NA
CHRISTOPHER LISSA
UZINDUZI
wa kampeni za umoja
usio rasmi wa katiba ya wananchi (UKAWA) uliofanyika juzi, viwanja vya
Jangwani, jijini Dar es Salaam, ni
kielelezo tosha kwamba umoja huo ni kundi dogo la wababaishaji dhaifu wenye nia rasmi ya kurubuni na kupotosha umma
wa Watanzania.
Kwa kiswahili cha mtaani, huu ni usanii wa wazi ambao
viongozi wa UKAWA wanawafanyia Watanzania kwa nia ya kuwapanda mabegani ili waweze kuingia Ikulu.
Inaashangaza
kuona kuwa wafuasi wa umoja huu wana macho, lakini hawaoni, wana masikio lakini hawatathmini nyimbo za kisanii wanazoimbiwa.
Wana akili
lakini hawatambui kabisa kuwa
wameingizwa ndani ya jumba kubwa la
sanaa na wasanii.
Moja ya
mambo yanayothibitisha udhaifu mkubwa wa
UKAWA ni wanachama kutokuelewa wanalolifanya na wanalofanyiwa na viongozi
wao. Ni kama waliofanyiwa mazingaombwe
ya kutokujielewa.
Wafuasi hao
wanatumia muda na nguvu nyingi kujikusanya
kwa wingi ili kushindana na wafuasi wa CCM. Watanzania hawataki kuona umati. Wanataka
kusikiliza sera za msingi.
Yaliyojiri
katika uzinduzi huo ni kielelezo tosha
kwamba umoja huo unaongozwa na kundi dogo la wababaishaji dhaifu wenye nia thabiti
ya kurubuni na kuupotosha umma wa Watanzania.
Jambo la
kushangaza zaidi ni udhaifu mkubwa wa hoja katika mikutano hiyo.
Yaani ni vichekesho tupu. Kwa kimombo tunaita ‘komedi’.
Umati wa
watu uliofika katika uzinduzi wa UKAWA,
ulikuwa na matumaini makubwa kwamba viongozi wao wangekuwa na hoja za
haja za kuwaeleza.
Waswahili
wanasema ukishangaa ya Musa utaona ya Firauni. Hivi wenzangu mlielewa nini cha
msingi kiliochojiri na kuzungumzwa na UKAWA?
Katika
historia ya mambo ya siasa hapa duniani,
sijawahi kushuhudia mgombea urais,
ambaye anadai eti yuko kwenye harakati za kuleta mabadiliko, halafu anawaambia wafuasi wake hawezi kuhutubia,
badala yake wasome hotuba hiyo kwenye tovuti. Huu ni udhaifu.
Hivi wafuasi
wa UKAWA kusoma hamjui, hata picha halisi ya aina ya mgombea wenu, Edward
Lowassa hamuioni?
Hali yake
hamuioni? Hata anavyosimama na kwenda
kwenye kizimba cha kuhutubia hamuitathmini kabisa?
Hata
anavyosimama mbele yenu na jinsi anavyoongea
hammuoni? Hata kutoka kwa sauti yake kwenye vipaza sauti hamuisikii?
Hivi tangu Lowassa aingie UKAWA ni lini aliwahi
kuhutubia wafuasi wake walau kwa dakika
hata 20 tu na kuzungumza hoja zenye
mashiko? Hoja zinazomaanisha kwamba ni
mtu aliye kwenye harakati za mabadiliko?
Inashangaza
kwa mtu mzima kama Frederick Sumaye,
kujibebesha udaktari wa kujua ukweli wa
afya ya Lowassa na kuthubutu kutamka mbele ya wafuasi kwamba eti afya ya Lowassa
haina maana kubwa kwa sababu yeye anaenda Ikulu kuwa meneja tu.
Hivi Watanzania
kweli tunahitaji meneja Ikulu? Wafuasi
wa UKAWA mnampigia kura Lowassa ili awe meneja wa Watanzania Ikulu? Haya ndiyo
mabadiliko mnayoyataka?
Emmanuel Makaidi, naye
na uzee wake alipewa nafasi ya
kuhutubia, lakini badala ya kujenga
hoja alianza kusifia uzuri wa Lowassa.
Eti ni
mweupe, ana nywele nyeupe, yuko safi! Toba!
Tena bila aibu wafuasi wanashangilia.
Mgombea
mwenza, Juma Haji Duni, kama kawaida
alipopanda jukwaani, aliendeleza
mipasho yake. Huyo siku zote hana jipya. Hata uwaziri wa afya katika serikali
ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ulimshinda.
Mtu ambaye
alitegemewa kujenga hoja UKAWA, alikuwa James Mbatia. Lakini ajabu ni kwamba aligeuka mwimbaji wa kwaya. Wakati wananchi wanasubiri kusikiliza hoja za
nguvu, Mbatia alitumia muda mwingi
kuimbisha watu kwaya jukwaani. Huu si usanii jamani?
Wafuasi wa UKAWA
wakawa na matumaini makubwa kwamba Lowassa
atalipuka kisawasawa.
Ndiyo siku
yake ya ‘kufunguka na hata pengine kujisafisha na kashfa chafu ya Richmond.
Ajabu
Lowassa alihutubia kwa kubabaikababaika huku akitamka ‘peoples’,
salamu ya CHADEMA mara nyingi.
Mgombea
huyu alithubutu kuwaeleza wafuasi wake
kwamba hotuba yake wakaisome kwenye tovuti.
Ni ajabu kwa
UKAWA kushangilia mtu anayeongea pasipo na hoja za msingi.
Eti Lowassa
anaahidi kumtoa ‘Babu Seya’ jela
pamoja na masheikh wa Zanzibar. Hivi ni vitu ambavyo havina mantiki kwa jamii
ya wale wanaojiita wana mabadiliko.
Kumtoa Babu
Seya jela ndiyo mabadiliko wanayoyataka UKAWA?
Ajabu ni kwamba wanashangilia hoja dhaifu na zisizo na mashiko. Hoja
mbovu, zilizochoka na zisizo na mbele wala nyuma.
Utamkuta mfuasi
wa UKAWA anatoka kijasho chembamba akiwa
katikati ya umati wa watu, wakati hakuna chochote ambacho viongozi wake
wanamweleza kikakaa akilini.
Hivi wafuasi
wa UKAWA wanajitambua kweli? Naweza
kusema pengo la Willbroad Slaa na
Profesa Ibrahim Lipumba, kutokuwepo kwenye majukwaa ya umoja huo limeanza
kuonekana. Watu ambao angalau walikuwa wanajenga hoja za haja kiasi kwamba
wakipanda jukwaani, mambo wanayozungumza
yanaingia akilini.
Watanzania
mnapaswa kutafakari.
No comments:
Post a Comment