Friday, 28 August 2015

KIMELIPUKA CUF, HATMA YA MAALIM SEIF SASA SHAKANI, DK SLAA HAKIJAELEWEKA

MAALIM Seif Sharifu Hamad
Dk. Willbrod Slaa

NA MWANDISHI WETU
TANGU kuachia ngazi kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, mambo bado si shwari ndani ya chama hicho ambapo bomu zito linatarajiwa kulipuka wakati wowote.
Profesa Lipumba aliachia wadhifa huo kutokana na mmoja wa washirika wa vyama vinavyounda UKAWA, CHADEMA kumpokea Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa.
Lowassa alijiunga na CHADEMA baada ya kukatwa kwenye mchakato wa kuwania urais ndani ya CCM kutokana na kutokuwa na sifa huku akituhumiwa kuwa na makandokando, hivyo isingekuwa rahisi kupewa nafasi kubwa ya kuongoza nchi.
Mbali na Profesa Lipumba, pia Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa, naye aliachia wadhifa huo kutokana na kuchukizwa na hatua ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kubariki Lowassa kujiunga na CHADEMA.
Kwa miaka mingi na kwa nyakati tofauti, Mbowe na Dk. Slaa wamekuwa wakimtuhumu Lowassa si msafi huku wakimtaja kwenye orodha za watu waliodai kuwa ni mafisadi nchini.
Hata hivyo, bundi hilo la migogoro bado linatikisa ndani ya CUF, baada ya wajumbe wa Kamati Kuu na Mkutano Mkuu wa chama hicho kujipanga kumbana Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Shariff Hamad.
Habari za kuaminika zinasema kuwa baadhi ya wajumbe hao wamemtaka Maalim Seif kuweka hadharani maslahi ambayo CUF itayapata kwa kujiunga na kundi la UKAWA.
Aidha, wanajipanga kumpinga na kutompigia debe Lowassa, ambaye amekuwa akisaka nafasi ya kutimiza ndoto za kuwa rais wa Tanzania.
Kwa nyakati tofauti, wasomi, wanasiasa na makundi mbalimbali yameweka bayana kuwa Lowassa hana sifa za kuwa rais na kuwaasa Watanzania kutompigia kura.
Habari kutoka kwa baadhi ya wajumbe ambao hawakupenda kutajwa majina gazetini, wamemshutumu Maalim Seif kwa kukiongoza chama hicho kibabe na kwa upendeleo.
Wamedai kuwa kumekuwepo na upendeleo wa wazi miongoni wajumbe ambapo kuna wanaosikilizwa na wengine wamekuwa wakipuuzwa hata kama wana mawazo yenye kujenga.
Wamedai CUF kimeingizwa ndani ya UKAWA bila baraka za wanachama na kwamba hata mambo yanayoamliwa kwa sasa ni uamuzi wa kikundi cha watu wachache, jambo ambalo halina afya kwa chama.
"CUF kimeingizwa UKAWA 'kichwa kichwa' na sasa hivi mambo ni magumu zaidi na hatujui hatima yake…makubaliano na ahadi tamu ambazo zilitolewa awali kwa sasa zimeyeyuka.
"Makubaliano ya kuachiana majimbo kwa sasa yamekuwa shubiri, hakuna kinachoeleweka na wagombea wetu wamepoteza mwelekeo na viongozi wamekaa kimya.
“CUF kwa upande wa Bara ni kama kimekufa kinasubiri kufukiwa shimoni kwa sababu ya uamuzi wa wachache na ulioghubikwa na usiri mkubwa,” alisema mmoja wa wajumbe hao.
Vyanzo hivyo vimeongeza kuwa kabla ya kujiunga na UKAWA, CUF ilikuwa ikisimamisha wagombea wake kwenye nafasi zote za ubunge na udiwani katika majimbo yote.
Hata hivyo, wamedai bado wako njia panda na wanaamini hata Maalim Seif mwenyewe atakuwa anajutia uamuzi wa kuiingiza CUF ndani ya UKAWA bila kutafakari kwa kina.
Mjumbe mwingine alidai kutofuatwa kwa makubaliano katika mgawanyo wa majimbo na hata nafasi ya mgombea urais, kumevuruga mambo zaidi na kuipoteza mwelekeo CUF.
Aliongeza kuwa makubaliano ya awali ni kila chama kuteua mgombea urais wake, ambapo baadaye wangeshindanishwa na kuchaguliwa kwa kura na wanachama wanaounda UKAWA.
Ndani ya CUF mchakato huo ulifanyika, ambapo Profesa Lipumba aliteuliwa huku Dk. Slaa akitajwa kuwa mgombea kwa upande wa CHADEMA na Dk. George Kahangwa akiteuliwa kupitia NCCR-MAGEUZI.
Hata hivyo, makubaliano hayo hayakuheshimiwa na badala yake CHADEMA kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi walilazimisha nafasi hiyo kupewa Lowassa.
Uamuzi huo ndio uliomng’oa Dk. Slaa ndani ya CHADEMA na Profesa Lipumba ndani ya CUF na kuwaacha Mbowe na James Mbatia (Mwenyekiti wa NCCR-MAGEUZI), wakipambana kumsafisha Lowassa.
Pia, mjumbe huyo alidai kuwa wakati Lowassa akipokewa ndani ya UKAWA kulikuwa na ahadi ya kujiunga na zaidi ya wabunge 80 kutoka CCM huku CUF ikiahidiwa kupata 40.
"Hakuna utekelezaji wa ahadi hiyi, wabunge wachache waliotoka CCM wote wamejiunga CHADEMA na kupewa majimbo…Tumehoji hili mara kadhaa, lakini hakuna majibu," alidai.
Lingine ambalo wajumbe hao wameeleza kukerwa nalo ni hatua ya kumruhusu Makamu Mwenyekiti wa CUF Taifa, Juma Duni Haji, kujivua uanachama na kujiunga na CHADEMA.
Duni alijivua uanachama na wadhifa wake huo ili aweze kupata uhalali wa kuwa mgombea mwenza wa Lowassa, jambo ambalo limechukuliwa kuwa ni dharau kubwa na hatima yake baada ya uchaguzi iko gizani iwapo atarudi ama la.
"Kulikuwa na kelele nyingi kuwa CUF inaingizwa shimoni, lakini watu waliziba masikio…wenzetu CHADEMA wamecheza na akili zetu na kutuzidi. Ni aibu kwa kiongozi wa ngazi za juu kurubuniwa kwa ahadi ya uongozi na kukihama chama kirahisi kabisa," alihoji mjumbe huyo.
Kutokana na hilo, baadhi ya wanachama wa CUF kwa sasa wamegawanyika na majina kama Boko Haram au CUF Profesa yakiibuka.
“Kwa sasa tunaopinga CUF kuingia kichwa kichwa ndani ya UKAWA tumepewa majina kama 'Boko Haram au CUF Profesa,” aliongeza.
Dk. Slaa kulamba matapishi yake?
Katika hatua nyingine, habari zilisema kuna  mikakati ya kumshawishi Dk. Slaa ili aibukie kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho uliopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam kesho.
Ingawa hakuna taarifa rasmi kutoka Chadema inayoeleza kuwa Dk. Slaa atahudhuria mkutano huo, baadhi ya viongozi wameeleza kuhusu uwezekano wa jambo hilo kutokea.
Gazeti hili lina taarifa kutoka mmoja wa wanachama wa CHADEMA aliyeshiriki katika vikao vya kuandaa Ilani ya Uchaguzi inayojumuisha vyama vyote vilivyo kwenye UKAWA kuwa wajumbe walielezwa Dk. Slaa atahudhuria uzinduzi wa kampeni.
“Tumeambiwa kuwa Dk. Slaa atahudhuria uzinduzi wa kampeni…haifahamiki kama ndiyo anarejea moja kwa moja ama ni mgeni tu. Kama atakubali itakuwa njema ila akiendelea na msimamo wake bado doa halitafutika na itatuathiri sana,” alisema.
Habari za kuaminika zinasema baada ya kumaliza mapumziko yake, Dk. Slaa akiwa nyumbani kwake Karatu, ndugu, jamaa na marafiki walijaribu kumshawishi ili arejee CHADEMA.
Tayari, Mbowe alitangaza kuwa UKAWA imemweka Dk. Slaa pembeni ili harakati za kusaka Ikulu ziendelee kwani, hawajui msimamo wake hivyo hawawezi kumbembeleza.
Naye Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, atautumia mkutano huo kutangaza rasmi kujiunga na NCCR-MAGEUZI, ambacho amekuwa akihusishwa nacho.

No comments:

Post a Comment