Friday, 8 January 2016

RAIS MAGUFULI AKUTANA NA KUTETA NA MKAPA, WARIOBA




RAIS Dk. John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba.

Akizungumza baada ya mazungumzo hayo yaliyofanyika jana, Ikulu, mjini Dar es Salaam, Rais mstaafu Mkapa alisema lengo la kukutana na Rais Magufuli ni kumpongeza kwa dhamana aliyopewa na Watanzania kuiongoza nchi, kuunda serikali na kumtakia heri ya mwaka mpya.

Mkapa alimhakikishia Rais Dk. Magufuli kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano wakati wote ama kufanyakazi yoyote endapo atahitajika kufanya hivyo. Kwa upande wake, Jaji Warioba pamoja na kumtakia heri ya mwaka mpya, alimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa jinsi alivyoanza kazi vizuri, hususan katika kusimamia ukusanyaji wa mapato, kubana matumizi na kuelekeza matumizi kwenye maeneo muhimu, ambayo yanawahusu wananchi yakiwemo afya na maji.

Jaji Warioba alisema Watanzania wanapaswa kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kazi kubwa anazofanya, ambazo ni kukomesha rushwa, ufi sadi, matumizi mabaya ya madaraka na wizi wa mali ya umma.

“Lazima kila mmoja amuunge mkono Rais, tusije tukamuacha peke yake, kama ni mambo ya rushwa tuanzie hapo hapo, kama ni mambo ya matumizi mabaya ya madaraka, tuanzie hapo hapo, tusije tukamuachia Rais pekee yake. Yeye awe kiongozi wetu, lakini Watanzania wote tushughulike na matatizo hayo,” alisema.

No comments:

Post a Comment