Monday, 31 August 2015

DK. MASSABURI ATANGAZA NEEMA JIMBO LA UBUNGO



NA RACHEL KYALA

MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Didas Massaburi, ameahidi kutatua kero zilizoshindikana kutatuliwa na mbunge aliyepita, ikiwemo maji, miundombinu na  huduma za jamii,  iwapo atapewa ridhaa ya kuliongoza jimbo hilo.

Aidha amesema atatoa sh. milioni 10 kwa kila kata katika jimbo hilo, ili zikopeshwe kwa wanawake, wajasiriamali na walemavu kwa riba nafuu na kujaza fedha katika vikoba vyote, ili watu wengi wanufaike.

"Zikijumlishwa na zile sh. milioni 10  alizoahidi kwa kila kata mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, iwapo mtampa kura zenu, maisha yenu yataboreka," alisema.

Dk. Massaburi, alisema hayo jana, Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa kampeni  kwa jimbo la Ubungo.

"Iwapo mtanichagua, nitafanya hivyo kwa kutumia akili, rasilimali, nguvu na kutafuta wafadhili ili kuhakikisha kila mtaa unapata maji kwa kipindi cha miaka miwili hadi mitatu ijayo," alisema.

Dk.Massaburi alisema atahakikisha serilali za mitaa kupitia manispaa, zinarekebisha sheria kama alivyoahidi Dk.Magufuli, ili wajasiriamali na bodaboda wasisumbuliwe na askari wa jiji.

"Nitaboresha miundombinu ya Kinondoni kwa kuwekea barabara zote lami, ili kurahisisha usafiri, kama ambavyo nimeanza kwa kusimamia vema ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo kazi (DART), uzoefu ninao.

Kuhusu mitaro ya maji machafu katika jimbo hilo, Dk. Massaburi, aliahidi kurekebisha, hususani 'Mto Sinza' ambao umekuwa kero kwa muda mrefu kiasi cha  kuleta mafuriko.

Pia aliahidi kuimarisha masoko yote katika kila kata, ili wafanyabiashara wa barabarani kupata nafasi nzuri ya kufanyia biashara jirani na maeneo wanayoishi.

Dk.Massaburi aliahidi kusimamia ilani ya CCM ili kuhalikisha wananchi wananufaika. Aliwataka Watanzania kuichagua CCM katika nafasi zote za udiwani, ubunge na urais.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo, aliwataka wananchi kuichagua CCM kwa kuwa hakuna mgombea wa upinzani katika nafasi yoyote anayeweza kuwaletea maendeleo ya kweli.

No comments:

Post a Comment