Friday, 8 January 2016
MSHITAKIWA WA KWANZA KESI YA MAUAJI YA DK. MVUNGI AFARIKI
MSHITAKIWA wa kwanza, Chibago Magozi, katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi, amefariki dunia. Taarifa za kifo hicho zilipatikana jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati shauri hilo linalomkabili Magozi na wenzake lilipokuja kwa kutajwa.
Shauri hilo lilitajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, ambapo upande wa jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Credo Lugaju, alidai upelelezi haujakamilika. Baada ya kudai hayo, mmoja wa washitakiwa katika kesi hiyo alidai mwenzao huyo amefariki dunia.
Kutokana na taarifa hiyo, Hakimu Simba alielekeza askari wa Magereza, kufuatilia cheti cha kifo cha mshitakiwa huyo. Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 19, mwaka huu, litakapokuja kwa kutajwa.
Magozi alikuwa mahabusu katika gereza la Keko. Washitakiwa wengine katika shauri hilo ni Longishu Losingo, Juma Kangungu, Msungwa Matonya, Mianda Mlewa, John Mayunga, Masunga Makenza, Paulo Mdonondo, Zacharia Msese na Ahmad Kitabu.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao wanadaiwa Novemba 3, mwaka 2013, eneo la Msakuzi Kiswegere, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, kwa pamoja na kwa makusudi walimuua Dk. Mvungi. Washitakiwa hao wapo rumande kwa kuwa shitaka linalowakabili halina dhamana.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment