeid Abdallah, ambaye alikutana naye kueleza nia yake ya kutaka kujenga nyumba za watumishi mkoani Dodoma.

Alisema serikali imeamu iwe hivyo kwa sababu haitaki kurudia makosa yaliyofanyika kwenye miji mingine.

“Katika kuupanga ule mji, ni lazima uwe kama ambavyo miji mingine mikuu duniani inapangwa.

"Kila eneo kutakuwa na nyumba za aina fulani. Hatuwezi kuachia watu wajenge popote na wanavyotaka. Mji unakuwa haupangiki na hilo ndilo kosa lililofanyika kwenye miji mingine mikubwa, ambayo tunayo kwa sasa nchini,” alisema.

Waziri Mkuu alisema kamati ya kitaifa ya maandalizi ya kuhamia Dodoma, imepewa jukumu la kupitia upya, master plan ya mji wa Dodoma na kuainisha maeneo, ambako nyumba za aina mbalimbali zitajengwa.

Alitumia fursa hiyo kuikaribisha kampuni hiyo ya ujenzi ili ielekeze nguvu zake Dodoma, ambako kuna mahitaji makubwa ya nyumba za watumishi.

“Kimsingi tunataka tuanze kujenga miji iliyopangiliwa na Dodoma tunataka uwe wa mji kwanza kuujenga vizuri kwa standard ya sasa.

"Kutakuwa na nyumba za ghorofa katika maeneo fulani na nyumba za kawaida katika maeneo fulani, Mkurugenzi wa CDA amekwisha andaa ramani rasmi,”  alisema.

Akizungumzia ujenzi kwenye maeneo, ambayo tayari wananchi wanaishi, Waziri Mkuu alisema serikali itaweka utaratibu ili kuwe na mikataba baina ya mwekezaji na mwananchi anayemiliki eneo husika ili asinyimwe haki ya kumiliki eneo lake.

“Kama tutahitaji eneo, ambalo tayari lina makazi, taratibu zetu ni zilezile kwamba tutaweka mikataba kati ya mwekezaji na mwananchi,"alisema.

Alisema katika utaratibu huo, kama mwekezaji atataka kujenga kwenye eneo lile, lazima amhusishe mwenye eneo na kama atataka kujenga ghorofa ni lazima ahakikishe mwenye eneo anapata umiliki kama ilivyofanyika eneo la Magomeni, Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mkurugenzi huyo alimweleza Waziri Mkuu kwamba, wako tayari kushirikiana na serikali katika zoezi la serikali kuhamia Dodoma, kwa lengo wa kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini kupata makazi bora ya kudumu.

Alimweleza Waziri Mkuu kuwa nyumba ya vyumba vitatu vya kulala, yenye sebule, jiko, stoo na choo inatosha eneo la mita za mraba 94.

“Kati ya vyumba hivyo vitatu, kimoja ni master, pia kuna sebule, chumba cha kulia na kibaraza.

"Hii inaanzia shilingi milioni 35 hadi milioni 41, kutegemea na aina ya vifaa unavyoweka kwenye umaliziaji, lakini tukiongeza na servant quarter, utalazimika kulipia shilingi milioni saba, ambapo unapata vyumba viwili, choo na bafu ndani,” alisema.

Mkurugenzi huyo aliongeza: "Kimsingi ni lazima tutaweka madirisha, milango, vyoo, masinki ya bafuni na jikoni, tiles ambazo mtu anaruhusiwa kuchagua kati ya za China, Italia au Hispania."

Akifafanua kuhusu nyumba yenye vyumba viwili vya kulala, Abdalla alisema nayo itakuwa na sebule, jiko, stoo na choo kimoja na inatosha eneo la mita za mraba 54.

Gharama za nyumba hizo alisema  zitaanzia sh. milioni 20 hadi 25, kutegemeana na aina ya vifaa vinavyowekwa kwenye umaliziaji.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, ujenzi wa nyumba moja unachukua wiki sita na kama viwanja viko eneo moja au jirani, wanaokoa muda wa siku tatu hadi tano kwa kila nyumba.

“Tunajenga ukuta kwa kumwaga theluji isiyochanganywa na kokoto, ambayo ni mchanganyiko wa saruji, mchanga na kemikali. Theluji yetu inakauka baada ya saa saba na ukuta wetu ni imara mara nne zaidi ya ukuta uliojengwa na tofali la zege," alisisitiza.

Alisema teknolojia yao, ambayo inapunguza gharama za ujenzi kwa asilimia 40, inawezesha ukuta wa nyumba nzima kukamilika ndani ya siku sita huku pia ukistahimili matetemeko na vimbunga.

No comments:

Post a Comment