Wednesday, 2 September 2015

MGOMBEA UBUNGE CHADEMA AMUOMBEA KURA MAGUFULI




NA PETER KATULANDA, MAGU
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Magu mkoani Mwanza kupitia CHADEMA, amemmwagia sifa kemkem mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli na kumuombea kura za kishindo.
Kalwinze Ngongoseke, amesema Dk. Magufuli ni mchapa kazi, anastahili kupata kura za kishindo na ili afanye kazi vizuri, wamchagulie wabunge safi akiwemo wa jimbo hilo na madiwani wachapa kazi.
Ngongoseka, alisema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni zake uliofanyika kwenye uwanja wa Mnada, mjini hapa, na kuwavunja mbavu wananchi wakiwemo wana CCM waliokwenda kumsikiliza.
Mgombea huyo miezi michache iliyopita alikuwa UDP, kabla ya kupigwa ‘stop’ na Mwenyekiti wake wa taifa, John Cheyo na kukimbilia mahakamani (mahakama ya wilaya ya Magu) kupinga kuvuliwa uanachama wa UDP.
Kauli hiyo iliwafanya wananchi wamshangilie na kuonekana kumvimbisha kichwa, bila kujali balaa litakaloweza kumpata kutoka kwa viongozi wa chama chake kipya.
“Tumchague Magufuli na ili afanye kazi vizuri, anastahili mbunge mahili kama…..” alikatishwa na shangwe za wananchi walioangua kicheko na kuzua gumzo uwanjani hapo, baadhi wakidai huyo ni CCM B.
Wakizungumza na Uhuru baada ya mkutano huo, baadhi ya wakazi wa Magu waliohudhuria mkutano huo walidai kuwa, Ngongoseke amewafurahisha kwa kumpigia debe mgombea urais safi, hodari, mchapa kazi wanayempenda wana Magu na wananchi wengi nchini.
“Nimefurahi na nadhani ndiyo maana hata wengine wamemshangilia maana amempigia debe mgombea safi Dk. Magufuli, tunayemhitaji wana Magu awe rais wa Tanzania,” alisema mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa majina ya Daniel Andrew.
Alisema Dk. Magufuli katika hotuba zake, anawaomba wananchi wamchague pamoja na wagombea wenzake wa CCM, Magu watamchagulia mbunge wake wa CCM (akiwa na maana ya Bonaventura Kiswaga) na madiwani wa chama hicho ili iwe rahisi kuwawajibisha iwapo watashindwa kuendana na kasi yake.
Akizungumza katika ufunguzi wa kampeni za CCM wilayani humo, uliofanyika kwenye uwanja wa Mwana Nkanda mjini Magu, mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kutumia mifano ya Biblia Takatifu, Kiswaga alidai Magufuli ni sawa na dhahabu, Edward Lowassa sawa na vyombo visivyokuwa na heshima katika nyumba kubwa.
Alidai Dk. Magufuli anaweza kujenga nchi, lakini Lowassa atabomoa maana tayari alishaonekana ni  mtafuna nchi.
“Vitu vyote ni halali bali si vyote vifaavyo. Vitu vyote ni halali bali si vyote vijengavyo,” alinukuu waraka wa Wakorintho 1, 10:23-24 na waraka wa Pili wa Thimoteo 2:20.
Kiswaga, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, alieleza kuwa kipaumbele chake cha kwanza kwa wana Magu ni kuondoa kero ya maji katika mji huo na tayari amesimamia mipango ya mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya sh. bilioni 10, akienda bungeni atasukuma kero hiyo itatuliwe haraka.

No comments:

Post a Comment