Friday, 28 August 2015

NEC YAFAFANUA UKAWA KUKATALIWA KUTUMIA VIWANJA VYA JANGWANI



NA RACHEL KYALA
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema ni sahihi kwa CHADEMA kukataliwa kufanya uzinduzi wa kampeni katika Uwanja wa Jangwani kwa kuwa hawakutimiza matakwa ya kisheria.
Aidha, NEC imekabidhi majina 52,780 ya watu waliojiandikisha zaidi ya mara moja kwa Jeshi la Polisi ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Miongoni mwa watu hao, wapo madiwani wawili wa CHADEMA ambapo diwani wa Kimara amejiandikisha mara tano na diwani wa Msongola alijiandikisha mara saba, katika vituo tofauti.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Silima Abdallah, alisema CHADEMA, imekiuka kanuni ya 40 ya uchaguzi wa rais na wabunge ambayo inakitaka chama chochote cha siasa kuwasilisha NEC ratiba ya kampeni, mkoa, muda na mahali watakapofanyia mkutano.
“Wenzao CCM katika ratiba yao walionyesha kuwa watazindua kampeni Agosti 23, Dar es Salaa, Wilaya ya Ilala katika Uwanja wa Jangwani, saa 2 asubuhi hadi 12 jioni. Vile vile, itafunga kampeni zake Oktoba 24, mwaka huu viwanja vya Tanganyika Packers, Kinondoni, Dar es Salaam, saa 5 hadi 12 jioni,” alisema.
Alisema CHADEMA, walionyesha tu kuwa ni Dar es Salaam katika wilaya zote tatu saa 7 hadi 12 jioni, lakini hawakuonyesha viwanja halisi watakavyofanyia kampeni hizo jambo ambalo ni kinyume cha kanuni.
Alifafanua kuwa chama hicho kinatakiwa kuwasilisha marekebisho ya ratiba hiyo kwa NEC kwa kuonyesha ni kiwanja gani itafanyia uzinduzi wa kampeni zake.
“NEC ingeweza kikitetea chama hicho kama kinavyodai kunyimwa Uwanja wa Jangwani, iwapo tu kingekuwa kimeonyesha kwenye ratiba ya kampeni zake iliyopitishwa na tume,” alisema.
Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa sheria, Tume itakachohakikisha ni kwamba Agosti 29, hakuna chama kingine kinachofanya kampeni kwa kuwa tarehe hiyo imeshatajwa na CHADEMA,” alisema.
Mtaalamu wa Idara ya TEHAMA wa NEC, Sist Kariah, alisema kujiandikisha zaidi ya mara moja, kisheria ni kosa la jinai ndio maana limekabidhiwa jeshi la polisi ili kuwachukulia watu hao hatua za kisheria.
“Tayari kuna kesi 12 nchini zilizotolewa hukumu ambapo miongoni mwao wapo waliohukumiwa mwaka mmoja na nusu hadi miwili ikiwemo kutozwa faini kutokana na kujiandikisha zaidi ya mara moja,” alisema.
Alisema mfumo mpya wa uandikishaji kupitia mashine za kielektroniki (BVR), ni wa kisasa ambapo ni rahisi kubaini udanganyifu na iwapo mtu aliandikishwa zaidi ya mara moja kimakosa, mfumo huo unabainisha.
“Tume inaandaa utaratibu ili kupeleka Idara ya Uhamiaji majina ya watu waliojiandikisha kupiga kura ambao si raia wa Tanzania, ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao,” alisema.
Alisisitiza kuwa watu wanaodhani wakijiandikisha mara nyingi wanaweza kupiga kura zaidi ya mara moja wanajidanganya kwani upigaji kura si wa kielekroniki.
Alisema kazi ya uhakiki na utayarishaji wa Daftari la Wapigakura bado inaendelea, hivyo watu zaidi watakaobainika kufanya udanganyifu hawataepuka mkono wa sheria.
Aliwataka watu waliojiandikisha zaidi ya mara moja na wale ambao si raia wajisalimishe wenyewe NEC na kukiri makosa hayo ambapo walioandikishwa zaidi ya mara moja kimakosa, hawatashitakiwa.
Alionya kuwa watu watakaohukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi sita, ni kosa kisheria kupiga kura hata katika uchaguzi mwingine.
Alisema watu ambao hawataona majina yao kwenye daftari la wapigakura watambue kuwa wamefutwa kutokana na dosari ikiwemo kujiandikisha chini ya umri wa miaka 18.
Akipokea majina hayo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Benedict Wakulyamba, alisema uchunguzi dhidi ya watu hao utafanyika haraka ili kuwashitaki mahakamani kabla ya uchaguzi, Oktoba 25.
“Ili kuharakisha kazi hii, tutafanya mawasiliano haraka na mikoa walipo watuhumiwa ili hatua dhidi yao zichukuliwe haraka,” alisema Wakulyamba.

No comments:

Post a Comment