UGOMVI wa kugombea majimbo na kata baina ya wanachama wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umezidi kushika kasi na kutishia kupasua
umoja huo.
Hali hiyo ilidhihirika katika mkutano wa kampeni za
UKAWA jimbo la Ukonga, Chanika, Magengeni, Dar es Salaam jana, ambapo mgombea
urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, alikuwa akihutubia sambamba na kutambulisha
wagombea udiwani na ubunge wa jimbo hilo.
Awali, wakizungumza na Uhuru, wafuasi wa CHADEMA wa eneo
hilo, walisema kumekuwa na mvutano mkali kuhusu nafasi za wagombea udiwani,
hali iliyowalazimu kuwaacha wagombea wenye mvutano wasimame wote.
"Kutokana na hali hiyo CCM (Chama Cha Mapinduzi),
hakitakuwa na kazi kubwa katika kata zote 12 za jimbo, maana tumeshagawanyika
hivyo ushindi kwao ni mweupe.
"Lakini sisi (CHADEMA), ndio tuliohangaika sana
kujenga chama katika jimbo hili, wenzetu CUF walikuwa wamelala tu, hata
uhamasishaji kujiandikisha BVR ni sisi ndio tulifanya, mimi peke yangu nilitoa
80,000, ila wenzetu wanataka kutumia nguvu yetu,"alisema Joyce Chacha,
ambaye ni mama lishe katika eneo hilo la Chanika Magengeni.
Mpasuko huo uliwalazimu viongozi wa CHADEMA kuugeuza
ajenda badala ya sera za uchaguzi.
Alipopata nafasi ya kupanda jukwaani, Mwenyekiti wa
CHADEMA, Freeman Mbowe, alimtaka mgombea ubunge wa jimbo la Ukonga, Mwita
Waitara, kulishughulikia tatizo hilo ndani ya siku moja na kuwafukuza wote
watakaokaidi maagizo.
Katika kauli zake za vitisho, Mbowe alisema wameshafanya
maamuzi kila eneo la ubunge na udiwani asimame mtu mmoja, hivyo ni marufuku
kujitokeza wawili.
Katika mkutano huo, ambao ulijaa wafuasi wa CHADEMA bila
kuhusisha vyama vingine, kauli hiyo ya Mbowe ilizua minong'ono ya chini kwa chini na kuanza kudhihakiana wenyewe kwa
wenyewe.
"Kila nafasi mtu mmoja, tatizo la kugombea nafasi ya
ubunge au udiwani haliruhusiwi, jimbo hili tulishasema atasimama Waitara na
katika nafasi za udiwani viongozi wenu wa jimbo watatoa majina ya wanaostahili
kusimama kwenye kata.
"Kama kuna wagombea wengine, ajue kabisa
hawakilishi Ukawa, asimame mwenyewe, na atakayekaidi afukuzwe tu,"alisema
Mbowe katika kauli zake za kujihami.
Katika hali ya kushangaza na kutapatapa, aliyekuwa
Waziri Mkuu, Frederick Sumaye na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro
Mahanga walitoa kauli za kujikaanga wenyewe.
Kwa upande wake, Mahanga alisema aliwahi kuwa mbunge wa
jimbo la Ukonga kabla ya kugawanywa na kupatikana jimbo la Segerea, na kwamba
tangu alipoondoka jimboni humo, hakuna maendeleo.
Alisema alikuwa Naibu wa Waziri wa Kazi, lakini hakuna
kazi kwa vijana, kauli ambayo inamfunga kwamba utendaji wake ulikuwa ni mbovu.
Hata hivyo, Ukonga na Segerea zinaelezwa zilikuwa kwenye
vipindi vigumu vya ukosefu wa maendeleo wakati Mahanga akiwa mbunge katika
majimbo hayo, hali iliyowalazimu wananchi kumuengua kwenye kura za maoni za CCM
jimbo la Segerea, na yeye kukimbilia CHADEMA.
Sumaye, ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10,
aliwashangaza watu alipodai hakuna maendeleo yaliyofanyika na viongozi ni
wazembe.
Alisema kwa sasa hakuna matumaini labda mtu awe mwizi
ama mpenda magendo na kuwataka wananchi kufanya mabadiliko ama waiache CCM
madarakani.
Akimalizia mkutano huo, Lowassa alitoa kauli ambazo
zinaonyesha dhahiri akiingia madarakani, nchi itakuwa kama jalala.
Alisema ataruhusu shughuli nyingi zifanyike popote
wakiwemo wamachinga, bodaboda na mama lishe,
hali inayotishia ustawi wa taifa kutoweka, kwa sababu kila kitu lazima
kifanyike kwa utaratibu na si holela kama alivyotangaza yeye.
No comments:
Post a Comment