Friday, 8 January 2016
MIMI BADO RAIS ZANZIBAR-DK. SHEIN
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema bado ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na wasioiamini wapeleke shauri hilo Mahakama Kuu ya Zanzibar ambayo ndiyo pekee yenye uwezo wa kutafsiri Katiba.
Alibainisha kuwa anaongoza nchi kwa mujibu wa katiba na sheria na kwamba kama si uwezo huo aliopewa kikatiba hana sababu ya kuendelea kukaa madarakani na serikali anayoingoza.
“Tuko madarakani na uongozi wote wa serikali. Yupo Makamu wa Kwanza wa Rais, Makamu wa Pili wa Rais na mawaziri,” alisema Dk. Shein na kuongeza kuwa hao wanaodai kujiondoa serikalini huo ni uamuzi wao wenyewe.
Alibainisha kuwa yeye na serikali anayoingoza kuendelea kuwepo madarakani ‘si uamuzi wake’ na wala yeye hana ‘ubavu’ wa kujiweka madarakani bali ni katiba ambayo inajieleza wazi. Dk. Shein alitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Kusini, Pemba katika siku yake ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu kisiwani humo kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi.
Aliwaambia wananchi hao kuwa yako mengi yanayosemwa, lakini hawapaswi kuyasikiliza kwa kuwa kama ni serikali yeye ndiye rais, hivyo wanapaswa kumuamini anachowaeleza. ìYa mjini yapo yasikilizeni, lakini kwa serikali mimi ndiye Rais na nisiposema mimi nitawatuma wasaidizi wangu kuwaeleza,î alisema Dk. Shein.
Alifafanua kuwa kama ni suala la CCM yeye ndiye Makamu Mwenyekiti Zanzibar na kama kuna la kuwaeleza wana CCM na wananchi atawaeleza yeye na viongozi wenzake wa Chama na taarifa za vikao vya chama chake. Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa ushindani wa kisiasa si ugomvi bali ni utaratibu wa kupeana changamoto katika uongozi ambao lengo ni kuwaletea wananchi maendeleo.
“Tusikejeli maendeleo yetu, tuthamini chetu na ushindani wetu wa kisiasa usirejeshe nyuma maendeleo yetu,” Dk. Shein alitahadharisha.
Dk. Shein alirejea wito wake wa kuwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo yameanza na yanatarajiwa kufi kia kilele Januari 12, mwaka huu.
Aliwakumbusha wananchi hao kuwa Mapinduzi ya Zanzibar ambayo yaliyomfanya Rais wa kwanza wa Zanzibar Mzee Abeid Amani Karume, kutangaza Jamhuri ya Zanzibar, ndiyo yaliyowakomboa wanyonge wa Zanzibar kwa kuondosha aina zote za ubaguzi na kuwapa mamlaka ya kujiamulia mambo yao. Dk. Shein aliwaeleza wananchi wa Pemba kuwa meli mpya iliyonunuliwa na Serikali MV. Mapinduzi II ambayo ilizinduliwa hivi karibuni, itawasili kisiwani humo Januari 10 na siku itakayofuata itawachukua baadhi ya wananchi kwenda Unguja kushiriki maaadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi.
Alisisitiza kuwa serikali itawalipia gharama za usafi ri wa kwenda na kurudi Unguja wale wote watakaoteuliwa kuwemo kwenye safari hiyo kufuatana na utaratibu utakaowekwa kama alivyokuwa ameahidi wakati meli hiyo ilipokuwa inatengenezwa Korea ya Kusini.
Katika ziara hiyo, Rais Dk. Shein alifuatana na viongozi mbalimbali wa serikali wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu na wabunge.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment