WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amevunja uongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Songea (SONAMCO) huku akiagiza kukamatwa na kufunguliwa mashitaka kwa ofisa shughuli wa chama hicho, Paul Gwerema kwa tuhuma za ubadhirifu.
Uamuzi huo umechukuliwa baada ya ushirika huo kujiendesha bila kufuata utaratibu na kusababisha kuwepo kwa ubadhirifu huku wakulima wakishindwa kulipwa madeni yao, kiwanda kusimamisha uzalishaji wa tumbaku na kusababisha wakulima kukata tamaa ya kuendelea kulima zao hilo.
Aidha, Mrajisi wa Ushirika aliagizwa kufuatilia kwenye Bodi ya Usajili wa Kampuni (BRELA), taratibu zilizotumika kuanzishwa kwa kampuni ya FDTU, iliyoundwa na baadhi ya vyama vikuu vya ushirika baada ya kubainika kutokuwepo kwenye orodha ya mrajisi.
Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo kwenye kikao kilichokuwa kikijadili hatma ya zao hilo na ushirika wa SONAMCO, kutokana na kuporomoka kwa kilimo cha tumbaku, ambacho kilikuwa kikichangia mapato ya mkoa huo.
Alisema baadhi ya viongozi wa chama hicho waliopo mahakamani, serikali inasubiri maamuzi yatakayotolewa na chombo hicho ili kufahamu namna fedha zilizoibwa zitakavyorudishwa, lakini alihitaji kufanyika kwa mkutano wa vyama vya msingi vya ushirika kuchagua viongozi wengine wa SONAMCO.
Alisema viongozi wa SONAMCO hawapaswi kuendelea kubaki madarakani kwa sababu wameshindwa kupanga mikakati ya kufufua zao hilo na kutatua migogoro ya wakulima.
Aliongeza kuwa licha ya kuondoka madarakani, wote waliotajwa kwenye ripoti ya uchunguzi wafikishwe mahakamani na kuagiza chama hicho kuacha kufanya biashara, badala yake kisimamie maslahi ya wakulima na kuhamasisha kilimo cha zao hilo.
“Kila aliyetajwa kwenye ripoti kuhusika na ubadhirifu, hakuna kuachwa, lazima afikishwe mahakamani. RPC hakikisha unaondoka na ofisa shughuli ambaye ni miongoni mwa viongozi waliotajwa kwenye ripoti ili aende akafunguliwe mashataka.
“Matatizo haya yametokana na SONAMCO kujiingiza kwenye biashara na kusahau majukumu yenu ya msingi ya kusimamia na kuhamasisha kilimo, hivyo muache kufanya biashara na kurejea kwenye majukumu yenu,” aliagiza.
Alimtaka Mrajisi wa mkoa huo, kuvisimamia vyama vya ushirika, ikiwemo kutoingilia uchaguzi wa viongozi wa vyama hivyo.
Awali, Waziri Mkuu Majaliwa alitembelea kiwanda cha kukausha tumbaku cha Ushirika huo, ambacho kilisimamisha uzalishaji tangu mwaka 2004, kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo.
Aliuagiza uongozi wa mkoa kuwasiliana na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kupatiwa maelezo kuhusu jitihada zinazofanywa za kukifufua.
Ofisa Biashara wa kiwanda hicho, Stella Lugongo, alisema mashine za kiwanda hicho zipo kwenye hali nzuri na kinaweza kuvutia wawekezaji.
Alisema tayari wawekezaji wawili wamejitokeza kuwekeza kwenye zao hilo mkoani Ruvuma, ambazo ni kampuni za British America Tobacco na Philip Modern International (PMI).
Aliongeza kuwa katika maombi yaliyotumwa na kampuni hizo, kuna dosari kadhaa zilizojitokeza, hivyo wametakiwa kuzifanyia marekebisho kwa kuzingatia zaidi maslahi ya taifa.
