Friday, 28 August 2015

BODABODA WAIKANA UKAWA




JESCAR KILEO NA CHRISTOPHER LISSA
VIONGOZI wa Vyama vya Madereva wa Pikipiki (Bodaboda), jijini Dar es Salaam, wamewaonya baadhi ya madereva wenzao  ambao ni wafuasi wa UKAWA kuacha  mara moja hila za kuwagawa wanachama kutokana na maslahi binafasi wanayopata kutoka umoja huo usio rasmi.
Aidha walisema wataendelea kuwa watiifu kwa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho Ilani yake ndiyo ilirasmisha ajira na bishara ya bodaboda hapa nchini ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete.
Walisema wanaheshimu msimamo wao huo na kwamba wako tayari kumpigania, mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli na mgombea mwenza Samia Suluhu Hassan ili waweze kushinda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba,  mwaka huu.
Hata hivyo, walisema ni ruksa kwa wanachama wa bodaboda ambao ni UKAWA kuendelea kushiriki harakati za vyama yao.
Walisema msimamo wa vyama vya bodaboda ni kuunga mkono CCM, ambayo ilani yake ndiyo iliyoanzisha sekta hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Bodaboda Taifa, Mapinduzi Mapande, Katibu wa kamati hiyo, Rashid Salu, Mwenyekiti wa Umoja wa Wapanda Pikipiki Temeke (UWAPITE), Msham Nassoro na  Katibu Mkuu wa Umoja wa Bodaboda Wilaya ya Ilala (UMABWILA), Hamza Saidi, walisema hayo jana katika mkutano wao na waandishi wa habari uliofanyika jana, Ilala, Dar es Salaam.
“Kama viongozi wa vyama vya Bodaboda, hatuwezi kuyumbishwa na wafuasi wachache wa UKAWA ambao tunaamini kuwa wengi si wanachama wetu.
“Hatukatai kwamba bodaboda wanakabiliwa na changamoto, lakini ni kiongozi gani wa UKAWA, ambaye aliwahi kujitokeza kututetea. Viongozi ambao tulikuwa tunahangaika nao kuyatafutia ufumbuzi matatizo yetu ni kutoka CCM tu,” alisema.
Alisisitiza kuwa: “UKAWA wamesubiri tumeteseka hadi kampeni zinaanza ndiyo wanaanza kujifanya wanatujali, walikuwa wapi siku zote.”
Mpema, alisema baadhi ya bodaboda wa UKAWA wanaridhika na vijisenti wanavyohongwa ili kukaa mbele ya misafara ya wagombea,  lakini hawafikirii kipindi ambacho wameteseka na changamoto.
“Kwanza bodaboda wangeishurukuru CCM kwa kurasimisha usafiri huo na kutambulika kuwa ajira rasmi. Wanataka serikali ya CCM iwafanyie nini. Haya mambo yalijadiliwa bungeni na wabunge wengi wa UKAWA walikuwa wakipinga kurasimishwa kwa biashara ya bodaboda,” alisema.
Alisema hawako tayari kuyumbishwa na kwamba, wanasimama kidete kuhakikisha bodaboda wote nchini wanaunga mkono CCM.
Kwa upande wake, Salu aliwataka wanachama wa bodaboda wasikubali kuyumbishwa katika kampeni za uchaguzi bali wawasilikilize viongozi wao ingawa ni ruksa kwa kila mwanachama kufuata itikiadi yake ya kisiasa.
Mwenyekiti wa UWAPITE, Nasoro alisema hawako tayari kuona baadhi ya watu wanaojifanya bodaboda wanawapotosha wenzao  kuunga mkono UKAWA huku wao wakiendelea kujineemesha.
“Mbunge wa Ilala, Mussa Zunguna, Temeke, Abaas Mtemvu ndiyo tuliokuwa tushirikiana nao kudai haki za bodaboda Dar es Salaam,  lakini hatukuwahi kuwaona kina John Mnyika au Halima Mdee,” alisema.

No comments:

Post a Comment