Friday, 28 August 2015

LAIZER AMSHUKIA LOWASSA, ADAI NI MNYANYASAJI NA MBINAFSI




NA EPSON LUHWAGO, NAMANGA
MBUNGE wa Longido anayemaliza muda wake, Lekule Laizer, amesema Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ni mbinafsi na mnyanyasaji, hivyo hafai kuwa Rais wa Tanzania.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye mji mdogo wa Namanga, mpakani mwa Kenya na Tanzania, Laizer alisema Lowassa alichangia kwa kiasi kikubwa kwa Wilaya ya Longido kuwa nyuma kimaendeleo.
Kwa mujibu wa Laizer, kiongozi huyo alikuwa mstari wa mbele kuikandamiza Longido kwa kuwa hata wakati wa kuunda uongozi wa halmashauri ya wilaya, alikuwa anahakikisha mwenyekiti anatoka Monduli na si Longido.
“Tulipokuwa katika Wilaya ya Monduli na yeye akiwa Waziri, miradi mingi alikuwa anaipeleka Monduli. Hata nilipokuwa naomba Longido iwe wilaya alikuwa anapinga na hata kusema ni ndoto kwa Longido kuwa wilaya.”
Hata tulipofanikiwa kupata, alitufanyia ubaya kwenye mgawanyo wa mali. Magari yote tuliyopata yalikuwa mabovu tupu. Nilikwenda TAMISEMI kwa (Mizengo) Pinda wakati huo akiwa waziri kumweleza, lakini kwa kuwa Lowassa alikuwa ndiye Waziri Mkuu, hakuna tulichopata,” alisema.
Alitoa mfano wa miradi ya maji ambapo wakati huo ikiwa wilaya moja, walipata miradi 20,  lakini cha ajabu Longido haikupata na Monduli ilipata 20 na katika uchimbaji mabwawa, Monduli ilipata 14 kati ya 18 huku Longido ikiambulia minne tu.
“Haya ni mambo machache nimeamua niseme namna Lowassa alivyotutesa watu wa Longido. Mwenyewe alininyanyasa sana, lakini kuna siku nilimwambia kuwa hatakuwa Waziri Mkuu wa milele labda wa Monduli,” alisema Laizer.
Katika kuthibitisha kuwa ni mbinafsi, aliwapasha wana Longido juu ya kuamua kumteua aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo ole Nangole, kuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo wakati hakushiriki hata kura za maoni ndani ya CHADEMA.
Kutokana na sifa hizo, Laizer alisema Lowassa hafai kuwa kiongozi wa nchi na Watanzania wanapaswa kujifunza ili kupata undani juu yake badala ya kumshabikia na kumwona ni mtu mzuri.
Kuhusu hali ya kisiasa katika jimbo hilo, alisema bado ni nzuri licha ya kwamba kuna kikundi cha watu kilichoondoka baada ya Lowassa kujiengua CCM.
Alizungumza katika mkutano huo, Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, alisema Laizer ameweka mambo hadharani, hivyo wana Longido wasifanye makosa kuchagua upinzani.
Samia alisema kero zinazoukabili mji mdogo wa Namanga, zikiwemo maji na ajira kwa vijana, vitapatiwa ufumbuzi katika serikali ya awamu ya tano chini ya CCM.
Alisema tatizo la maji limeshaanza kushughulikiwa ambapo serikali imetenga sh. bilioni 13 kwa ajili ya kutoa maji Mto Simba wilayani Siha, Kilimanjaro na kupeleka kwenye miji ya Longido na Namanga.
Kuhusu ajira kwa vijana, alisema serikali inatarajia kuanzisha mpango maalumu wa ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati ambavyo vitasaidia kupunguza tatizo hilo.
Pia, alisema sh. milioni 50 zitakazotolewa kwa kila kijiji, zitawezesha kina mama na vijana kupata mikopo ambayo itawasaidia kupunguza ajira miongoni mwao.
Kuhusu afya, alisema serikali inatarajia kujenga hospitali kubwa na ya kisasa katika mji wa Longido na kuboresha vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali ili kuwaondolea wananchi adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hizo.
“Kwa hiyo ndugu zangu serikali ijayo ya CCM imepania kwa nguvu zote kuhakikisha tatizo la ajira linapunguzwa kwa kiasi kikubwa. Ichagueni CCM ili tuweze kutekeleza ahadi hizi.
“Baadhi ya vyombo vya habari vimeandika leo (jana) kuwa ahadi za Samia zitekelezwe. Napenda kuwaambia kwamba ahadi hizo zitatekelezwa kwani maana ya Samia ni mtu anayesikia na ni mtu aliyechaguliwa na hatasema uongo,” alisema.
Sambamba na hiyo, alisema serikali itashughulikia tatizo la upatikanaji wa vibali kwa wafanyabiashara katika mji mdogo wa Namanga.

No comments:

Post a Comment