Kutoka Iringa, Mwandishi Wetu, Anita Boma anaripoti kuwa, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, ameamuru kunyang’anywa kwa matrekta tisa yaliyokuwa yakimilikiwa na viongozi wa Muungano wa Vyama vya Msingi vya Tumbaku (ITCOJE).
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kugundulika kuwa matumizi yake ni ya kifisadi na tofauti na makubaliano na wanachama.
Mbali na kuwanyang’anya matrekta viongozi hao na kutaka yawe yanamilikiwa na wanachama wa vyama vya msingi vya Tumbaku, Mwigulu amevunja uongozi wa ITCOJE na kutaka wanachama wachague viongozi wapya kuanzia katika vyama vyao vya msingi.
Mwigulu alifikia uamuzi huo juzi, alipokuwa akiongea na wakulima wa Tumbaku mkoani Iringa, katika mkutano ulioandaliwa na viongozi wa wilaya na mkoa, ambao ulikuwa na lengo la kutatua migogoro ya ndani na changamoto za wakulima katika zao la Tumbaku.
Aidha, alichukua uamuzi wa kutaka matrekta yanyang’anywe baada ya kupata malalamiko ya wakulima wadogo kuwa yanatumika tofauti na makubaliano, kutokana na viongozi hao kumiliki matreka kama ya kwao huku wakijua walikopa matrekta yale katika Benki ya CRDB kupitia vyama hivyo vya msingi.
Ilibainika kuwa viongozi wakiongozwa na Mwenyekiti wa ITCOJE, Msafiri Pamagila, walikopa matrekta katika benki hiyo kwa kutumia mwamvuli wa vyama vya msingi halafu deni likimalizika wanajimilikisha wao, kitu ambacho kilipingwa na wanachama kwani fedha inayokatwa kulipa deni hilo ni fedha za wakulima kutoka vyama hivyo vya msingi.
Mwigulu alisema viongozi hao wameshindwa kujibu nani mmiliki halali wa matrekta hayo, kati ya vyama na viongozi, ambapo viongozi hao walijichanganya kwa wengine kudai ni mali yao huku baadhi wakidai ni mali ya chama na kuwa wakifanya kazi vizuri wanategemea kumilikishwa.
“Hivyo kutokana hali halisi, huu ni utapeli na ufisadi. Haiwezekani mkakopa kupitia mwamvuli wa vyama na mkopo unalipwa na wanachama kukatwa, halafu deni likiisha mnajimilikisha kwa kuwa tu mlitunza vizuri, hamuoni mnaowanea wanachama wenu ambao wao ndiyo wanaoumia zaidi halafu nyinyi mchukue tu,” alisema.
Aliongeza: "Huu ni ufisadi mkubwa kwa viongozi kuwageuza wakulima wenzao kuwa vibarua kwa kutumia vyeo vyao kukopa na kulipiwa na wakulima, jambo ambalo si la kuvumilika, hivyo ninaamuru kuanzia kadi za mkopo hadi umiliki uende kwenye vyama vya msingi na kama kuna anayedhani hili azigo si sahihi, ajitokeze. "
Waziri Mwigulu alisema hawezi kuhalalisha utapeli wakati wakulima wadogo ndio wanaoumia, hivyo mbali na matrekta hayo, aliwataka viongozi hao kukabidhi ofisi na mali halali ya vyama vya msingi vya wakulima wa tumbaku na kutaka viongozi wapya wachaguliwe mara moja.
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera, aliwaweka chini ya ulinzi viongozi wawili wa chama cha Kiwem, Valentino Nyavi na Seth Mvela na kulitaka Jeshi la Polisi kuwahoji kutokana na kuhusika katika ubadhirifu wa matumizi mabaya ya fedha katika chama chao .
Awali, Mkuu wa Wilaya akimkaribisha Mkuu wa Mkoa ili amkaribishe Waziri Mwigulu, aliwataka wakulima wa tumbaku kuacha kuwatumikisha watoto katika mashamba yao.
No comments:
Post a Comment