NA MWANDISHI WETU
UMOJA wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), umeviomba
vyombo vya habari nchini viache
kuwachagulia Watanzania viongozi, badala yake watangaze sera za vyama na sifa
za wagombea.
Ombi hilo lilitolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Abubakar
Karsan wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa Mwandishi wa
Habari wa Channel Ten, Daud Mwangosi, yaliyofanyika katika Hotel ya Peacock,
Dar es Salaam.
Mwangosi alifariki
dunia Septemba 2, mwaka 2012, eneo la Nyororo, mkoani Iringa, wakati
akiwa anatimiza majukumu yake kama mwandishi wa habari.
Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Karsan alisema vyombo vya
habari vimekuwa vikiwachagulia na kuwaambia Watanzania wamchangue mtu fulani
nzuri na mwingine mbaya.
Alisema kazi ya vyombo vya habari ni kuwaeleza Watanzania
uzuri na ubaya wa sera za vyama pamoja na sifa za wagombea kutokana na mambo
waliyoyafanya huko nyuma.
Karsan, aliwataka wandishi wa habari kuacha kujiingiza katika kazi ya kuchagua na wasipige kura
kwenye magazeti, redio na televisheni,
badala yake watawachagua wenyewe Oktoba 25, mwaka huu.
Kwa upande wake, Rais wa UTPC, Kenneth Simbaya, aliwaomba
waandishi wa habari wasiwe na upande wowote badala yake wafanyekazi huku
wakijua wanafanya kazi iliyotukuka.
Pia, aliwataka waandishi wa habari wazingatie maadili ya
uandishi wa habari na kwamba kujiingiza katika mambo hayo watakuwa wanakwenda
kinyume na maadili.
Simbaya alisema kuna wengine wanachangia katika mitandao ya
kijamii, wamejisahau kuwa ni waandishi wa habari, hivyo aliwaasa waache kuchanganya
siasa na habari.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa UTPC, Jane Mihanji, aliwataka
waandishi wa habari kuwa wamoja na kwamba wasipokuwa wamoja, wataendelea
kulaumiana.
No comments:
Post a Comment