Monday, 14 September 2015
AZZAN: MSIKUBALI MABADILIKO YASIYOKUWA NA MPANGILIO
NA KHADIJA MUSSA
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Kinondoni (CCM), Iddy Azzan, amewataka Watanzania kuwa makini na kukataa mabadiliko yasiyokuwa na mpangilio kwani yanaweza kusababisha machafuko kama ya Libya na Syria.
Azzan, ameiomba serikali ya awamu ya tano kutoa kipaumbele katika Hospitali ya Mwananyamala, ambapo amesema licha ya hospitali hiyo kuboreshwa, bado imeelemewa kutokana na kupokea wagonjwa wengi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za jimbo la Kinondoni, katika mkutano uliofanyika viwanja vya CCM Mwinjuma, Mwananyamala, Azzan alisema mabadiliko bora ni yale yanayofanywa kwa mpangilio.
Mgombea huyo alisema haiwezekani mtu anakurupuka na kuwahadaa wananchi kuwa wawachague kwa dhumuni la kutaka mabadiliko bila ya kufafanua ni ya aina gani, hivyo aliwashauri wananchi kuwaepuka kwa kuwa mabadiliko yao yana madhara.
Azzan alisema wananchi hawana budi kupuuza kelele zinazotolewa na wapinzani wanaodai kuwa wanataka mabadiliko bila ya kufafanua yatapatikanaje, jambo ambalo linaonyesha kuwa ni walaghai na hawafai kuchaguliwa.
Kwa mujibu Azzan, CCM imefanya mabadiliko makubwa ya maendeleo katika sekta mbalimbali ndani ya jimbo hilo, ambayo yanaonekana na yameweza kubadilisha maisha ya wananchi kiuchumi, kiafya na kielimu.
Kuhusu suala la afya, Azzan aliipongeza serikali kwa kuipandisha hadhi hospitali hiyo kuwa ya rufani ya mkoa.
Mgombea huyo alisema bado hospitali hiyo inatakiwa kupewa kipaumbele kwa kuwa imeelemewa na wagonjwa wengi.
“Badaa ya kupata mafanikio makubwa katika ujenzi wa shule za sekondari za kata, kwa sasa tunajipanga katika ujenzi wa shule za kidato cha tano na cha sita,”alisema.
Kuhusu suala la wafanyabiashara ndogo ndogo, bodaboda, mama na baba lishe, alisema atahakikisha wanaendelea kuwajengea mazingira mazuri ili waweze kufanya shughuli zao bila ya kubughudhiwa.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda, aliwaomba wananchi wa jimbo hilo kumchagua Azzan kwa kuwa ni makini na ambaye amechangia kwa kiasi kikubwa wilaya hiyo kusonga mbele kimaendeleo.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Salum Madenge, aliwataka wananchi hao kutowachagua wapinzani kwa sababu hawana msimamo na hawaeleweki, hivyo wakichaguliwa watakuwa wanajirudisha nyuma kimaendeleo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment