KIONGOZI Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akihutubia wananchi wakati wa mkutano wa ufunguzi wa kampeni uliofanyika jana kwenye viwanja vya Zakhem, Mbagala, Dar es Salaam. |
MSHAURI Mkuu wa ACT Wazalendo, Profesa Kitilya Mkumbo akihutubia wananchi wakati wa mkutano huo |
CHAMA cha ACT Wazalendo kimezindua kampeni za urais na kuwataka Watanzania kutomchagua kiongozi mwenye tabia za kikabila, udini na ukanda.
Pia kimewaomba wananchi kutomwuunga mkono mgombea urais mwenye uwakala na matajiri, huku akishindwa kutamka vita dhidi ya kupambana na mafisadi.
Chama hicho kimesema kiongozi mwenye sifa za kuiongoza nchi anapaswa kuzingatia misingi ya demokrasi ndani na nje ya chama chake.
Kama mgombea akiwa amechaguliwa kiujanja ujanja kwa kulaghai ili apate mafaniko ya haraka, hapaswi kuongoza nchi.
Katika uzinduzi huo uliofanyika jana kwenye viwanja vya Mbagala Zakhem, Mshauri wa ACT, Profesa Kitila Mkumbo, alisema Tanzania haimhitaji rais mbabaishaji.
Alisema mgombea mwenye tabia ya kutaka mafaniko ya haraka, yeye na chama chake wanapaswa kuogopwa kwa sababu hawana nia nzuri na taifa.
“Tunamtaka kiongozi ambaye hata katika chama chake awe amepatikana kwa msingi ya kidemokrasia na si ujanja ujanja wa kutaka mafaniko ya haraka,” alisema.
Profesa Kitila alisema madai ya kuwa rais si mtendaji bali anapaswa kuunda timu ya watu wa kumsaidia, alisema nchi haitafuti ofisa miradi, bali kiongozi mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kutoa dira ya taifa.
MCHANGE AWAVAA UKAWA
Meneja Kampeni wa ACT, Habibu Mchange, alisema wananchi waliogope kundi la UKAWA kwa sababu ni la mafisadi waliojificha kwa kusema uongo.
Alisema Agosti 15, mwaka 2007, katika viwanja vya Jangwani, uliokuwa umoja wa vyama vya upinzani ulitangaza majina ya watu 11 ambao walidaiwa kuwa mafisadi.
Katika orodha hiyo iliyoitwa ‘list of shame” alidai kuwa ilitiwa saini na viongozi wa vyama hivyo. wakiwemo Freeman Mbowe wa CHADEMA, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi pamoja na Augustino Mrema wa TLP.
Alisema kuwa kwenye majina hayo, mgombea urais kupitia CHADEMA, ambaye pia ni waziri mkuu akiyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa alitajwa.
Alisema inashangaza kuona viongozi hao wa UKAWA ambao waliwaambia wananchi kuwa Lowassa ni fisadi, leo wanamshabikia na kumwuunga mkono.
Mchange aliwasihi wananchi kuwa makini na UKAWA kwa kuwa ni kundi la mafisadi lililojificha kwa mwamvuli wa vyama vya upinzani.
Kwa upande wake, kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, alisema Watanzania wasidanganyike kwa kuwa hakuna mabadiliko kutoka kwa viongozi ambao awali walikuwa wakiendeleza mambo yasiyokuwa na manufaa kwa umma.
Alisema endapo chama hicho kikipata ridhaa ya kuongoza nchi, watawashughurikia mafisadi hao.
Akizungumzia vipaumbele vya ACT, mgombea urais wa chama hicho, Anna Nghwira, alisema wataunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Alisema serikali watakayoiunda itahusisha makundi na watu wenye kutaka maendeleo ya nchi kwa uzalendo.
Alisema katika kuunga mkono harakati za mwasisi wa taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, makao makuu ya serikali yatahamia Dodoma
No comments:
Post a Comment