Monday 21 September 2015

MATHAYO AMZIMA NYERERE, WAFUASI 3,800 CHADEMA WATUA CCM




Na Mwandishi Wetu, Musoma

KUJITOKEZA  kwa  mgombea   ubunge    wa  jimbo   la  Musoma   Mjini   kupitia   ACT Wazalendo,  Eliud  Tongoara (Mkorea) kumesabisha  mpasuko  mkali ndani ya CHADEMA, hatua  ambayo  imesababisha zaidi  ya  wanachama  na mashabiki  3,800  kukihama  chama hicho  na kujiunga na CCM  katika  mikutano mitatu ya  CCM.

Wanachama  hao  na  mashabiki  wajiunga  na CCM kwa  nyakati  tofauti,  katika mikutano  ya  uzinduzi wa  kampeni  za CCM,  ambayo  ilifanyika viwanja vya  shule  ya  Sekondari  ya  Mara, Kata  ya Nyamatare, Bweri  na  Kata  ya  Nyasho  mjini  mjini hapa.

Baadhi  ya  wanachama hao  wakizungumza wakati wakijiunga  na CCM), walidai kutoridhishwa na mchakato wa mgombea ubunge wa Chadema, Vicent Nyerere, kwa kumuengua Eliud Tongora,  ambaye  alilazimika kujiunga na ACT Wazalendo.

“Kwa  vile  baadhi  ya  viongozi wa  Chadema walitanguliza ubinafsi na chuki  kwa kumuengua ‘Mkorea’,  sasa  na sisi  tumeamua  kuingia CCM  ili tuone  wao  walimwaga mboga, sisi tumemwaga ugali, tuone nani mshindi,” alisema Magafu Willison, mkazi wa Nyasho.

“Tumeamua kujiunga na CCM na si ACT  Wazalendo ili  tusionekane tumemfuata Mkorea, sasa tunajiunga na CCM na tutahakikisha hakuna kulala hadi ushindi unapatikana,” alisema Pendo James, mkazi wa Mwisenge.

Akihutubia  katika  mkutano  wa kampeni  katika viwanja vya  kituo cha mabasi  Nyasho, mgombea ubunge wa CCM, Vedastus  Mathayo, alitangaza   kutoa  sh. milioni  200  kwa   kila   kikundi   cha   wanawake    huku    vikundi    vya   vijana   vikiwezeshwa   sh. milioni  50  kama    mitaji ya  biashara,    ikiwa  ni moja    ya   mkakati     wake     wa   kupambana    na  umasikini     kwa    wananchi    wa   jimbo    hilo   kwa   vitendo.

Mathayo, ambaye    pia  ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, alisema    amepanga  kupambana     na    umasikini    kwa   vitendo   kwa   kuwataka    vijana    na   wanawake kuunda    vikundi    hivyo   ili    kuwezeshwa    mitaji    hiyo    kuanzia    Januari,   mwakani.

Alisema kwa   sasa   taratibu    maalumu   zinandaliwa    katika  kusaidia   makundi   mengine    katika   jamii    yakiwemo    ya   wazee.

Alisema endapo  atachaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba  25,  mwaka huu, suala la kupambana na umasikini kwa wananchi wa jimbo la Musoma Mjini ni la kufa  na kupona,  ikiwa ni pamoja na kubuni mikakati mipya ya kupambana na ajira  kwa vijana.

“Nimepanga kuanzia Januari, mwakani, tuanzishe kambi maalumu ya vijana bila kujali itikadi za vyama vyao kwa ajili ya kuwapa mafunzo maalumu ya ujasiriamali, ufundi na ujuzi mwingine ili baada ya kuhitimu waweze kupatiwa mitaji na kujiajiri wenyewe,” alisema Mathayo.

Mathayo  amewataka   wananchi   wa   jimbo   la  Musoma  Mjini,   kufanya   uamuzi    kwa   kupima   maendeleo,   ambayo   yamefanywa    wakati   jimbo   hilo,  likiongozwa   na   mbunge    wa  CCM katika   kipindi   cha   mwaka  2005-2010   na   2010-2015  wakati    likiongozwa   na  upinzani badala   ya   kupiga   kura   kwa   ushabiki  wa  kisiasa.

No comments:

Post a Comment