SERIKALI imepiga marufuku hospitali binafsi
zinazotoa huduma za vipimo, kupata gawio la malipo kutoka Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF), kwa wagonjwa wanaoagizwa na hospitali za serikali kwenda
kupima katika hospitali hizo.
Aidha, imeiagiza ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali
kutoa orodha ya dawa zote za asili, ambazo zimethibitishwa katika ofisi hiyo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla, alitoa agizo hilo juzi, wakati
alipofanya ziara ya kushtukiza katika Taasisi ya Kansa ya Ocean Road na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Akiwa katika Hospitali ya Ocean Road, Dk.
Kigwangalla alibaini kuwepo kwa ulaghai wanaofanyiwa wagonjwa wanapotumwa
kutoka hospitali za serikali kwenda kupima katika hospitali za watu binafasi,
ambapo zimekuwa zikiwaongezea idadi kubwa ya vipimo ili kunufaika na makato ya
NHIF.
Dk. Kigwangalla alisema hospitali za watu binafsi
zinapopokea wagonjwa walioagizwa na
hospitali za serikali kupata
vipimo, ni lazima zitekeleze maagizo yaliyotolewa na daktari na sio kwenda kinyume.
Katika hatua nyingine, Dk. Kigwangalla aliuagiza
uongozi wa taasisi hiyo kumuorodheshea changamoto zote muhimu ili kuzitafutia
ufumbuzi.
Miongoni mwa changamoto hizo ni ununuzi wa mashine
za vipimo na tiba za kansa, ikiwemo PECT, yenye uwezo wa kuzalisha kemikali za kutibu maradhi ya
kansa, ambapo hivi sasa taasisi hiyo inaagiza kemikali hizo kutoka Afrika Kusini.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Julius
Mwaiselange, alisema taasisi ina uwezo wa kutibu wagonjwa 180 hadi 200, kwa
siku na kwamba hivi sasa wanatibu wagonjwa180 kutokana na ukosefu, uchakavu na
kuharibika mara kwa mara kwa mashine za tiba na vipimo.
Akiwa katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk.
Kigwangalla, alimuagiza Mkemia Mkuu, Profesa Samwel Manyelle,
kuwasilisha orodha ya dawa zote za tiba mbadala zilizothibitishwa ili kuwabana
na kuwachukulia hatua watengenezaji holela wa dawa hizo.
Hata hivyo, aliitaka ofisi hiyo kuwa na hifadhi ya
kutosha ya kumbukumbu kwa njia ya teknolojia ili kurahisisha utendaji wake.
Kwa upande wake, Profesa Manyelle alimueleza Dk.
Kigwangalla kuwa, ofisi hiyo iko katika hatua ya kuboresha huduma zake ili
ziweze kukidhi mahitaji ya wananchi.
No comments:
Post a Comment