Na Mwandishi Wetu, Manyoni
WAZIRI wa zamani na
Mbunge Mstaafu wa Manyoni, Kapteni John Chiligati, amewalipua mawaziri wakuu wa
zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, ambao wamejiengua CCM na kujiunga
na upinzani.
Akizungumza kwenye
mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa urais wa CCM kwenye viwanja vya CCM
Wilaya ya Manyoni, mjini hapa, Chiligati alisema kitendo kilichofanywa na
wanasiasa hao ni cha usaliti mkubwa.
Alisema anashangazwa
na kauli zilizokuwa zikitolewa na wanasiasa hao kabla hawajaondoka CCM, ambazo
zimeonyesha kuwa ni wanafiki wakubwa na hawapaswi kuaminiwa.
“Wakati wa harakati
za kuwania urais, Lowassa alisema asiyempenda na anayemchukia aondoke CCM.
Lakini hilo limekuwa kinyume kwani ni yeye aliyeondoka.
“Alipokuwa akitoa
kauli hiyo alionekana ana mapenzi ya dhati kwa CCM, lakini kitendo chake cha
kuondoka kimeonyesha alivyo kigeugeu,” alisema.
Kwa upande wa
Sumaye, alisema naye ameonyesha kuwa kigeugeu na unafiki wa hali ya juu
kutokana na kauli zake kwamba anamchukia Lowassa na kwamba CCM ingempitisha
kuwa mgombea urais, angejiondoa kwenye Chama.
“Lakini ukweli umeonekana
wazi kwamba alichokuwa akisema sicho alichokuwa akimaanisha. Badala yake
amemfuata yule aliyekuwa akisema hafai kuongoza Tanzania. Huu ni unafiki wa
hali ya juu,” alisema.
Chiligati pia
aliwashangaa wapinzani kwa unafiki ambapo walikuwa wakisema Lowassa ni miongoni
mwa mafisadi, lakini baada ya kutemwa kugombea urais, wamemchukua na kumteua
kugombea.
Kutokana na hali
hiyo, alisema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa wapinzani ni wasanii na
hawapaswi kupewa uongozi wa nafasi yoyote kwani hawajakomaa.
Chiligati, ambaye
aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi; Kazi, Vijana na Ajira na
baadaye Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alipasua jipu kwa kusema
wananchi wa Manyoni watamchagua mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, kwa
kuwa ni mchapakazi na mtu wa vitendo.
“Hivi mmewahi
kusikia habari zozote za kashfa dhidi ya Magufuli?” alihoji na kujibiwa:
“Hakuna”. Aliendelea kuuliza: “Hivi mliwahi kusikia Magufuli ana chembe zozote
za ufisadi?” alijibiwa “hapana”.
Kutokana na majibu
hayo, aliwaambia wananchi wa Manyoni kuwa kamwe wasifanye kosa kwa kufanya
majaribio kwa kuuchagua upinzani bali wamchague Magufuli pekee ili aendeleze
gurudumu la maendeleo.
Alisema Magufuli
amejenga barabara ambapo sasa Manyoni inafikika kwa urahisi na pia serikali ya
CCM imefanya mambo makubwa.
000000
No comments:
Post a Comment