Tuesday, 15 November 2016

DK. SHEIN ATIA SAINI SHERIA YA GESI NA MAFUTA


RAIS wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, ametia saini Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia ya Zanzibar na kusema kuwa, wanaoikosoa hatua hiyo ni watu wenye choyo na wasioitakia mema Zanzibar.

Akizungumza baada ya kutia saini sheria hiyo, Dk. Shein aliwaeleza viongozi na waandishi wa habari kuwa, sheria hiyo Namba 6 ya mwaka 2016, inaipa Zanzibar mamlaka ya kisheria ya kuendeleza rasilimali ya mafuta na gesi asilia, ambapo kabla ya hapo haikuwa nayo.

Katika hotuba yake, Dk. Shein alisema kitendo cha kutia saini sheria hiyo hakijavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano kama baadhi ya watu wanavyodai.

“Hakuna aliyevunja sheria, anayevunja sheria wala atakayevunja sheria, lakini kama wao wanadai kutia saini sheria hii ni kuvunja sheria, watafute suluhisho la kisheria,” alisema Dk. Shein na kuongeza kuwa, watu hao wanatafuta umaarufu.

Aliwashauri wenye mawazo hayo wakasome vizuri Sheria ya Mafuta Namba 21 ya 2015, iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo imeweka msingi imara wa kisheria wa kutambua kuwa rasilimali ya mafuta na gesi asilia ni miongoni mwa mambo yaliyoorodheshwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo yanahitaji usimamizi bora na imara wa kisheria.

Dk. Shein alifafanua kuwa, sheria hiyo imeainisha mambo makuu matatu, ambayo ni shughuli zote za mafuta na gesi asilia kwa upande wa Tanzania Bara, ambazo zitasimamiwa na taasisi zilizoanzishwa ndani ya Sheria namba 21 ya 2015.

Sheria hiyo inatamka pia kuwa, shughuli zote za mafuta na gesi asilia kwa upande wa Tanzania Zanzibar, zitafanywa na taasisi zitakazoanzishwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania Zanzibar.

Kuhusu mapato yatokanayo na shughuli hizo za mafuta na gesi asilia, Dk. Shein alisema sheria hiyo inatamka kuwa kwa upande wa Tanzania Bara, mapato yatatumiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa faida ya Tanzania Bara, wakati kwa upande wa Tanzania Zanzibar, mapato hayo yatatumiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa faida ya Zanzibar.

Dk. Shein alieleza kwa kirefu mchakato mzima wa kupitishwa Sheria Namba 21 ya 2015 na kusisitiza kuwa, mamlaka zote husika zilishirikishwa kikamilifu, ikiwemo mashauriano kati ya viongozi wakuu, vikao vya baraza la mawaziri, Baraza la Mapinduzi, wanasheria wakuu wa Zanzibar na Tanzania Bara.

“Kila upande ulishiriki kikamilifu katika mchakato huu. Tulifanya mashauriano ya kina, sisi viongozi na tukapata ushauri wa kutosha kutoka kwa wanasheria wetu wakuu hadi kufika bungeni na kupitisha sheria hiyo,” Dk. Shein alisema.

Alikumbusha kuwa sheria hiyo ya utafutaji mafuta na gesi asilia ya Zanzibar ni matokeo ya kupitishwa kwa Sheria 21 ya 2015, ambayo iliipa Zanzibar uwezo wa kutunga sheria zake za kusimamia rasilimali hiyo.

Dk. Shein alisema sheria hiyo ni mpya na anaelewa changamoto, ambazo zinaweza kutokea, lakini akatoa wito kwa wananchi kuiunga mkono na kushirikiana na serikali kuendeleza sekta hiyo.

“Mafuta ni jambo kubwa katika maendeleo, lakini pia yasipotumika vyema, yanaweza kuitikisha nchi,”alionya Dk. Shein.

Aliwatahadharisha wananchi kutotegemea mafanikio ya haraka kutoka sekta hiyo kwa kuwa mbali ya uwekezaji wake kutumia fedha nyingi, hata faida ya moja kwa moja ya sekta hiyo inachukua miaka mingi hadi kufikia 10.

Alipongeza hali ya maelewano ambayo imekuwepo tangu hatua za mwanzo za mashauriano kuhusu suala hilo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Katika mnasaba huo, Dk. Shein alisema kutia saini sheria hiyo kunafungua milango kwa kampuni na wawekezaji, ambao wangependa kushiriki katika kuendeleza sekta hiyo Zanzibar.

“Wako waliokuja kwetu kabla ya kutaka kushiriki katika kuendeleza sekta hii,  lakini tukawajibu kuwa bado hadi mazingira ya kisheria yatakapokuwa tayari; sasa tuko tayari, tunawakaribisha,”alisema Rais Dk. Shein.

Hafla hiyo iliyofanyika Ikulu, Zanzibar, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, wakiwemo mawaziri, wanasheria wakuu na makatibu wakuu.

Miongoni mwa waliohudhuria ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania,  George Masaju na ujumbe kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC).

No comments:

Post a Comment