Thursday, 3 September 2015
CCM YAMSHUKIA MBATIA
NA CHRISTOPHER LISSA
KATIBU wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba 'Gaddafi', amemshukia Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa, James Mbatia, kuwa ni mtu asiye na chembe ya aibu wala shukrani.
Juma amesema Mbatia umekosa adabu na uungwana kiasi cha kuthubutu kumnyoshea kidole Rais Jakaya Kikwete, ambaye alimpa ubunge wa Viti Maalumu.
Alimshangaa Mbatia kutoa kauli za uchochezi na shutuma kwa Rais Kikwete, kwamba hathamini vyama vya upinzani huku akisahau kuwa bila yeye kumpa ubunge wa viti maalumu, asingekuwa chochote hapa nchini.
Akihutubia mamia ya wananchi waliofurika katika viwanja vya Chama, Boko, wakati akimnadi mgombea ubunge wa jimbo la Kawe kwa tiketi ya CCM, Kippi Warioba, Juma alisema Mbatia ni mtu asiyejitambua kwamba thamani aliyonayo hivi sasa inatokana na mchango wa Rais Kikwete ambaye alimpa ubunge wa viti maalumu.
"Mbatia hana fadhila. Bila ya Rais Kikwete kumkumbuka, asingekuwa pale alipofikia na NCCR yake. Amshukuru rais kwa kumnusuru. Hivi kweli Mbatia anaweza kuongea nini juu ya Rais Kikwete? Bila ya rais, Mbatia bunge angekuwa analisikia tu. Eti leo anatamka hadharani kuwa hakuna demokrasia kwa vyama vya siasa hapa nchini. Huyu ni mtu wa aina gani?" alihoji.
Aidha, Juma alimshukia Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA) kuwa, amewatelekeza wananchi wa jimbo hilo kwa sababu hana familia, hivyo hajui uchungu walionao wananchi hao juu ya mahitaji yao muhimu.
"Hivi Halima amewahi kuwaonyesha mumewe? Hawezi kujua shida za kina mama kwa sababu hata kwenye chumba cha kuzalia hajawahi kuingia. Hana familia, hivyo hajui kabisa mahitaji ya wananchi. Ndiyo maana huko bungeni, tukisema tulete barabara Kawe, yeye kazi yake ni kupinga. Tukisema tulete maji, anapinga. Anapinga shughuli zote za maendeleo na kuwaacha wananchi wanateseka,"alisema.
Alisema Warioba ni chaguo sahihi kwa wananchi wa Kawe na ambaye atawaletea maendeleo ya haraka kupitia Ilani ya CCM ambayo alikabidhiwa.
"CCM inaongozwa na Ilani ambayo Warioba atakuwa akifuata muongozo wake na kutekeleza. Ilani ya mwaka huu ni nzuri na imelenga kuwakomboa wananchi, hivyo Oktoba 25, mwaka huu, nafasi ya urais mpeni Dk. John Magufuli na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan, ubunge ni Kippi Warioba na chagueni madiwani wote wa CCM ili kuharakisha maendeleo,”alisema Juma.
Naye Warioba, ambaye ni mtoto wa Jaji Mstaafu, Joseph Warioba, alisema ana nia na ari ya kuwaongoza wananchi wa Kawe, lakini kikubwa ni kulirejesha jimbo hilo mikononi mwa CCM kutoka CHADEMA.
"Nitatekeleza Ilani ya CCM ili kuhakikisha kuwa wananchi wangu wa Kawe wanafaidi rasilimali zilizopo. Naamini kuwa Ilani hii ya CCM itabadili maisha ya wananchi katika jimbo hili na kufungua ukurasa mpya wa maendeleo ya haraka. Naombeni kura zenu siku ya Oktoba 25, mwaka huu, ili CCM iweze kuibuka na ushindi wa kishindo.
“Lakini pia ninawahimiza wananchi wa Kawe, kumchagua kwa kura nyingi mgombea wa urais, Dk. Magufuli na mgombea mwenza Samia, pamoja na madiwani wote ambao wataunda baraza letu la madiwani," alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment