Saturday, 29 August 2015

BORAFYA: LOWASSA KAPOTEA NJIA


Na Rashid Zahor

LINAPOTAJWA jina la Borafya Silima Juma katika visiwa vya Zanzibar, picha itakayokujia moja kwa moja ni ya mwanasiasa mkongwe na machachari, ambaye ni kipenzi cha viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ni mwanasiasa anayeifahamu vyema historia ya Chama cha Afro Shiraz (ASP), ambacho baadaye kiliungana na TANU na kuunda CCM.

Ni mwanasiasa anaiyefahamu vyema hali ya kisiasa visiwani Zanzibar, nini wana-CCM wanataka na nini cha kuzungumza nao na kwa wakati gani. Kwa ujumla, Borafya ni miongoni mwa 'majembe' ya CCM katika medani ya kisiasa.

Borafya, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini, ni miongoni mwa makada waliokuwa wakimuunga mkono Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Riichmond, Edward Lowassa, aliyekuwa miongoni mwa makada 42 wa CCM waliotangaza nia ya kuomba kuteuliwa kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

Hata hivyo, baada ya Lowassa kujitoa CCM na kujiunga na Chadema, Borafya na wenyeviti wenzake wa CCM wa mikoa mitano ya Unguja, waliokuwa wakimuunga mkono kada hiyo, wameamua kuachana naye na kujikita zaidi katika kutetea maamuzi yaliyofikiwa na vikao halali vya Chama katika kufanya mchujo wa wagombea.

Akizungumza na Uhuru mwishoni mwa wiki iliyopita, Borafya ameuelezea uamuzi wa Lowassa, kujitoa CCM na kujiunga na Chadema, kuwa umetokana na kutofuata na kuheshimu ushauri wa wenzake.

            LOWASSA KAPOTEA NJIA

Alisema iwapo Lowassa angeamua kubaki CCM baada ya jina lake kukatwa na Kamati Kuu ya CCM wakati wa mchujo wa wagombea  walioomba nia ya kuteuliwa kuwania urais, angeendelea kuwa na heshima kubwa ndani ya Chama.

"Tatizo lake alishakuwa na fikra kwamba kwa vyovyote vile na kwa lolote lile, lazima awe rais, hili haliwezekani. Vipo vitu duniani unaweza kuvilazimisha vikafanyika kama vile kujenga nyumba, kununua gani na vinginevyo, lakini maamuzi ya nani awe rais yanafanywa na Mwenyezi Mungu,"alisema.

Borafya alisema CCM imekuwa ikiteua wagombea wake wa nafasi mbalimbali kwa kufuata taratibu, kanuni na katiba na kwamba vikao vyenye maamuzi hayo ni vya mwisho na vinapaswa kuheshimiwa.

"Hivi ndivyo vitu vinavyokifanya Chama kidumu. Ukiwa muumini wa chama, lazima ukubaliane na maamuzi ya vikao hivyo. Hapo utaitwa muumini na mwanachama safi kwa sababu hautakuwa na doa.

"Usipokuwa na imani hiyo, utaitwa mchawi au mwanga kwa sababu huna imani. Binadamu yoyote ukiwa na busara, siku zote utatoa maamuzi sahihi. Mwenye kusubiri siku zote hajuti.

"Alisubiri sana tangu alipojiuzulu uwaziri mkuu. Alipoonyesha nia, wengi tulimpenda na kuwa tayari kumuunga mkono, lakini bahati mbaya uvumilivu umemshinda mwishoni.

"Na tena ni bora angekwenda kwenye chama kingine chochote, tungesema afadhali. Lakini huko alikokwenda Chadema ni chama kilichokuwa kikimkashifu na kumtolea maneno ya matusi na aibu ya kumwita fisadi. Hao ndio waliomtia dosari kubwa sana wakati wa mchakato,"alisema.

Borafya alisema yeye na viongozi wenzake wa CCM wa mikoa mitano ya Unguja waliokuwa wakimuunga mkono Lowassa, wameamua kubaki ndani ya Chama na wako tayari kufanyakazi ya kumnadi mgombea aliyepitishwa Dk. John Magufuli ili aweze kushinda kwa kishindo uchaguzi mkuu ujao.

"Tutahakikisha tunafanya kampeni nzito kwa ajili ya Dk. Magufuli, Samia (Suluhu Hassan-mgombea mwenza) na Dk. Shein ili CCM ipate ushindi wa kishindo, ambao haujapata kutokea Tanzania,"alisema.

UKAWA NI PAKA WALIOUNGANA MIKIA

Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Borafya alisema CCM itaibuka na ushindi wa kishindo kwa vile ilianza maandalizi mapema na kusimamisha mgombea anayekubalika.

Amesema CCM itashinda kwa vile ndicho chama pekee cha siasa nchini kinachopigania amani, umoja, utulivu na mshikamano, tofauti na vyama vingine, ambavyo vimekuwa vikihubiri vurugu na uvunjifu wa amani.

Borafya amesema kujitokeza kwa makada wengi wa CCM kuomba kuteuliwa kuwania urais katika uchaguzi huo ni uthibitisho wa wazi wa kukomaa kwa demokrasia ndani ya Chama.

Ameufananisha muungano wa vyama vya kisiasa kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuwa ni sawa na paka wawili walioungana mikia, ambao baada ya kumuona panya, mikia yao hukatika.

"Hakuna ishara yoyote inayoonyesha kwamba mgombea wa UKAWA atashinda. Hawa ni sawa na paka wawili walioungana mikia, ambao wakimuona panya, kila mmoja atamtaka. Lengo la vyama hivi kila kimoja ni kutaka urais. Panya wa UKAWA ni urais,"alisema.

Alisema kukatika kwa vyama hivyo kumeanza kujionyesha baada ya Profesa Lipumba kujiuzulu wadhifa wake wa uenyekiti taifa na kubaki kuwa mwanachama huku Juma Haji Duni akijiondoa CUF na kujiunga na Chadema.

            CUF YA KISULTANI

Akizungumzia uchaguzi mkuu wa rais wa Zanzibar, Borafya alisema CCM kitaibuka na ushindi mkubwa kutokana na Chama cha CUF kupoteza mwelekeo.

Borafya amesema kwa sasa hakuna tena upinzani Zanzibar ndio sababu viongozi wawili wa juu wa CUF, Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba amejiuzulu na Makamu Mwenyekiti wake upande wa Zanzibar, Juma Haji Duni, amejitoa na kujiunga na Chadema.

Amesema CUF si chama cha siasa kwa vile hakikuundwa kutokana na fikra za wanachama wake bali ni kampuni ya mtu binafsi, ambaye ndiye mwenye maamuzi ya mwisho kuhusu kila kitu.

"Fikra za wanachama ndizo zinazoweza kukifanya kishinde uchaguzi na kuongoza nchi. Kikiwa  hakina fikra za wanachama, kinaendeshwa na fikra za mtu mmoja, hicho si chama ni kampuni,"alisema Borafya na kuongeza:

"Ukitaka kufukuzwa CUF, utoe fikra zako. Ukitaka kufukuzwa CUF, gombea nafasi yoyote ya juu ya uongozi."

Borafya alisema kwa sasa wanachama na wafuasi wa CUF wameshaanza kuutambua ukweli huo ikiwa ni pamoja na kukubaliana na sera za CCM ndio sababu hakina uwezo wa kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.

Amesema CUF kinaendeshwa kwa kuiga tabia, maadili na mwenendo wa kifalme, ambapo mfalme hawezi kurithiwa hadi atakapofariki dunia ndio sababu kwa miaka yote tangu kilipoanzishwa na tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, mgombea wake wa urais visiwani Zanzibar ni Maalim Seif Sharrif Hamad pekee.

"Hiyo ndiyo hulka na maadili ya kifalme. Hakuna mwingine anayeweza kugombea urais CUF Zanzibar hadi Maalim Seif atakapokufa.

"Ndio maana nasema sasa wameshaanza kuelewa. Juzi alitoka Profesa Lipumba, baadaye amefuata Duni kaenda Chadema,"alisema.

        SERIKALI YA KITAIFA

Borafya amesema pia kuwa hakuna uwezekano wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo kwa vile serikali hiyo haikuwa ya kudumu bali ilikuwa ya mpito kwa lengo la kuleta amani, umoja na mshikamano.

Alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa ililenga kuwafanya wananchi wa visiwa hivyo wawe wamoja na kuondosha uhasama uliokuwepo baina ya wanachama na wafuasi wa vyama vya CCM na CUF.

"Tulikuwa tumechoshwa na matukio ya vurugu wakati wa uchaguzi na uhasama baina ya wananchi wa Zanzibar ndio sababu tulikubali kuwasikiliza wenzetu duniani, tukaunda serikali ya umoja wa kitaifa, lakini haikuweza kutimiza malengo yaliyokusudiwa,"alisema.

Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Mjini alisema, miezi sita baada ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa visiwani Zanzibar, yalianza kujitokeza matukio mbalimbali yanayoashiria vurugu na uvunjifu wa amani, ikiwemo mashekhe na mapadri kumwagiwa tindikali, makanisa kuchomwa moto kama ilivyokuwa kabla ya kuundwa kwa serikali hiyo.

"Tuliyoyakusudia hayakufanikiwa, yalirejea yaleyale ya Zanzibar ya zamani kupitia Uamsho. Wananchi wamechoshwa na serikali ya aina hiyo kwa sababu malengo yaliyokusudiwa hayakufikiwa,"alisema.           

            HAKUNA KAMA MAGUFULI
Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Mjini, amesema mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, atapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na rekodi, utendaji wake wa kazi na kukubalika na wananchi.

Amesema tofauti kati ya Magufuli na wagombea wengine wa vyama  vya upinzani, akiwemo Lowassa ni sawa na Mlima Kilimanjaro na vichuguu.

"Kitakachomuongoza Magufuli kushinda uchaguzi huo kwa kishindo mbali na kukubalika kwake ni Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Hii ndiyo dira ya Chama kwa wananchi kwa vile inaeleza nini ambacho serikali yao itawafanyia. Vyama vingine havina ilani na wala hawana mkataba na wananchi,"alisema.

Borafya amesema Ilani ni sawa na vitabu vitakatifu vya Zaburi, Taurati, Injili na Kuraani vilivyoshushwa na Mungu kwa mitume wake, kwa ajili ya kuwaelekeza binadamu juu ya maisha yao na nini wanachopaswa kukifanya.

"CCM katika kuthamini hayo yote imetoa ilani yake ili kuwaeleza wanachama na wananchi nini itawafanyia kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Siku zote msisitizo wetu ni amani, utulivu na utawala bora wa kidemokrasia,"alisema kada huyo mkongwe wa CCM.

"Wapinzani siku zote wamekuwa wakihubiri uvunjifu wa amani. Mara waseme nchi haitatawalika, haitakalika, haya yote ni mambo ya ajabu ajabu ambayo watanzania hawako tayari kuyashuhudia,"alisisitiza.

            UTEUZI WA SAMIA
Borafya pia ameipongeza CCM kwa uamuzi wake wa kumteua Samia kuwa mgombea mwenza wa urais, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya nchi kuwepo kwa mgombea mwenza mwanamke.

Amesema uteuzi huo umezidi kudhihirisha kupanuka kwa demokrasia ndani ya CCM na pia kutekelezwa kwa vitendo azma ya serikali ya kuwepo kwa uwiano wa 50 kwa 50 katika uteuzi wa viongozi ndani ya chama na serikali.

Amesema mwamko wa wanawake katika kuwania nafasi za juu za uongozi nao umezidi kuongezeka ndio sababu mwaka huu walijitokeza wanawake watano kuomba kuteuliwa kuwania urais, wakiwemo wawili waliofika hatua ya mwisho ya kupigiwa kura na mkutano mkuu wa CCM.

