Sunday, 30 August 2015

TUNDU LISSU ALIPULIWA NDANI YA NGOME YAKE



Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia Suluhu Hassan, akimnadi mgombea Ubunge, wa Bahi Omari Badwel, mkutano wa kampeni uliofanyika leo kaika jimbo la Bahi mkoani Dodoma
Mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, akihutubia wakati  wa mkutano huo.

 
Wananchi wakiwa katika shamrashamra kumpokea Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia alipowasili jimbo la Bahi kuhutubia mkutano wa kampeni
NA EPSON LUHWAGO, IKUNGI
WANANCHI wa Jimbo la Singida Mashariki, wametakiwa kutorudia makosa ya kuchagua tena mbunge wa upinzani kwa kuwa kufanya hivyo ni sawa na kurudia makosa na kuendelea kuwa masikini.
Wakati hayo yakielezwa na Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Tundu Lissu (CHADEMA), ameelezwa kuwa hafai kuwa kiongozi kwa vile ni mchochezi na mtu aliyekwamisha maendeleo ya wananchi.
Kila aliyekuwa akisimama kuzungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha Makiungu, kilichoko katika jimbo hilo, wilaya ya Ikungi, alikuwa akimshambulia Lissu kwa kila namna.
Aliyeanza kufungua jukwaa la mashambulizi dhidi ya kinara huyo wa CHADEMA ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Singida, Martin Lissu, ambaye alisema Lissu ni sumu ya maendeleo kwa wananchi wa Singida Mashariki.
“Tundu Lissu alishajitangazia kwamba Singida Mashariki ni jamhuri yake hivyo hakuna wa kumng’oa. Huyu ni mwanasheria na anajua kuwa kujitangazia jamhuri ndani ya jamhuri (Tanzania) ni kosa la jinai.
“Ndugu zangu wana Singida Mashariki, najua mlifanya kosa kwa kumchagua mtu ambaye amelirudisha nyuma jimbo kimaendeleo. Sasa umefika wakati wa kuhakikisha tunalirejesha jimbo kwa CCM. Kufanya kosa si kosa bali kurudia kosa, mchagueni Jonathan Njau, mtoto wenu kipenzi,” alisema.
Baada ya mwenyekiti huyo, alifuatia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kutoka Rombo, Evod Mmanda, ambaye alimwanika na kumwacha akiwa ‘mtupu’.
Mmanda alisema anamfahamu  vyema Lissu na kwamba uwezo wake wa kuongoza ni mdogo, hivyo kuendelea kumchagua kuwa mbunge ni sawa na kutafuta matatizo.
“Wana Singida Mashariki tokeni kwenye mchepuko (upinzani) mrejee kwenye njia kuu (CCM). Mwenzangu amesema kufanya kosa si kosa, lakini mimi nasema mlifanya kosa kumchagua Tundu Lissu.
“Ninamfahamu Njau miaka 15 iliyopita ni mtu mwelewa na mpenda maendeleo. Tundu Lissu namfahamu tangu akiwa kidato cha nne, ni mtu msanii na mhamasishaji wa fujo, kamwe ndugu zangu wa Singida msifanye makosa ya kumrejesha madarakani,” alisema.
Mmanda alisema Lissu amekuwa akihamasisha wananchi wasishiriki katika shughuli za maendeleo kama vile kuchangia miradi ya elimu na afya, jambo ambalo limesababisha jimbo hilo kuwa nyuma kimaendeleo.
“Wana Ikungi mnahitaji madaktari, wahandisi na wataalamu wa kilimo na mifugo kwa vile ninyi mnajishughulisha na mambo haya. Sasa kama mtu anakataa kuchangia maendeleo, anataka mkose madaktari na wanasayansi ili muendelee kuwa masikini. Hakika mtu huyu anayeitwa Tundu Lissu si mzuri na hapaswi kuchaguliwa kabisa,” alisema.
Aliongeza: “Tundu Lissu hana nia ya dhati ya kuwanedeleza wana Singida Mashariki. Watoto wake wanasoma shule nzuri zenye maabara, lakini anataka ninyi msiwe nazo. Hiyo ni haki?”
Naye Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mary Maziku, alimwelezea Tundu Lissu kuwa ni mtu asiye na nia ya dhati ya kuwaletea wananchi wa Singida Mashariki maendeleo.
“Kama mnakumbuka ndugu zangu, huyu Lissu aliwahi kuwahamasisha wananchi wafukie kisima cha maji kwa madai kuwa analeta mabomba ya maji. Wananchi wale walifanya hivyo, lakini hadi sasa zaidi ya miaka mitano hakuna mabomba,” alibainisha.

SAMIA AHITIMISHA
Baada ya mashambulizi hayo, Samia alihitimisha kwa kusema wananchi hao wamejifunza, hivyo wasiendelee kukubali hadaa za Lissu, ambaye alimwelezea kuwa si mpenda maendeleo.
Alisema kosa walilolifanya wananchi wa Singida Mashariki kwa kuchagua upinzani limekuwa funzo kwao, hivyo wanapaswa kubadilika na kuchagua wagombea wa CCM ambao wana nia ya dhati ya kuleta maendeleo.
“Mmesikia wenyewe habari zake kutoka kwa watu wanaomfahamu. Sasa tubadilike na kuichagua CCM kwani huo ndio mpango mzima. Tundu Lissu anakaa Dar es Salaam kwenye umeme, maji na barabara nzuri, lakini amewatekeleza tangu mlipomchagua,” alisema.
Samia aliwakumbusha wananchi hao kuwa maendeleo hayaletwi na watu kutoka nje kama ambavyo wanadanganywa kuwa wasichangie maendeleo, badala yake wanapaswa kuchangia ili kuunga mkono serikali katika kusambaza huduma mbalimbali za kijamii.
“Nina imani kuwa mtu mzima anadanganywa mara moja tu. Na hivyo ndivyo ambavyo alifanya Tundu Lissu kwenu. Sasa mmejifunza na hamtarudia kosa hilo kwa kumchagua ili muendelee kudidimia kimaendeleo,” alisititiza.
Kuhusu maendeleo ya jimbo hilo, Samia alisema kwenye Ilani ya Uchaguzi, serikali ijayo ya CCM itahakikisha inaendeleza miradi ya elimu, afya, barabara na kusambaza umeme katika vijiji vyote.  
00000

No comments:

Post a Comment