NA STEPHEN
BALIGEYA
MTAALAMU wa
elimu ya jamii wa Kiingereza, H.Spencer (1820-1903), aliwahi kueleza kuwa wanadamu
wa rangi nyeusi wamejaliwa kuwa na akili isiyoweza kujizamisha katika uwazaji
mtupu.
Akili yake
Mwafrika kwa kadri ya Spencer ni akili iliyojifungia katika mitokezo tu. Katika
hali hiyo, akili yake Mwafrika hutegemea hisia zaidi kuliko mawazo.
Kwa msingi
huo, akili ya Mwafrika hushindwa kupokea fikra za kifalsafa, fikra ambazo ni
daraja la juu.
Kwa kuzingatia,
mantiki na dhana ya Spencer, tunaweza kutumia hisia na sisi kuona kwamba, Mwingireza
huyu alitukana sana Waafrika na Bara la Afrika kwa ujumla. Lakini ukijaribu
kutafakari kwa kina, unaweza kuhitimisha kwamba, kuna ukweli kuntu juu ya
mtazamo wa Spencer.
Tatizo la Spencer
katika mtazamo wake huo, ni kuwajumuisha Waafrika wote kuwa katika kundi la
watu wanaotumia hisia kufikiri au kuwaza na badala yake kujizamisha katika
kutumia hisia.
Kimsingi, Spencer
alitakiwa kueleza kuwa baadhi ya Waafrika, kwa kuwa si Waafrika wote wenye
hulka za kujizamisha katika kufikiri au kuwaza kwa hisia bali wapo wenye fikra
pana, ambao wanatumia akili kuwaza mambo mazito na kuibua fikra mpya.
Mifano ya
wanadamu au Waafrika weusi, ambao wameibua fikra mpya na ambao wamebaki kama
wanafalsafa wa kuigwa katika Bara la Afrika ni pamoja na Mwalimu Julius Nyerere,
Kwame Nkrumah, Nelson Mandela, Martin Luther King, kutaja kwa uchache.
Pamoja na kutoa
mtazamo huo wa kiujumla wa Spencer lakini haiondoi ukweli uliomo hasa kwa
kutazama maisha ya mwanadamu bila kujali rangi yake, kabila, nchi au ukanda
atokao. Ukweli unabaki kwamba dhana ya kutumia akili kuamua na kufikia
hitimisho la maana, huambatana na tafakari ya kina, ambayo huchangiwa na
utulivu na ushirikishwaji mzuri wa akili.
Mtu ambaye hawezi kutumia akili kufikiri na
badala yake, kutumia hisia na hivyo kujiona amejenga hoja za mawaa, hana sifa
nyingine zaidi ya kile kinachoweza kuitwa upumbavu na ulofa.
Uhakika na
uhalisia huo wa Spencer, ulidhihirika siku ambayo, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
ulipozindua kampeni zake katika Viwanja, vya Jangwani, Dar es Salaam, Jumamosi
ya Agosti 29, 2015.
Kila Mtanzania
mpenda maendeleo alisubiri kwa hamu
kutaka kujua ni vitu gani murua ambavyo umoja huo ungekuja navyo ili kuvilinganisha
na vile vya CCM, ambao nao walizindua kampeni zake katika viwanja hivyo.
Kusema kweli,
kitu muhimu ambacho Watanzania walikishuhudia au kukisikia, kipo katika dhana
na mantiki ya Spencer, kwamba akili yake Mwafrika hutegemea hisia zaidi kuliko
mawazo.
Ilidhihirika
kabisa kwamba, kati ya viumbe weusi ambao wanapatikana katika Bara la Afrika, hasa
katika ukanda wa Jangwa la Sahara, katika
nchi ya Tanzania, ambao wameingia katika dhana na mantiki ya Spencer, ni
aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Frederick Sumaye.
Sumaye
kadhihirisha kile kilichoelezwa na mwanafalsa huyo wa Kiingereza, ambaye
aliungwa mkono na Mwingereza mwenzake, aitwaye Hegel, ambaye alisema kuwa Afrika
imezama katika giza, ambapo akili yake haijafika kwenye kiwango cha fikra pembuzi
au fikra jumla.
Kwa kuwakumbusha
ni kwamba Sumaye huyu wa Ukawa, wakati yupo CCM alipita katika makanisa, kwenye
kumbi za harambee na matamko lukuki kupitia vyombo vya habari kwa kujipambanua
kwamba anachukia rushwa na ufisadi, kiasi cha baadhi yetu kushawishika naye na
kumtakia harakati njema za safari za kwenda kutokomeza rushwa na ufisadi kama
angefanikiwa kuingia Ikulu.Kumbe tulikuwa kwenye kundi lile alilolizungumzia
Spencer.
Ni Sumaye huyu
tuliyeamini kwamba anamaanisha anachokisema kuhusu Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya
Richmond, Edward Lowassa, kwa kutuaminisha kwamba ni mchafu na fisadi mkuu.
Ni Sumaye
huyu, ambaye alifikia hatua na kutishia kwamba, kama CCM ikimteua Lowassa yuko
tayari kuhama chama hicho. Tena ni Sumaye huyu, ambaye alishiriki kwa namna
kubwa kuhakikisha Lowassa hapitishwi na CCM.
Leo ni Sumaye
huyu, ambaye anachukua jukumu la kumsafisha Lowassa kwa tuhuma alizoshiriki
kumtuhumu mwenyewe kwa lengo la kumwandalia njia ya kuingia Ikulu. Kuna mpango
gani hapa kwa Taifa letu? Wanapanga mkakati gani wakishaingia Ikulu? Kutakuwa
na usalama kwa viongozi vigeugeu wa namna hii?
Tena Sumaye
huyu akakazia kwamba, CCM wameshiriki katika kumchafua Lowassa ili kumkosesha
nafasi aliyotaka. Kama CCM walishiriki kumchafua Lowassa, Sumaye alikuwa nani
na kwa nini alishiriki kumchafua Lowassa? Kwa nini Waziri Mkuu Mstaafu
alishirki kudanganya umma kwamba Lowassa hafai?
Kwa nini Sumaye
alishiriki kutumia makanisa na sehemu za harambee kumkashifu mtu ambaye alijua
ni msafi na anaonewa kwa sababu za kutaka kwenda Ikulu? Kwa nini Sumaye
aliwadanganya viongozi wa dini wa makanisa hayo aliyotembelea kuwaaminisha
kwamba Lowassa anatafuta madaraka kwa rushwa?
Ni lini Sumaye
katubu dhambi ya uongo, uzandiki na upuuzi mkubwa wa namna hii, kiasi cha kuliambukiza
taifa ugonjwa wa ‘Lowasalism’, kwamba Lowassa ni mtu hatari kwa mustakabali wa
taifa hili?
Kwa nini Sumaye
huyu alishiriki kuuaminisha umma kwamba, taifa haliwezi kuchagua kiongozi ambaye
anatumia mapesa yake kwenda Ikulu? Sumaye alijuaje kwamba Lowassa anatumia
mapesa?
Sumaye hajui
kwamba Watanzania wengi walimwamini kutokana na nafasi aliyowahi kuishika kwa
kuwaaminisha kwamba Lowassa ni fisadi na mtu anayetafuta madaraka kwa kutumia
nguvu ya fedha?
Kwa nini
Sumaye anakuwa laghai kwa Watanzania na wakati huo huo anataka Watanzania
wamwone mtu makini na mwenye uchungu na taifa hili kama si ulaghai wa kisiasa?
Kwa nini Sumaye
ameamua kuchezea akili za Watanzania kiasi cha kuwafanya wajinga na watu wasio
na akili za kuwaza mbali kwa mujibu wa mwanafalsafa Spencer?
Tena katika
kuonyesha kiwango cha uduni wa fikra wa Sumaye, anawaambia Watanzania kwamba,
Lowassa alijitoa mhanga kumwokoa Rais na serikali, maana mwenye mamlaka ya juu
ni rais mwenyewe.
Hivi huyu
alikuwa waziri mkuu wa Tanzania kweli au kuzimu? Hivi wakati masuala ya
Richmond yanatokea alikuwa mzima huyu au alikuwa milembe akitibiwa?
Lowassa
mwenyewe kakiri kwamba alisaini mkataba kwa kuamini simu ya msaidizi wake. Je, tumwonee
huruma Lowassa kwamba msaidizi wake alimdanganya kwamba rais kamtuma?
Pili, tangu
lini suala la kusaini mkataba wa maslahi ya taifa kama huo ukaamini simu tena
ya msaidizi wako tu kama kweli wewe ni kiongozi makini na si fisadi na jizi la
mali za umma lililokubuhu?
Hoja ya
kwamba rais ndo mwenye mamlaka, na hivyo Lowassa alitekeleza kile alichotaka
bosi wake ambaye ni rais haina mantiki. Je, wakati Lowassa anasaini mkataba huo
wa kifisadi alikuwa kashikiwa bunduki?
Hoja za kipumbavu
na kilofa hizi zinatakiwa kutolewa kweli na watu wa aina ya Lowassa na Sumaye,
maana mtu makini na anayetambua maana ya kufikiri kwa kina hawezi kutoa majibu mepesi
kwenye maswali magumu.
Wakati Augustino
Mrema anajiondoa CCM mwaka 1995 akiwa Naibu Waziri Mkuu, alipingana na kile
alichoona hakina maslahi ya umma. Akaona kuliko kushiriki uovu akaamua kuachia
ngazi na kuondoka chamani.
Hapa kwa
watu wenye akili (sidhani kama Sumaye na Lowassa watakuwemo), wanatambua
kwamba, Mrema alionyesha uzalendo kwa taifa na kwa watu wake. Je, kwa nini Lowassa
hakuachia ngazi badala yake kushiriki uovu kama kweli alikuwa na mapenzi na Watanzania?
Kwa nini
hakuondoka CCM baada ya tukio hilo na badala yake alisubiri kukatwa? Hivi Sumaye
na Lowassa wasingekatwa wangetwambia upuuzi huu ambao wanausema leo? Hivi Sumaye
anaposema rais ndo mhusika mkuu, nani alisaini mkataba? Mshikwa na ngozi si ndo
mwizi?
Ikitokea
akapelekwa mahakamani atajitetea vipi wakati alisaini yeye kwa mkono wake kama
hajaenda kuungana na Babu Seya wake? Tuna akili sisi au tumerogwa?
Kwa vile,
Samweli Sitta, ameomba mdahalo na Lowassa juu ya ukweli wa Richmond, ni wakati
sasa Lowassa kujitokeza na kukubali mdahalo huo kama kweli anataka tumwamini
yeye na Sumaye wake.
Kwa sasa
nimetambua bila shaka, kile alichokieleza Rais Mstaafu Benjamini Mkapa kwamba,
watu wa aina ya Sumaye, ambao walikuwa serikalini tena kwa nafasi za uwaziri
mkuu leo kujidai wanataka kulikomboa taifa hili ni upumbavu na malofa.
Nimekubali
bila shaka kwamba, Sumaye ni lofa ambalo halitengamani sana na mantiki ya Spencer
kwamba bado anaishi katika ulimwengu wa giza wa kutumia hisia kufikiri na kuwaza,
kwa sababu bado hana mwanga katika kichwa chake.
Pia, kwa
sasa nimetambua kwa nini Watanzania walimwita Sumaye Mr. Zero. Hakika nimeamini
kwa nini Sumaye baada ya kukaa kwenye uwaziri mkuu kwa miaka 10, lakini hakujua
umasikini wa Watanzania unasababishwa na nini mpaka alipokwenda kusoma nje ya
nchi.
Watanzania
wanatakiwa kukumbuka kwamba, ni Sumaye huyu aliyetuongoza kwa miaka 10
alipostaafu na kwenda kusoma na aliporudi akawaeleza waandishi wa habari
kwamba, hakujua umasikini wa Watanzania unasababishwa na nini ila baada ya
kusoma ametambua.
Fikra hizi
za giza za kutumia hisia zimekuwa mwendelezo wa kile alichokizungumza juzi na
hivyo kutaka kufanya Watanzania wajiunge katika kundi la wapumbavu ambao pamoja
na kukaa madarakani miaka 10 bado ni maziro kichwani.
Dhana na mantiki
ya Sumaye kusema kwamba, sasa anatambua umaskini wa Watanzania unasababishwa na
nini, ilikuwa gia ya kuutafuta urais, ambao ameutaka siku nyingi.
Ni upuuzi
mkubwa unakuwa waziri mkuu kwa miaka 10 eti hujui chanzo cha umasikini wa watu
wako. Haya ni matusi na bila shaka tusingekuwa na fikra za hisia, huyu
tungekwisha mshughulikia siku nyingi.
Matusi ya
namna hii ndiyo aliyoeleza Watanzania juzi kwamba, Lowassa anasingiziwa uchafu
wake, wakati ni yeye aliyehusika kumchafua. Upumbavu na ulofa wa kiasi gani
huu?
Katika
kujitoa ufahamu ama kutekeleza malengo maalumu, Sumaye anadai kwamba ugonjwa si
tatizo, maana hata Dk. Magufuli anaumwa, Kikwete anaumwa na pia Mkapa akiwa
rais aliwahi kuumwa na kwenda kutibiwa nje.
Kwa msingi
huo, Sumaye hataki tuhoji afya ya Lowassa, anataka tushuhudie na tuchague rais
ambaye tukimtuma kwenda kuwakilisha
taifa letu nje ya nchi kwenye masuala muhimu ana uwezo wa kuzungumza dakika 10
tu.
Uwendawazimu
na ulaghai huu wa Sumaye, unataka kuungana na shahada aliyosomea Lowassa
mwenyewe, ambaye anatambua kwamba, kwa nafasi anayoomba, hawezi kuhimili bali
tamaa ya madaraka tu.
Lazima Sumaye
atambue kwamba, afya ya rais ni mali ya taifa na si mali yake. Kama bado
hajatambua hili arudi shule Chuo Kikuu
cha Havard ambako huwa akienda angalau anafanikiwa kuongeza ufahamu wa fikra.
Afya ya rais
ni mali ya umma, ni mali ya umma kwa sababu fedha atakazotumia kujihudumia ni
mali ya umma, kwa mantiki hiyo, lazima Watanzania wajue afya ya rais wao.
Hatuwezi
kujitia upofu wa tamaa ya madaraka na ukanda, eti afya ya rais si tatizo tena
kwa hoja za kijinga kwamba Ikulu haendi kubeba zege. Rais ni zaidi ya meneja
kama anavyotaka Sumaye tuamini, urais ni taasisi nyeti ambayo Watanzania lazima
wapeleke mtu anayewadumia kwa ufasaha.
Hatuwezi
kuchagua mtu ambaye maisha yake yatakuwa Ujerumani, kwa hoja dhaifu kwamba,
hata kama hatakuwepo shughuli za serikali zitaendelea. Sasa tuna haja gani ya
kuchagua rais mgonjwa wakati tunajua shughuli za serikali zitaendelea?
Kwa nini
tutumie rasilimali za taifa kuhangaika na taasisi ambayo, hata kama haipo
shughuli za serikali zitaendelea? Sumaye lazima atambue kwamba, ujinga wake si
ujinga wa Watanzania, pia atambue kwamba, unaweza kuwaghilibu Watanzania kwa
muda na si kwa wakati wote.
Nimeshajua
kabisa kwamba, Sumaye yupo katika ulimwengu wa giza la kufikiri hivyo ingekuwa
vigumu kwake kutambua kwamba Rais Kikwete ni meneja au kiongozi mkuu wa nchi.
Pia, ni
vigumu Sumaye kutambua kama Nyerere, Mwinyi na Mkapa walikuwa mameneja wa taifa
letu au viongozi wakuu wa nchi, ambao ni zaidi ya fikra zake za giza ambazo
zinasubiri kupatiwa mwanga akienda kusoma nje.
Kama ambavyo
anasema ndani ya CCM kuna mizengwe, hivi Sumaye huyu ni wa kuzungumza habari za
kuwepo mizengwe ndani ya CCM? Ni nani atashindwa kuungana na Spencer kuthibitisha
kiwango cha kufikiri kwa hisia cha waziri mkuu huyu mstaafu?
Ni Sumaye
huyu ambaye mwaka 2000 wakati wa uchaguzi mkuu aliwahi kutamka kwamba, mfanyabiashara
ambaye anataka kufanikiwa, lazima ajiunge na CCM? Kati ya CCM na Sumaye nani
alionyesha mizengwe hapa?
Si ni Sumaye
huyu ambaye anatambua kwamba kukwamishwa kwake kupata Ujumbe wa Halmashauri Kuu
ya CCM Taifa ilichangiwa na mizengwe aliyofanyiwa na Lowassa? Kuna siri gani
sasa kuungana na mtu aliyekuwa anamfanyia mizengwe ndani ya CCM?
Sumaye anataka kutufanya watu wote tufikiri
kwa kutumia hisia kama yake na kugeuza kazi ya kichwa kuwa ya makalio na ya makalio
kuwa ya kichwa?
Sumaye amejiondoa
pia, ufahamu na kuibuka kwamba, wanaomsema Lowassa kwa rushwa na ufisadi ni
walaghai na wanafiki, kwa kuwa tangu aondoke, serikali ya Rais Kikwete
imekumbwa na madhila mengi.
Ni kweli,
kumetokea kashfa mbalimbali ambazo zimelitikisa taifa, Je, tunataka kuhalalisha
uchafu wa mtu mwingine kumsafisha mchafu mwingine? Yaani unashiriki kuua na
unakimbia kwenda kwa watu nje na kujifanya hujashiriki kuua na kuanza kutaja
majina ya wauaji wenzako?
Huu nao ni
uwendawazimu au upumbavu na ulofa kwa mujibu wa Mkapa. Maana wizi au ufisadi wa
Lowassa unabaki wake kama yeye na taifa lazima lihoji uadilifu wa viongozi wake
bila kujali uchafu wa chama au taasisi nyingine.
Hata Marekani
na Uingereza zenye demokrasia zina matatizo lukuki, lakini kitu muhimu ambacho
wanakitazama ni uadilifu wa kiongozi wanayetaka awaongoze. Hawawezi kuhalalisha
uchafu wa kiongozi aliyepita ili kumpata mwizi na fisadi mwingine.
Sumaye anataka
kuhalalisha maovu yaliyotokea, hivyo kuwa karata ya kupeleka mwovu mwingine Ikulu.
Viongozi wa namna hii huwa najiuliza waliupataje uwaziri mkuu?
Sumaye
anajitoa ufahamu kabisa kwamba, katika kipindi chake ndipo ndege ya rais
ilinunuliwa, tena kwa laana, wale waliotwambia tule majani leo wako gerezani? Kiburi
hiki cha Sumaye kina maanisha nini?
Ni Sumaye
huyu akiwa waziri mkuu ndipo iliponunuliwa radar kwa bei ya kuruka kiasi cha
Tanzania kurudishiwa chenji. Sumaye huyu ambaye leo anajitwisha jukumu la kumsafisha
fisadi aliyemtuhumu mwenyewe ujasiri huu unatoka wapi?
Wenye akili
wametambua bila shaka, kwamba, mkakati ni kuungana kikanda katika kuiteka nchi.
Pia, mkakati ni kuunganisha nguvu za kidini ili kuhakikisha anapatikana rais
kama ambavyo huku mitaani tunasikia.
Kama fikra
hizi ndizo ziko kwenye kichwa cha Sumaye, basi sina maneno matamu ya kumwambia
zaidi ya kumfananisha na kile alichosema Spencer kwamba, fikra zake zinaishia
kuhisi kuliko kuwaza. Pia, naungana na kile alichokisema Mkapa kwamba, watu wa
namna hii ni wapumbavu na malofa.
Tafakari!
No comments:
Post a Comment