Monday, 14 September 2015
MAPUNDA ATAKA WANAOMSHABIKIA LOWASSA WAPUUZWE
NA DUSTAN NDUNGURU, MBINGA
WATU wanaomshabiki Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, wanapaswa kupuuzwa kutokana na kumbebesha mzigo ambao kamwe hawezi kuubeba.
Kauli hiyo ilitolewa jana na mgombea ubunge wa jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma, Sixtus Mapunda, alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika viwanja vya Sokoni mjini hapa.
Mapunda alisema wafuasi wa Lowassa na wananchi kwa ujumla wanapaswa kufahamu kuwa kuongoza nchi sio jambo la mchezo kama wanavyodhani.
Alisema baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakipoteza muda mwingi kuyasema maneno ambayo hayana mashiko kwa taifa hivyo kinachotakiwa kwa Watanzania ni kufikiria kwa umakini mkubwa kabla ya kufanya maamuzi.
Kwa mujibu wa mgombea huyo, kiongozi ambaye anang’ang’ania kuingia Ikulu kwa udi na uvumba, ni lazima watu kwanza wamtafakari na kujua kitu kinachomsukuma kufanya hivyo, si vinginevyo.
Alisema vyama vya upinzani hasa UKAWA, havina dhamira ya dhati ya kuwaongoza Watanzania, bali wanachokitafuta ni kuingia Ikulu ili wajinufaishe wao wenyewe na kuwaacha wananchi wakiteseka.
“Kama kweli wana nia ya kufanya mabadiliko, mgombea wa UKAWA alikuwa waziri mkuu, lakini hakuna cha maana alichokifanya zaidi ya kujihusisha na mambo mabaya yaliyosababisha ajiuzulu.
“Kwa sasa navionea sana huruma vyama vya NCCR na NLD kwa kuingizwa kwenye mkenge na CHADEMA, kwani baada ya Oktoba 25, mwaka huu, vyama hivi vitapoteza mwelekeo kabisa,najua CCM kitashinda na kuendelea kushika dola na kuwaacha hawa jamaa wakipoteana,”alisema.
Aliwataka wananchi wa jimbo hilo kuwachagua wagombea wanaotokana na chama makini CCM ili kiendelee kuwatumikia kwa kuwaletea maendeleo ya kweli, kama inavyoelekezwa katika Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2015 hadi 2020.
Mapunda alisema iwapo atachaguliwa kuongoza jimbo hilo katika kipindi cha miaka mitano ijayo, atahakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama inakwisha na pia atashirikiana na wananchi katika kufanikisha ujenzi wa zahanati katika kila kijiji na kituo cha afya kwa kila kata.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment