Friday, 28 August 2015

DK. SHEIN ASISITIZA UCHAGUZI KUWA HURU NA WA AMANI

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein akiwa katika viwanja vya CCM Tawi la Kangagani Pemba,

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesisitiza tena kuwa dhamira ya kweli ya serikali ya kufanya uchaguzi huru na wa haki na kuwahakikishia wananchi wenye haki ya kupiga kura, watafanya hivyo kwa uhuru na amani.
“Kila mwananchi mwenye haki ya kupiga kura haki yake italindwa. Tutafanya uchaguzi huru na wa haki wala wananchi wasitiane hofu,” alisema Dk. Shein jana wakati akizungumza na wana CCM na wananchi wa Kijiji cha Kangagani, Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Dk. Shein, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, alisimama katika Tawi la CCM la Kangagani wakati akitokea Wete ambako asubuhi alizindua Mradi wa Hifadhi ya Misitu Asili (HIMA) katika Kijiji cha Makangale.   
Aliwaeleza wananchi hao kuwa wakati wote wa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake amekuwa akihimiza upendo na mshikamano miongoni mwa wana CCM na wanachama na wapenzi wa vyama vingine kwa kuamini kuwa wananchi wa Zanzibar ni watu wamoja, hivyo hawana haja ya kuhitilifiana kwa sababu za kisiasa.
“Nitashangaa nitakapowaona wananchi wa Pemba wanashikana mashati kutokana na tofauti zao za kisiasa wakati wa uchaguzi,” Dk. Shein alieleza.
Kwa hiyo alitoa wito kwa wananchi wote kuwa watulivu na kuishi kwa upendo miongoni mwao na kuwasihi kuacha kuchukiana, kufarakana wala kujenga chuki miongoni mwao kwa sababu za itikadi za vyama na kusisitiza kuwa uchaguzi utakapofika washindane kwa sera na si kwa matusi wala kukashifiana.
Dk. Shein ambaye anagombea tena nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia CCM, aliwahakikishia wananchi hao kuwa vyombo vya dola vipo kwa ajili ya kuwatumikia kwa kuwapatia ulinzi na usalama wao na mali zao na kamwe havina ugomvi nao.
Hata hivyo, alionya kuwa si vyema wananchi kupimana misuli na vyombo hivyo hasa vijana hivyo akawatahadharisha dhidi ya kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
“Wazee na kina mama mara nyingi wamekuwa watulivu, lakini wako baadhi ya vijana wanafanya vitendo vya uvunjifu wa amani kwa makusudi na kuvilazimisha vyombo vya dola kutumia nguvu. Nawatahadharisha hivyo sivyo,” Dk. Shein alionya.
Akizungumzia kwa ujumla uongozi wake wa serikali ulio katika mfumo wa umoja wa kitaifa, Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa ilikuwa changamoto kubwa kwake, lakini ameweza kuanzisha na kuiongoza kwa mafanikio makubwa.
“Nakumbuka wakati nilipofika hapa kuomba kura mwaka 2010 niliwaeleza kuwa mkinichagua changamoto ya kwanza ni kuunda serikali yenye mfumo wa umoja wa kitaifa, lakini niliwaahidi kuwa nitalifanya hilo kwa mafanikio makubwa na kwa hakika nimeweza kwani sasa tumekaribia mwisho wa safari yenyewe kwa awamu hii ya miaka mitano,” Dk. Shein alieleza.
Katika kipindi cha uongozi kinachomalizika, Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa serikali imeweza kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa zaidi ya asilimia 90 na kuwataka wana CCM wasiwe wanyonge kwani, Ilani yao ndio iliyoendesha serikali na mipango mengine ya maendeleo ikiwemo MKUZA II na Dira ya Maendeleo 2020.
Aliwafafanulia wananchi hao kuwa ilani ilitoa maelekezo kwa kila sekta ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii hivyo wanapaswa kujivunia utekelezaji wa Ilani yao kwa kiwango hicho kikubwa.

No comments:

Post a Comment