Monday, 31 August 2015

MAGUFULI ATANGAZA KUIFUMUA SERIKALI


 
Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akihutubia wakazi wa kijiji cha Itundu kata ya Mlangali ambapo alisema kuwa endapo ataingia madarakani atahakikisha atatoa elimu bure mpaka kidato cha nne,ataboresha huduma za afya pamoja na kuhakikisha haki za msingi za wakulima, walimu na wafanyakazi zitaboreshwa.


Wananchi wa Madaba wakimsikiliza Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli.

Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akiwasili kwenye uwanja wa Fisi kata ya Madaba ambapo alihutubia wakazi wa Madaba kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni na kuahidi kuwa serikali yake itatengeneza Tanzania Mpya .
Jenista Mhagama (MB) akihutubia wakazi wa Jimbo la Madaba kwenye uwanja wa Fisi ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaaga rasmi.
Mbunge wa Jimbo la Ludewa Ndugu Deo Filikunjombe akihutubia wakazi wa kijiji cha Itundu, kata ya Mlangali kwenye uwanja wa MTC ambapo aliwaambia wananchi wa kata hiyo kumpigia kura Dk. John Pombe Magufuli kwani ni kiongozi pekee mwenye dhamira ya kuleta maendeleo 

 Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akiwa amembeba mtoto Shadrack haule mara baada ya kumaliza kuhutubia wakazi wa Ludewa mjin

NA SELINA WILSON, LUDEWA
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema anakusudia kufanya mabadiliko makubwa ndani ya serikali na chama ili kujenga Tanzania mpya.
Pia, ametangaza kiama kwa vigogo wote waliochukua viwanda kisha kuvitelekeza bila kuviendeleza na kusababisha wananchi kukosa ajira, kujiandaa kuchukuliwa hatua baada ya serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani.

Dk. Magufuli aliyasema hayo kwa nyakati tofauti katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu katika maeneo ya mbalimbali ya wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
“Sijaomba nafasi hii kwa majaribio. Ndugu zangu nimegombea urais nikiwa na nia thabiti ya kuwatumikia Watanzania kwa kuwa najua changamoto zinazowakabili, najua shida zenu,” alisema.
Alisema anataka kubadilisha utendaji uwe wa kusimamia mambo na kuleta mabadiliko ya haraka katika shughuli za maendeleo na kwamba, watendaji waliozoea kufanya kazi kwa mazoea hawatakuwa na nafasi.
Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, matatizo madogo madogo ndio yanawafanya wananchi waichukie serikali, hivyo katika utawala wa serikali ya awamu ya tano, atahakikisha kero za wananchi zinaondolewa.
“Serikali yangu itakuwa ya watu makini wanaoujua kusimamia kazi. Itakuwa ni serikali ya watu waadilifu wanaomjua Mungu,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema kero ya Watanzania si kuwa na vyama vya siasa bali ni kupata maendeleo ya haraka na kwamba, maendeleo hayo yataletwa na wananchi kwa kufanya kazi kwa bidii chini ya uongozi wa serikali makini ya awamu ya tano.
Aliwataka wananchi wasikubali kupotoshwa na wanasiasa wanaotoa ahadi kwamba, wakiingia madarakani wataleta kila kitu jambo ambalo ni uongo kwa kuwa maendeleo yanaletwa kwa watu kuwajibika kufanya kazi.
Dk. Magufuli aliwaomba wananchi wamuamini na wampe kura za kutosha ili aweze kutekeleza azma yake ya kutengeneza Tanzania mpya yenye maendeleo.
Alisema katika utendaji wake hatabembeleza mawaziri bali atakuwa anawaagiza kazi na atakayechelewa kutekeleza wajibu wake hatokuwa na nafasi yake.
Akiwa katika Kijiji cha Mlangali, Dk. Magufuli aliahidi wananchi kwamba serikali yake itajenga barabara ya lami kutoka Njombe hadi Ludewa na kwamba upembuzi yakinifu na usanikifu wa kina umefanyika.
Alisema hatua inayofuata ni kumpata mkandarasi  na kwamba kukamilika kwa barabara hiyo kutafungua fursa za kibiashara na kwamba kuna shughuli za uchumi zinazoendelea, hivyo barabara hiyo itakuwa kipaumbele cha kwanza akiingia Ikulu.
Dk. Magufuli alisema wataanza na kilometa 50. Alimpongeza Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe kwa kuwa ni mtu wa kufuatilia mambo na kusimamia maendeleo ya wananchi wake.
“Hongera Filikunjombe, nimesikia umepita bila kupingwa. Mimi nilipita bila kupingwa miaka 10 mfululizo sasa na wewe  umeshakuwa Magufuli. Nakuahidi kwamba serikali ya awamu ya tano itakuletea lami,”alisema.

WALIOHUJUMU VIWANDA KITANZINI
Kuhusu walioshindwa kuendeleza viwanda, Dk. Magufuli alisema siku akiingia Ikulu ndio itakuwa mwisho wa waliochukua viwanda na kuvitelekeza na kuwaacha Watanzania hususan vijana wakiwa hawana ajira.
Alisema anataka viwanda vyote vifanye kazi na serikali yake itahakikisha kila mkoa unakuwa na viwanda ili watu wafanye kazi na kukuza uchumi.
"Viwanda ambavyo havijaendelezwa virejeshwe ili tuvifungue vifanye kazi vijana wapate ajira. Najua ninaowasema hadharani hawatanipa kura, lakini lengo langu ni kuleta maendeleo," alisema.
Alisema hataki aje kusutwa na Watanzania kwa vile changamoto ni nyingi na hapendi watu wa chini wanyanyaswe kwa kuwa hata Mungu hapendi.
Dk. Magufuli alisema kuna watu wamehodhi viwanda kwa kisingizio cha uwekezaji halafu hawaviendelezi. Alisema anataka wavirejeshe vitumike na wananchi wapate maendeleo.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Chama cha Walemavu, Amon Mpanju, aliwaomba wananchi waichague CCM katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu, ili iendelee kuongoza nchi.
Alisema CCM inawajali walemavu na kwenye Ilani yake ya Uchaguzi ya 2015-2020, imeeleza vizuri namna itakavyowawezesha walemavu ili nao wapate maendeleo.
Mpanju alisema Dk. Magufuli ni kiongozi bora na mtendaji wa kiwango cha kupigiwa mfano hivyo aliwaomba watu wenye ulemavu na wananchi wote bila kujali itikadi wampigie kura za ndio ili aingie Ikulu.


LUDEWA YALIPUKA
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli alipata mapokezi makubwa ya Tsunami, katika Mji wa Ludewa, ambapo wananchi wakiongozwa na vijana wa bodaboda walifurika katika uwanja wa mpira wa mjini hapo.
Akizungumza na wananchi, Dk. Magufili aliwashukuru kwa kujitokeza kwa wingi ambapo aliwaahidi kwamba akiingia madarakani, atatatua kero kubwa ya maji katika Mji wa Ludewa.
Alisema miradi ya barabara ndio inayochukua mabilioni ya fedha tofauti na maji, hivyo atahakikisha Ludewa  inapata maji ya uhakika ili wananchi waishi maisha bora.
Akizungumzia ulinzi na usalama, Dk. Magufuli alisema Rais Jakaya Kikwete katika utawala wake ameimarisha majeshi ya ulinzi na usalama  na yeye akiingia madarakani atahakikisha anaendelea kuboresha majeshi.
Dk. Magufuli alisema majeshi yote JWTZ, Polisi, Magereza, Uhamiaji  na mengine ili kuhakikisha yanafanya kazi zake vizuri, atayapatia vifaa vya kisasa na kuboresha makazi ya askari.

FILIKUNJOMBE: MAGUFULI MPANGO MZIMA
Akizungumza katika na wananchi, mgombea ubunge wa jimbo hilo, Deo Filikunjombe, alisema Dk. Magufuli ni njia kuu, hivyo wampigie kura za ndio kwa kuwa ni kiongozi makini na yeye anamuita Katapila.
Alisema mgombe wa CHADEMA ni sawa na mchepuko , hivyo asipewe nafasi na kwamba anachotaka Dk. Magufuli apate kura zote na Lowassa wa CHADEMA apate sifuri kwa kuwa ndio utaratibu wa wananchi.
“Mimi mnanifahamu huwa sipendi kusema uongo. Ludewa hatutaki uzuri, tunataka mtu anayefaa kuongoza nchi na kutatua kero zetu. Kero yetu kubwa ni maji, tunaomba hiyo iwe jambo la kwanza,” alisema huku wananchi wakishangilia.

No comments:

Post a Comment