"Lazima tuutekeleze kwa vitendo mkakati wetu wa 50 kwa 50 kwa vile tumekubaliana iwe hivyo na hili litafanyika kuanzia ngazi za chini za uongozi hadi juu,"alisema.

            WANAOJITOA CCM
Akizungumzia kujitoa kwa baadhi ya wana-CCM na kujiunga na upinzani baada ya majina yao kukatwa wakati wa uteuzi, Borafya amesema huo ni undumilakuwili unaotokana na wanachama hao kuweka mbele zaidi maslahi yao binafsi.

Alisema ndani ya CCM wapo wanachama wa aina tatu, wana-CCM damu, wakereketwa na wanachama maslahi na kila kundi lina udhaifu wake.

Akifafanua, alisema wana-CCM damu ni waasisi wa vyama vya TANU, ASP na CCM, ambao wamekuwa wakikipigania Chama kwa hali na mali, ikiwa ni pamoja na kujitolea maisha yao kuhakikisha kinadumu.

Alisema wakereketwa wa CCM ni wale wasiokuwa na kadi, lakini wanakipenda chama na kukipigania wakati wanachama maslahi ni wale wanaoingia kwenye chama kwa malengo ya kujinufaisha.

"Hawa ni wale ambao ukifika wakati wa nafasi zao kuchukuliwa na wengine au wakishindwa kwenye uchaguzi, wanahamia vyama vingine. Kwa vile wameshaanza kutambulika, Chama kimeshaanza kuwachukulia hatua.

"Slogan yetu ni chama kwanza mtu baadaye. Kama upo kwenye chama kwa maslahi yako, lazima ushughulikiwe kwa sababu wanachama wa namna hii wanazifahamu vyema taratibu za chama, lakini wanafanya makusudi kuzipuuza,"alisema.

            VYUO VYA SIASA

Ili CCM iweze kuendelea kuwepo madarakani kwa muda mrefu, Borafya ameshauri utaratibu wa kuwaandaa viongozi mapema urejeshwe, ikiwa ni pamoja na kufufuliwa kwa vyuo vya siasa.

Alisema viongozi wengi wa CCM na serikali waliopo madarakani hivi sasa waliandaliwa mapema kupitia Jumuia ya Umoja wa Vijana na vyuo vya siasa, lakini utaratibu huo kwa sasa umekufa.

"Vijana wa zamani wa chama walikuwa wakipelekwa vyuo vya siasa, walipewa itikadi na kuelekezwa mapema dhamana ya uongozi na hatimaye kupandishwa taratibu. Hilo sasa halipo. Kila mtu anataka uongozi, hajulikani ametoka wapi, hajui historia ya chama wala siasa, lakini anataka kuwa kiongozi.

"Ameambiwa tu ukitaka kugombea uongozi CCM vaa shati la kijani, lakini hakielewi Chama. hatuwezi kuendelea kuwa na viongozi wa aina hii, tutakiua chama chetu. Lazima utaratibu wa zamani wa kuwaandaa viongozi urejeshwe,"alisema.

Borafya amewataka watanzania waendelee kudumisha amani na mshikamano na kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao na kuendelea kuichagua CCM ili iweze kuwaletea maendeleo.

Amewataka wanachama kujiepusha na vitendo vya vurugu na uvunjifu amani ili uchaguzi huo uwe huru na wa haki na wapatikane viongozi bora watakaoieletea nchi mafanikio.

                WASIFU
Borafya alizaliwa miaka zaidi ya 65 iliyopita. Alianza uongozi tangu enzi za ASP. Alikuwa mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Mjini kwa miaka 15 kabla ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa mkoa wa Mjini mwaka juzi.

Alikuwa mwajiriwa wa Shirika la ZSTC kuanzia mwaka 1968, akiwa katibu wa ASP hadi mwaka 1992 alipostaafu na kuchaguliwa kuwa katibu mwenezi wa CCM wa jimbo la Rahaleo, wakati huo mbunge wake akiwa marehemu Hassan Diria na mwakilishi akiwa rais mstaafu Amani Abedi Karume.

No comments:

Post a Comment