Dk. Magufuli, picha ya chini na juu akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye stendi ya Mbalizi |
WANANCHI waliofurika kwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli |
MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli akihutubia mkutano wa kampeni jana |
Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akiwatambuisha kwa wananchi Mhe. Wiliam Lukuvi pamoja na Dk. Mary Mwanjelwa,kulia ni Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Abbas Kandoro |
NA SELINA WILSON, MBALIZI
KAMPENI za uchaguzi mkuu zimezidi kupamba moto katika mikoa ya Mbeya na Songwe, ambapo Mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli, amesema hadharani kwamba hana deni la kumlipa mtu kwa kuwa alipita kwenye mchujo bila kutoa fedha.
Amesema baadhi ya wagombea walitumia mamilioni ya shilingi kuhonga ili wachaguliwe kuwania urais kwa tiketi ya CCM, lakini hawakufanikiwa kwa kuwa vitendo vya rushwa haviruhusiwi ndani ya Chama.
“Sikuhonga hela kwa sababu hata kwenye maandiko matakatifu rushwa imekatazwa na ndio maana nilimkabidhi Mungu mchakato huu na alinisadia nikateuliwa na kushinda uchaguzi.
“Waliohonga mnawafahamu na tayari wengine wametoka ndani ya CCM baada ya kukatwa,” alisema.
Aliyasema hayo jana katika mikutano ya kampeni, ukiwemo mkubwa uliofanyika katika viwanja wa Stendi ya Mbalizi mkoani Mbeya, ambao ulifurika umati wa wananchi kiasi cha watu kukanyagana.
Alisema hana wa kumlipa na hakuna atakayemdai fedha, lakini anajua deni lake kubwa ni kuwatumikia Watanzania kwa kufanya kazi kwa bidii na kuleta maendeleo bora.
Dk. Magufuli alisema aliingia kwenye mchakato wa ndani ya chama wa kumpata mgombea urais sijatoa fedha na kwamba, Mungu ndiye aliyemfikisha hapo hivyo aliwaomba wana Mbalizi wampe kura bila kujali itikadi.
“Nilitoka nyumbani kwangu nikaenda kuchukua fomu kimya kimya, Nikatafuta wadhamini kimya kimya na nikarudisha fomu kimyakimya,” alisema.
Alisema wapo baadhi waliotumia mamilioni ili kupata nafasi hiyo, lakini Mungu aliamua yeye ndiye awe mgombea wa CCM kwa nafasi ya rais hivyo, aliwaomba wananchi wamuombee awe Rais awatumikie.
Dk. Magufuli alisema watu walihonga , waliwanunua watu na kwamba watu hao wakiingia kwenye madaraka watawauza mpaka watu na ndiyo maana mimi nimeamua kuwania urais ili nibadilishe mambo.
“Kama kuna mtu ana ushahidi kwamba nilitoa rushwa, au niliwanunua watu ili wanichague autoe,” alisema
Alisema akichaguliwa ataanzisha mahakama ya mafisadi ili kuhakikisha mtu akiiba fedha za serikali anafikishwa mahakamani bila kuchelewa
Alisema anatambua matatizo ya Mbalizi, ikiwemo ya barabara na maji ambapo, kina mama wanahangaika kutafuta maji umbali mrefu, hivyo aliwaomba wamchague mgombea ubunge wa CCM apate mtu wa kufanya nae kazi.
Dk. Magufuli alimpa nafasi mgombea ubunge wa Mbeya Vijijini, Olan Njeza, ambaye alisema wana tatizo kubwa la barabara ya lami ya Mbalizi Mjini ya kilomita moja ambayo ni kero na aliomba ikamilishwe kwa kiwango cha lami kwa kuwa ni ahadi ya ilani.
Baada ya ombi hilo, Dk. Magufuli alimuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya, aliyemtaja kwa jina moja la Lyakurwa ndani ya wiki moja aanze kutengeneza barabara hiyo.
“Mimi bado ni Waziri wa Ujenzi na kwamba huyo Njeza ameanza kunipa kazi na mimi nitaifanya na nitazungumza na mtendaji mkuu wa TANROADS ili kazi hiyo ifanyike na kuondoa kero kwa wananchi,” alisema.
UFISADI NA UTAJIRI WA HARAKA
“Nachukia ufisadi, nachukia wizi, nachukia mambo ya uzembe katika utendaji. Nina uhakika wengine nikiwateua wataniambia mzee hapana kwa kuwa wananifahamu,” alisema akiongelea vita vya ufisadi.
Dk. Magufuli akiwa katika Kijiji cha Mbala akielekea Mkwajuni katika Jimbo la Chunya, alisema wapo baadhi ya watu wanaotaka utajiri wa haraka haraka wamekuwa kikwazo kwa maendeleo ya Watanzania.
Alisema watu hao wanatamani Tanzania iingie kwenye vurugu na machafuko kwa sababu wao wanataka kutajirika na rasilimali za nchi, hivyo akiwa rais atahakikisha anawashughulikia.
“Watu hao walivyoona nimechaguliwa bila kutoa fedha, wameanza kuwa na hofu na wengine wakaamua kukimbia. Nataka niwaambie nahitaji niwe Rais ili kuhakikisha nadhibiti mianya yote ya mapato ya serikali ili yanawanufaishe wananchi wa chini,”alisema.
Alisema Tanzania ina rasimali nyingi, lakini baadhi ya wakubwa wamekuwa wakizitumia kinyume na matakwa ya wananchi ambapo alisisitiza kwamba wakati mwingine inakutwa meno ya tembo yamekamatwa nje ya nchi.
Dk. Magufuli alisema anachukia ufisadi, anachukia rushwa kwa kuwa hayo ndio yamesababisha asilimia 28.2 kuendelea kuwa masikini, lakini kwa sasa ataibadilisha Tanzania.
“Kuna watu wanasema Dk. Magufuli ni mzuri lakini kwa sababu yuko CCM…. msipate shida wanaohitaji mabadiliko mtayapata ndani ya CCM. Mfano halisi ni China ambayo imepiga hatua kubwa na chama cha kikomunisti bado kipo madarakani,” alisema.
Alisema wachina walifanya mabadiliko makubwa na sasa ni nchi ya kwanza kwa uchumi na mataifa makubwa yamebaki yanashangaa.
Alitoa mfano wa Libya ambapo Rais Muammar Gaddafi, aliongoza nchi kwa mafanikio makubwa, watu waliishi kwa raha, vijana wakioa wanapatiwa fedha na nyumba za kuishi, lakini walichoka na raha wakataka mabadiliko hadi wakamuua Gadafi na sasa wanajuta kwa kuwa hali ni ngumu.
WAZEE KUPATIWA PENSHENI
Alisema akichaguliwa kuwa Rais atahakikisha wazee wanapatiwa pensheni ili waweze kupata fedha kidogo za kujikimu.
Dk. Magufuli alisema serikali inatambua umuhimu wa wazee, hivyo itaendelea kuwatunza na kuwasimamia ili wapate pensheni.
Akiwa Makongolosi, aliwaahidi wananchi kwamba atajenga kilomita nne za barabara ya lami ili kuhakikisha mji huo unafunguka kimaendeleo wananchi wapate kusafirisha mazao.
Pia, alisema serikali yake ya awamu ya tano itatoa mikopo kwa wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli kwa ufanisi na wanufaike na uchumbaji madini na kukuza uchumi wa eneo hilo.
KUTIKISA MBEYA MJINI LEO
Leo Dk. Magufuli anatarajiwa kutikisa Jiji la Mbeya na viunga vyake katika mkutano mkubwa wa kampeni.
Mkutano huo ambao utakuwa wa aina yake utakaopambwa na burudani mbalimbali, utafanyika katika viwanja vya Ruanda Nzovwe na unatarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi wakiwemo wana CCM na wasio wana CCM.
Dk. Magufuli ataingia Mbeya Mjini, baada ya kufanya mikutano mikubwa ya hadhara katika viwanja vya Mwakangale Wilaya ya Kyela, ambapo pamoja na mambo mengine atamnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo, Dk. Harrison Mwakyembe.
Kwa mujimu wa ratiba ya mikutano ya kampeni za CCM katika Mkoa wa Mbeya, Dk. Magufuli ambaye amekuwa kivutio kwa wananchi bila kujali itikadi, amefanya mikutano mikubwa ambayo imekuwa ikifurika umati wa watu.
Kabla ya kuhutubia mkutano wa Mbeya Mjini, Dk. Magufuli atafanya mkutano mwingine mkubwa wa hadhara katika Uwanja wa Tandale wilayani Rungwe ambapo atazungumza na wananchi na kuomba ridhaa yao ili awe Rais wa awamu ya tano.
No comments:
Post a Comment