Monday, 14 September 2015

DK. MAGUFULI AAHIDI KUBORESHA BEI YA TUMBAKU

NA MWANDISHI WETU, IGUNGA

MGOMBEA Urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, ameahidi kuleta neema kwa wakulima wa zao la tumbaku kwa kuboresha bei ya zao hilo ili kuinua maisha yao.

Dk. Magufuli alisema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kampeni, uliohudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi wilayani Igunga mkoani Tabora.

Alisema ili kuinua maisha ya wananchi, hasa mkulima wa tumbaku wa Igunga na maeneo mengineyo hapa nchini, atahakikisha anaboresha bei ya zao hilo sambamba na kuondoa ushuru wa mazao ili kuwaondolea vikwazo vyote vinavyowakabili.

“Nasikitika bei ya pamba imeanza kushuka, lakini tatizo lililopo vyama vya wakulima vilivyo vingi vimedorora na havina nguvu. Nawaahidi nitamaliza tatizo hili mara tu mtakaponichagua kuingia madarakani,” alisema.

Mgombea huyo aliahidi kujenga viwanda vya nguo na nyuzi ili kuhakikisha pamba inayozalishwa nchini inaingia viwandani moja kwa moja, kuliko ilivyo sasa ambapo marobota ya pamba hupelekwa nchi za nje na kusababisha ujio wa bidhaa feki zilitengenezwa huko.

Alisema kujengwa kwa viwanda kutachochea ongezeko kubwa la ajira kwa vijana hapa nchini, soko la mazao ya wakulima, sanjari na kuinua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla, hali itakayosaidia kupunguza kiwango cha umaskini.

“Ndugu zangu hatuwezi kumaliza tatizo la nyumba za nyasi kwa maneno tu, isipokuwa kwa kujenga viwanda, kushusha bei za vifaa vya ujenzi, kuboresha bei za mazao na kuwabana wafanyabiashara wakubwa kulipa kodi inayostahili na kutowabana wafanyabiashara wadogo,”alisema.

Aidha,aliahidi kujenga barabara ya kilomita nne kwa kiwango cha lami katika wilaya ya Igunga ili kupunguza barabara za vumbi zilizoko katika mitaa mbalimbali ya mji huo.

Dk. Magufuli alisema atatumia mbinu mbadala itakayosaidia kumaliza tatizo la maji katika wilaya hiyo kwa kujenga mabwawa makubwa ambayo yatahifadhi maji kutoka mito mbalimbali iliyoko katika wilaya hiyo ikiwemo Mto Mbutu.

No comments:

Post a Comment