Tuesday, 15 November 2016
KISUKARI TISHIO NCHINI
ASILIMIA 9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25-64, wana ugonjwa wa kisukari na asilimia 80 ya wagonjwa wote wa kisukari duniani wanaishi katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
Hadi mwaka 2015, hapa nchini kulikuwa na wagonjwa wa kisukari 822,880.
Utafiti wa ugonjwa wa kisukari unaonyesha kuwa, mwaka 2007, kulikuwa na wagonjwa milioni 246, duniani na takwimu za 2015, kutoka kwenye Atlas ya kimataifa ya kisukari zinaonyesha kuwa, kulikuwa na wagonjwa milioni 415 duniani kote.
Aidha, ifikapo mwaka 2040, inatarajiwa kuwa na wagonjwa milioni 642, ambapo katika Bara la Afrika, kutakuwa na wagonjwa wa kisukari milioni 14.2 2015 na idadi hii itaongezeka hadi kufikia milioni 34.2.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, katika tamko la Siku ya Kisukari Duniani, ambayo huadhimishwa Novemba 14.
Waziri Ummy alisema utafiti uliofanyika 2012 na kuhusisha wilaya 50, nchini ulionyesha kuwa, asilimia 9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25-64, wana ugonjwa wa kisukari.
Aidha, takwimu za watoto wenye kisukari 2015 ni kati ya asilimia 15 mpaka 20 ya wagonjwa wote wa kisukari nchini, ambao wanatibiwa kwenye kliniki huku wengine wakiwa hawajitokezi kwenye kliniki kwa sababu mbalimbali, ikiwemo imani potofu, gharama, umbali wa huduma za afya na ukosefu wa elimu ya juu ya tatizo hilo.
“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwamo kisukari, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, kansa na magonjwa sugu ya mfumo wa hewa, yameongezeka kwa kasi na kuchangia zaidi ya asilimia 50 ya mzigo wa magonjwa duniani, kutokana na gharama kubwa za matibabu, ulemavu na vifo,”alisema.
Alisema maadhimisho hayo yalianza rasmi 1991 na mashirika mawili ya kimataifa ya International Diabetes Federation [IDF] na World Health Organization (WHO), baada ya kuona ugonjwa wa kisukari una ongezeko kubwa duniani.
“Ugonjwa wa kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa kuwa sukari hutumiwa na mwili ili kupata nishati lishe na ili mwili uweze kutumia sukari inayotokana na vyakula, unahitaji kichocheo cha insulin,”alisema.
Alisema Insulin husaidia sukari kuingia kwenye chembechembe hai ili kutengeneza nishati lishe, ambapo ugonjwa wa kisukari unasababishwa na kichocheo hicho kupungua au kutofanya kazi kama inavyotakiwa.
Alisema wananchi wengi hawajitambui kuwa wana ugonjwa huo na wengine wana dalili, lakini hawachukui hatua mapema.
"Dalili za kisukari ni rahisi kuzitambua, nazo ni kiu isiyoisha, kukojoa mara kwa mara, kupungua uzito, kusikia njaa kila wakati na mwili kukosa nguvu. Ukiwa na dalili mojawapo kati ya hizi ni muhimu kuwahi hospitali," alisema.
Alisema kutokana na kasi ya ongezeko la ugonjwa huo, kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani 2016 ni 'Macho yote kwenye Kisukari', ikiwa na lengo la kufumbua macho zaidi ili kuongeza nguvu katika kuhakikisha kinga na tabia katika ulaji unaofaa, kufanya mazoezi, kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi na matumizi ya tumbaku.
Alisema ulaji unaofaa ni pamoja na kula chakula mchanganyiko cha kutosha kukua na kuwa na uzito wa kawaida na virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini.
Ummy alisema ulaji usiofaa ni kula chakula bila kuzingatia aina na kiasi kulingana na mahitaji ya mwili, ikiwemo kula vyakula vyenye mafuta mengi, hasa yale yatokanayo na wanyama, kula vyakula vyenye chumvi nyingi, sukari nyingi, kula chakula kupita kiasi, kukoboa nafaka na kutokula mboga mboga na matunda kiasi cha kutosha.
"Kutofanya mazoezi ya mwili, uzito na unene uliozidi, msongo wa mawazo, huweza kusababisha ulaji usiofaa na huweza kufanya mifumo mbalimbali ya mwili kutofanya kazi vizuri. Pia, matumizi ya pombe husababisha kuongeza uzito," alisema.
Kutoka Mbeya, Solomon Mwansele anaripoti kuwa, Daktari bingwa wa Idara ya Tiba, Hospitali ya Rufani ya Mkoa Mbeya, Mtui Graham, amesema uzito mkubwa unamweka mtu kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kisukari.
Amesema haitakiwi mtu kuwa na uzito mkubwa kuliko ule unaokubalika na kuwataka watu kuachana na ile dhana potofu kwamba, ukiwa na uzito mkubwa ndiyo una hali nzuri ya kiafya, jambo ambalo siyo sahihi.
Dk. Mtui aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na gazeti hili, lililotaka kujua mambo mbalimbali kuhusu ugonjwa wa kisukari, ambao maadhimisho yake yalifanyika duniani kote jana.
Alisema ili kukabiliana na ugonjwa huo, ni vyema watu wapunguze kuwa na uzito uliopindukia, waanze kufanya mazoezi kwa wale wenye kisukari na wasionacho, kwani kiafya mtu anatakiwa afanye mazoezi.
Dk.Mtui aliongeza kuwa mazoezi ni jambo lolote lile ambalo linahusisha misuli ya mwili, ambayo itasababisha mapigo ya moyo kuongezeka na hali ya upumuaji kuongezeka kwa hiyo mazoezi yapo ya aina nyingi.
Alisema ili mazoezi yawe na faida kiafya, ni lazima mtu afanye mazoezi angalau siyo chini ya dakika 30, kwani akifanya chini ya dakika hizo, yanakuwa hayana faida ya kiafya na kwa wiki yenye siku saba, ni vizuri kufanya mazoezi kwa siku tano.
Aliongeza kuwa kitu kingine cha kuzuia mtu asipate ugonjwa wa kisukari, ni kupunguza unywaji wa pombe kupita kiasi.
“Tuachane na kunywa hizi juisi bandia, unywaji wa soda uliopitiliza kwani hivyo vyote vinahatarisha mtu kupata ugonjwa wa kisukari, kwa hiyo kwa kifupi wananchi wanatakiwa kuziepuka zile tabia hatarishi, si lazima ukiwa na uzito mkubwa utapata ugonjwa huu, lakini unakuwa kwenye hatari,” alisema.
Dk. Mtui alisema zaidi wanawasisitiza watu wapime ili kujua hali zao kiafya, kwani wakati mwingine ugonjwa hauna dalili, njia pekee ya mtu kuweza kujua kuwa anao ugonjwa wa kisukari ni kupima na hilo huwa linafanyika ndani ya dakika kumi tu mtu anapata majibu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment