CHAMA cha CUF mkoani Geita, kimeweka
msimamo kwamba kitamchagua mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli ili awe Rais wa
awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutokana na kutokuridhishwa
na jinsi makubaliano ya UKAWA yalivyokiukwa.
Kauli hiyo ilitolewa jana, na
mgombea ubunge wa CUF katika Jimbo la Geita Mjini, Michael Peter Malebo, wakati
akiomba kura kwa wakazi wa mji wa Geita, mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa
stendi ya zamani ya mji wa Geita.
Mgombea huyo alisema yeye ndiye
alikuwa ameteuliwa na UKAWA kupeperusha bendera ya umoja huo kupitia CUF,
lakini alishangaa kuona baadaye anateuliwa mgombea mwingine, Rogers Luhega
kutoka CHADEMA na hivyo kuamua kuchukua fomu kugombea kupitia CUF.
Alisema kitendo cha viongozi wa
ngazi za juu kukubali kumteua Rogers kuwa mgombea badala yake, ni uhuni na
alikataa kukubaliana nao.
Malebo alisema yeye na Chama chake
cha CUF mkoani hapa wamekubaliana wamchague Dk. Magufuli aongoze Taifa na
kusisitiza kuwa mikutano yao yote ya kampeni watawahimiza wananchi wa Geita
kumchagua Dk. Magufuli.
"Ndugu wananchi wote wa Geita
mchagueni John Pombe Magufuli kwa maendeleo ya Taifa. Sisi CUF hatumuungi
kabisa mkono Lowassa wa CHADEMA, natoa wito wakazi wote wa Geita mchagueni
Magufuli tu maana tumefanyiwa uhuni.
"Hapa ni kazi tu, chaguo letu
sahihi ni Magufuli, nawasihi sana wananchi msimchague Lowassa na UKAWA yao bali
mtu wa kazi na hata mimi mwenyewe kwa upande wa ubunge mkiona kura hazitoshi,
basi kura zangu zote mpeni Costantine Kanyasu mgombea wa CCM katika jimbo hili,“
alisema Malebo.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
CUF Wilaya ya Geita, Shaban Makunga, kabla ya kumkaribisha mgombea huyo kupanda
jukwaani, alisema wao baada ya kutafakari wamebaini viongozi wao ngazi ya Taifa
wamewafanyia uhuni.
Kutokana na hilo, alisema hawako
tayari kuendelea na umoja huo huku akisema chaguo lao sahihi ni Magufuli na
watatumia nguvu zao zote kumnadi kila wanakokwenda.
No comments:
Post a Comment