HOTUBA ya mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho, imeendelea kupondwa kila kona, kutokana na kuwa dhaifu na iliyojaa uchochezi.
Aidha kwa hotuba hiyo, inaonyesha tayari Lowassa ameshindwa kukidhi matakwa ya Watanzania, ambapo wananchi waliokwenda kumsikiliza walionyesha kukerwa na kuondoka uwanjani hapo kabla ya mgombea huyo kumaliza kuzungumza.
Tofauti na ilivyotarajiwa Lowassa, ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu kutokana na kashfa ya Richmond, alitumia takriban dakika 11 kutoa hotuba yake, huku akishindwa kueleza ilani ya chama chake.
Pia alishindwa kuinadi na kuitetea Ilani ya CHADEMA mbele ya umati uliohudhuria uzinduzi huo kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambapo aliwataka kwenda kusoma hotuba yake kwenye mitandao, jambo ambalo lilionekana kuwakera wengi na wengine kuanza kuondoka.
Aidha katika hotuba yake, Lowassa alitangaza kuwa akiingia madarakani atawaachia huru kutoka gereza mwanamuziki Nguzu Viking na wanawe, ambao walitiwa hatiani kwa kuwabaka na kuwalawiti watoto.
Pia katika kile kinachoelezwa kutafuta kuungwa mkono ili apigiwe kura, Lowassa aliahidi kuwa atawaachia huru watuhumiwa na makosa ya ugaidi wanaoshitakiwa kwa makosa mbalimbali, ikiwemo mauaji ya viongozi wa dini na matukio ya kumwagia watu tindikali visiwani Zanzibar.
Katika kuonyesha kuwa hajajipanga na hafahamu ni kitu gani Watanzania wanataka, Lowassa aliahidi atamleta aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daud Balali, ambaye kwa sasa ni marehemu.
Balali alifariki dunia Mei 20, 2008 nchini Marekani, ambapo baadhi ya vyombo vya habari nchini vilikwenda nchini humo na kushuhudia kaburi alilozikwa.
“Nimeona bango pale…nimesikia, nitamtoa Babu Seya na Balali nitamrejesha,” alisema Lowassa.
Aidha katika kuonyesha UKAWA na mgombea wake hawajajipanga, mwanasiasa aliyepoteza mvuto, Tambwe Hizza, ndiye aliyemkaribisha Lowassa kuzungumza jukwaani badala ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.
Watu wengi walielezea kufurahishwa kao na mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, wakati wa uzinduzi wa kampeni zake, ambaye aliingia katika viwanja hivyo akionekana mwenye furaha na alitumia dakika 58 akizungumza na umati wa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na kueleza vipaumbele vyake na kuinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2015-2020.
SHAKA AWALIPUA
Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), umesema hotuba ya Lowassa aliyoitoa juzi, imedhihirisha kuwa mwanasiasa huyo amechoka na hawezi kuwa kiongozi wa taifa.
Umesema kuwa Lowassa alishindwa kuikabili hadhira hiyo na kuwaelezea malengo yake iwapo atakuwa rais na badala yake alibaki kuduwaa, huku akizungumza mambo ya hovyo kwa kushindwa kuelezea Ilani ya chama chake.
Taarifa ya UVCCM iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Kaimu Katibu Mkuu wake, Shaka Hamdu Shaka, imesema Lowassa na UKAWA wamedhihirisha kuwa ni wababaishaji na hawana mipango endelevu kwa ajili ya Watanzania.
“Ni dhahiri Lowassa ameshindwa uchaguzi mkuu mapema, amebakia akilalama, kupiga soga na kujenga matumaini hewa kwa Watanzania, huku akishindwa kujua ni changamoto zipi za msingi zinazowakabili.
“Ameshindwa kabisa kukonga nyoyo na kugusa hisia za Watanzania katika mambo ya msingi kwa sababu ya kuandamwa kwake na pupa, kiherehere na kukurupuka toka chama kimoja hadi kingine, huku akiwa hana maandalizi yanayoweza kutoa majibu halisi yanayowakabili wafanyakazi, wakulima, wavuvi, wafugaji, walimu, madaktari, wauguzi pia wasanii na wanamichezo,” alisema Shaka.
Alisema UVCCM ilitarajia kuona shauku na kiu alionayo Lowassa ya kutamani urais kwa gharama yoyote angekuwaa na mikakati, sera na mipango mipya ya kushughulikia matatizo ya watu, lakini hakuweza kueleza wala kuwa na suluhisho.
“Hotuba ya Lowassa kuhusu azma na dhamira yake katika kukuza uchumi, tunaifananisha na orodha ya ununuzi, maana haionyeshi viashiria , njia au vyanzo vya mapato ya kukuza uchumi kwa mwendo wa haraka wa kisera na kujikuta akipiga porojo.
“Ameshindwa kuzungumzia masuala ya ufisadi na kutowataja wezi waliopora rasilimali za umma na wala rushwa na masuala ya maadili ya uongozi, ikiwemo kashfa ya Richmond ambayo ilimsababishia kulazimishwa ajiuzulu uwaziri mkuu…amekuja na porojo ambazo ziliishia kuwakera watu na kuamua kuondoka,” alisema Shaka.
Alitumia fursa hiyo kuwaambia Watanzania kwamba mabadiliko na mageuzi ya kiuchumi na kisiasa hayahitaji pupa na papara, hivyo wawe makini na Lowassa.
Pia alisema kitendo cha Lowassa kutaka kuingilia maamuzi ya mihimili mingine ni dalili za kiongozi dikteta na asiyeheshimu misingi ya utawala bora.
Alisema kauli kuwa atawaachia huru watuhumiwa wa ugaidi ni ishara ya uchochezi na kwamba amekuwa akiirejesha mara kwa mara, licha ya suala hilo kuwa mahakamani kwa sasa.
Aidha, Shaka alitumia fursa hiyo kumuonya Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ambaye amejiunga na UKAWA, kukaa kimya, kwani kuna uchafu mwingi ameufanya na kwamba ana tuhuma za kujibu.
Alisema wameshangazwa na ujasiri uchwara ulionyeshwa na Sumaye pale alipothubutu kuzungumzia ufisadi wakati ni miongoni mwa viongozi wanaotuhumiwa kwa kashfa.
“Huyu akae kimya kabisa, asijaribu kujivisha ujasiri uchwara kuzungumza jukwaani…ni miongoni mwa wanaotuhumiwa na kashfa ya uanzishaji wa Televesheni ya Taifa, ufufuaji wa fedha za umma, soko la Kibaigwa, uporaji ardhi huko Tondoloni. Halmashauri nyingi nchini ziliongoza kupata hati chafu kwa matumizi holela ya ruzuku ya serikali ilivyofichuliwa CAG,” alisema Shaka na kuongeza: “Sumaye kinywa chake wakati mmoja kikitoa moto na baridi ndiye aliyekitaka CCM kutompitisha Lowassa kwa madai ana tuhuma za ufisadi huku akitishia kuhama CCM”.
Hamad Rashid: Lowassa ameonyesha udhaifu
MBOMBEA urais wa Zanzibar kupitia chama cha ADC, Hamad Rashid Mohammed, amesema anashangazwa na kusikitishwa na kitendo cha mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa kushindwa kuwaeleza wananchi sera na vipaumbele vyake.
Alisema kitendo cha Lowassa kimeibua hisia tofauti kwa wananchi ambao wengi walitarajia kusikiliza sera zake, lakini alishindwa kuzieleza.
Hatua hiyo inadaiwa kuwa ni kutokana na afya ya mgombea urais huyo ambayo inadaiwa kudhoofika na kushindwa kusimama kwa muda mrefu.
Katika uzinduzi huo, Lowassa alisimama jukwaani kwa dakika kumi huku akisingizia anahofia muda.
Akizungumza na Uhuru jana, Mohammed alisema wananchi walitarajia kusikiliza sera za Lowassa akizitaja hadhara, lakini alishindwa kufanya hivyo.
“Tulitarajia kumsikiliza na kufahamu sera zake, lakini jambo la kushangaza alishindwa kuzieleza na kuwataka wananchi wazisome kupitia tovuti ya CHADEMA.
“Kwa mwanasiasa kama Lowassa kitendo cha kutoeleza sera zake ni kujishusha na kuonyesha udhaifu mkubwa. Asifikiri kuwa watu wote wana muda wa kupitia tovuti, walitaka wasikie kauli yake ndio ingependeza sana,” alisema Mohammed.
Alisema katika hali ambayo haikutarajiwa na wengi, Lowassa hakupaswa kumzungumzia msanii Nguza Viking (Babu Seya), badala yake alitakiwa azungumzie sera zake.
“Sidhani kwamba Watanzania wanataka kusikia mambo ya Babu Seya, hata ukimuachia jamii itafaidikaje na utamuachia kwa kipengele gani kama si kuingilia mhimili mwingine. Hakutakiwa kuzungumzia kabisa ,yeye alitakiwa kuwaeleza wananchi atafanya nini,” alihoji.
Hata hivyo Mohammed alisema sera ya kutoa elimu bure si jambo la kujivunia la msingi ni kueleza kuwa litatekelezeka vipi.
Alidai zipo baadhi ya nchi zikiwemo la Famle za Kiarabu, wananchi wanasoma bure, lakini nchi hizo zina uchumi mkubwa kuliko nchi za Afrika.
“Unaposema utatoa elimu bure ya chuo kikuu, kwanza unatakiwa ueleze utaitetelezaje azma hiyo, siyo kuzungumza tu,” alisema.
Alisema Lowassa alishindwa kuutumia mkutano huo kueleza sera na vipaumbele vyake.
Mohammed alisema wananchi wengi hawajawa na uelewa wa kutosha wa siasa na kwamba wanachofanya ni mhemko wa kisiasa.
No comments:
Post a Comment