Wednesday, 2 September 2015

DK. MAGUFULI ATAKA RASILIMALI ZA NCHI ZIWANUFAISHA WANANCHI






MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, akihutubia maelfu y wananchi kwenye mkutano wa kampeni, katika uwanja wa Mashujaa, mjini Mtwara, leo.

NA SELINA WILSON, NEWALA
WATANZANIA wametakiwa kulinda amani ya nchi na kuhakikisha rasimali za nchi ikiwemo gesi, mafuta na madini hazisababishi machafuko, badala yake ziwanufaishe wananchi wote.
Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, alisema hayo jana kwa nyakati tofauti katika mikutano ya kampeni za uchaguzi, aliyoifanya katika majimbo ya Newala, Tandahimba, Nanyamba na Mtwara  Vijijini.
Alisema Tanzania inazo rasilimali nyingi ambazo zikisimamiwa vizuri,  itakuwa nchi tajiri, lakini wapo baadhi ya watu hawafurahii kuona nchi ikipiga hatua, hivyo watafanya njama kuivuruga.
Dk. Magufuli aliwatahadharisha wananchi kuwa makini na watu wenye nia mbaya, ambao wanaweza kuwachonganisha wananchi kwa lengo la kuvuruga amani.
Alitoa mfano wa Libya, ambako hali ilikuwa shwari chini ya uongozi wa Kanali Muammar Gadafi, lakini wazungu walipoona neema ya mafuta, walivuruga kwa kuwagawa wananchi na kuivuruga nchi.
“Waliingia Libya na kuwagawa wananchi kwenye makundi zaidi ya 30, ambapo wananchi walianza kupigana wenyewe kwa wenyewe mpaka wakamuua rais wao,”alisema.
Dk. Magufuli alisema kutokana na machafuko hayo, wananchi wa Libya wamekuwa wakimbizi kwenye nchi yao, hawana amani, vijana wanakimbia hadi baharini wanakufa.
Aliwaomba wananchi kujenga umoja na mshikamano na kuiachia serikali ifanye kazi na kuhakikisha rasilimali za nchi zinaendelezwa kwa manufaa ya Watanzania wote.
“Msikubali kupotoshwa na baadhi ya wanasiasa wanaosema wataleta maendeleo kwa siku moja. Msikubali mtu afanye uchochezi kwa kuwa maendeleo hayawezi kupatikana kwa siku moja. Hata Mungu aliumba dunia kwa siku sita, siku ya saba akapumzika,”alisema.
Aliwaomba wazee na machifu wa mkoa wa Mtwara wawashauri vijana watunze amani kwa kuwa ikitoweka, kuirejesha ni kazi kubwa na kwa kuwa zipo nchi zilichezea amani kwa miaka mingi wameshindwa kuirejesha.
“Tusikubali kushawishiwa, wanataka mpigane ili waje  kuchimba gesi. Panapokosekana amani hakuna maendeleo, hapawezekani kujengwa viwanda, watu watashindwa kuishi kwenye nyumba zao. Tusikubali kuingia kwenye uchochezi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli alisema atasimamia na kuwahakikisha mahali ilipopatikana gesi, wananchi wake wanakuwa wa kwanza kunufaika kwa kupata huduma mbalimbali muhimu ikiwemo fursa za ajira.
“Huwezi  ukawa na gesi hapa halafu wananchi walio kwenye gesi wanashindwa kunufaika,” alisema na kusisitiza kwamba Tanzania ya Magufuli lazima wananchi wanufaike.
Alisema tayari kumeanza kuwa na fursa ikiwemo ujenzi wa kiwanda kikubwa cha saruji cha Dangote, ambacho kimeanza kutoa ajira na kitapunguza kabisa bei ya saruji.
Dk. Magufuli alisema akipata ridhaa pia atahakikisha anashusha bei ya vifaa vya ujenzi, ikiwemo saruji, mabati na nondo ili wananchi wapate maendeleo kwa haraka.
Mbali na viwanda, Dk Magufuli  alisema atahakikisha kunakuwa na viwanda vya korosho hapa nchini na wakulima hawatauza korosho ghafi kwa kuwa mapato yake yanakuwa kidogo.
“Mimi nimesomea korosho Shahada ya Uzamivu(PHD), hakuna atakayenidanganya. Korosho ina faida kubwa na sio mbegu tu, pia maganda yake yana faida yanaweza kutengenezwa  gundi na yanaweza kutengenenezwa kemikali ya kuzuia kutu,”alisema.
Kuhusu bei ya korosho, alisema ni ndogo kwa kilo ambapo kwa sasa ni sh. 300, hivyo wakulima wakijengewa uwezo wa viwanda zikabanguliwa na kutengenezwa nchini vizuri, watapata bei kubwa zaidi.
Alisema pia kuwa ataendelea kujenga barabara za lami ili kuhakikisha wananchi wanaweza kusafirisha mazao yao kwenye masoko, ikiwemo barabara ya  Mtwara/ Newala/Masasi kwa kiwango cha lami umbali wa kilometa 200.
Dk. Magufuli akiwa katika Kijiji cha Kitama, aliwataka wananchi kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), ambapo alimuona mtoto albino, Riziki Rashid na kumpatia shi. 100,000 kwa ajili ya kununua vifaa vya shule na mafuta ya ngozi.
Akizungumza baada ya kupokea fedha hizo, baba wa mtoto huyo, Faraji Rashid, alimshukuru Dk. Magufuli na kumueleza kwamba amepokea fedha hizo na anamkabidhi Mungu.
Akiwa katika kijiji cha Lidumbe, Dk. Magufuli alilazimika kusimamisha msafara wake na kwenda kuhani msiba wa mkazi wa eneo hilo, Zainab Abdallah.
“Ndugu zangu poleni  kwa msiba, binadamu wanazaliwa na kufa. Nimepita hapa nikaona watu wamekusanyika nikalazimika kusimama. Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu,”alisema Dk. Magufuli na kutoa ubani  kwa wafiwa.
Akiwa katika eneo la Ziwani, Jimbo la Mtwara Vijijini, Dk. Magufuli alimfagilia mgombea wa ubunge wa jimbo hilo, Hawa Ghasia kwamba ni mchapa kazi na mwenye ghasia kwenye masuala ya maendeleo.
Alisema alimsumbua kuhusu kivuko cha Msanga Mkuu mpaka wakakinunua kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa eneo hilo, ambao walikuwa na changamoto kubwa kwenye usafirishaji.
Dk. Magufuli aliwaomba wananchi wampigie kura ili washirikiane kuleta maendeleo na kutatua changamoto za sekta ya afya, maji, elimu,nishati na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Alisema serikali yake itaendelea kuimarisha huduma za afya kwa kujenga vituo vya huduma ikiwemo zahanati kwenye  vijiji, vituo vya afya kwenye kata na hospitali za wilaya na kwamba ataboresha huduma ili wananchi watibiwe ndani ya nchi badala ya kupelekwa nje.
“Watu wanauliza Magufuli atayaweza haya, Ninachoweza kusema ni nchi hii ina utajiri mkubwa, lakini kuna watu wachache waliokuwa wanautumia vibaya, lakini katika uongozi wangu nitasimamia rasilimali za nchi ziwanufaishe Watanzania wote,”alisema.
Dk. Magufuli aliwanadi wagombea ubunge wa Newala Mjini, Kapteni Mstaafu George Mkuchika, Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia na Tandahimba, Shaibu Likumbo, ambao nao walipata nafasi ya kumuombea kura na kumuhakikishia ushindi wa kishindo.

No comments:

Post a Comment